Kocha Fountain Gate aomba mechi ya moja tu

KOCHA wa Fountain Gate, Mohamed Laizer ameomba mechi moja ya kirafiki ili kukipima kikosi chake kabla ya kukutana na Pamba Jiji.

Ikumbukwe kwamba mwezi uliopita ulikuwa wa neema kwa kikosi hicho kwani kimechukua tuzo mbili – Laizer akibeba ya kocha na Juma Issa ya mchezaji bora.

Akizungumza na Mwanaspoti, Laizer amesema wake anaona ilikuwa sawa kwao kupewa tuzo hizo kwa kuwa walistahili kutokana na kile ambacho wamekifanya.

Amesema sasa hawana muda tena wa kutazama nyuma na kwamba wanaelekeza nguvu kwenye kazi iliyopo mbele yao.

“Nimewaambia wachezaji wangu kwamba tuzo ya kocha bora ni yao kwa namna walivyojituma kwenye mechi za hivi karibuni,” amesema Laizer.

“Nimeomba kwa uongozi ikiwezekana kabla ya kuvaana na Pamba Jiji tupate mechi moja ya kirafiki na timu iliyopo Ligi Kuu ambayo itakwenda kuwaweka wachezaji fiti zaidi.”

Aliongeza kuwa, “mipango na nguvu zote zipo kwa wapinzani wetu Pamba Jiji kwa sababu sio timu ya kuibeza kulingana na ubora walionao.”

FountainGate imecheza mechi sita ikiwa imeshinda mbili, sare moja na kupoteza tatu ikivuna pointi saba.

Timu hiyo itakaribishwa Mwanza na Pamba Jiji Novemba 23 katika Uwanja wa CCM Kirumba kuanzia saa 10:00 jioni.