KIPA wa Tanzania Prisons, Musa Mbisa amezungumzia kitu kilichoongezeka kwa msimu huu akiamini sasa kuwa matukio mengi wakati wa mechi yametawaliwa na ufundi na hilo linafanya timu zijipange kupambania pointi.
Ametolea mfano wa mechi dhidi ya Mbeya City waliyoifunga mabao 2-1 namna ilivyokuwa imetawaliwa na matukio mengi ya kiufundi na kilichoamua wamalize dakika 90 kwa kuvuna pointi tatu ni kuzidiana kimbinu.
“Nilichojifunza kwa upande wangu kama kipa nisipuuze mpira wa aina yoyote kwa kudhani unaweza ukadhibitiwa na beki kwa sababu ufundi na mbinu za washambuliaji vimeongezeka,” amesema Mbisa na kuongeza: “Mechi zikitawaliwa na ufundi siyo kitu rahisi kupata ushindi iwe ugenini ama nyumbani. Kwa maana nyingine kila mchezaji anapaswa kujifunza vitu vipya na kuwa makini muda wote anaokuwepo uwanjani.”
Amesema kwa nafasi anayocheza inamlazimu kila baada ya mechi kupata muda wa kuangalia wachezaji hatari na kuongeza mbinu za kudhibiti kushambuliwa.
“Washambuliaji wanasoma upungufu wa makipa ili kujua wapite njia gani ili kufunga. Vivyo hivyo kwa makipa tunatakiwa kuwasoma ili isiwe rahisi kutufikia,” amesema. Katika mechi nne iliyocheza Prisons imeshinda mbili na kufungwa mbili ikivuna pointi sita na kipa Mbisa anamiliki ‘clean sheet’ moja.