Samia: Sitachoka kunyoosha tena mkono wa maridhiano

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema ingawa dhamira yake ya maridhiano wakati wa muhula wake wa kwanza wa uongozi ilikatishwa na baadhi ya wadau, katika awamu hii hatachoka kunyoosha tena mkono wa kufanikisha hilo.

Katika muhula huo, Rais Samia amesema alikuja na falsafa ya R4 ili kuliunganisha Taifa. Serikali ilionyesha utayari wakati wote kuleta maridhiano ili kwa pamoja kulijenga na kulitunza Taifa.

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo, Ijumaa Novemba 14, 2025 alipozungumza wakati wa hotuba yake ya kulifungua Bunge la 13, jijini Dodoma.

“Katika muhula wa kwanza wa awamu ya sita, tulikuja na falsafa ya R4 ili kuliunganisha Taifa. Serikali ilionyesha utayari wakati wote kuleta maridhiano ili kwa pamoja tujenge na kulitunza Taifa letu.

“Serikali ilinyoosha mkono na kuwakaribisha vyama vya siasa, sekta binafsi na hata jumuiya za kimataifa ili kwa pamoja tuijenge Tanzania,” amesema.

“Kwa kuwa wananchi wa Tanzania wamenipa ridhaa ya kuendelea kuiongoza nchi hii, sitachoka kunyoosha tena mkono wa maridhiano. Ni matumaini yangu kuwa wadau wa kisiasa wataupokea kwa dhati mkono wa maelewano ili kwa pamoja tujenge mazingira mwafaka kwa Taifa letu,” amesema.

“Tutajifunza kutokana na makosa na mapungufu ya taasisi zetu za kidemokrasia, Tanzania ina uzoefu wa miongo mingi ya demokrasia na amani. Tanzania ina demokrasia iliyokomaa. Hata hivyo tunaendelea kuboresha kulingana na mazingira wakati. ni jukumu letu kujielekeza kwenye maboresho hayo kwa utashi wetu bila shinikizo lolote,” amesema.

Ameyaomba makundi yote ya Watanzania hasa vyama vya siasa, wakae pamoja, kuzungumza, kuangalia walipokosea, kujirekebisha na kwenda kwenye safari ya Taifa lenye amani na utulivu.

“Haya yatafanyika kwa kufuata mila na desturi zetu, miongozo yetu, kanuni zetu, mitindo yetu ya maisha na sio kwa shinikizo,” amesema.