Pantev atoa msimamo mzito Simba, mastaa wajipange!

SIMBA inaendelea kujifua kujiandaa na mechi mbili za kimataifa za Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Petro Atletico ya Angola na Stade Malien ya Mali, huku kocha wa timu hiyo, Dimitar Pantev akitoa msimamo kwa mastaa wote kabla ya mechi hizo na nyingine zijazo za Ligi Kuu.

Wekundu wa Msimbazi waliopangwa Kundi D lenye Esprance ya Tunisian pia, itaikaribisha Petro wikiendi ijayo kabla ya kuifuata Malien kisha kusubiri mapema mwakani kumaliza na wababe wa Tunisia nje ndani kuwania nafasi ya kutinga robo fainali ya michuano hiyo ya Caf.

Lakini wakati kikosi kikijifua kwa mechi hizo na za Ligi Kuu, Pantev amewapiga mkwara mastaa wa timu hiyo, hakuna mwenye uhakika wa namba kwa sasa na badala yake kila mmoja apambane na hali yake ili kupata nafasi ya kutumika kikosini.

Pantev aliyeiongoza Simba katika mechi tatu, zikiwamo mbili za raundi ya pili ya CAF na moja ya Ligi Kuu, aliliambia Mwanaspoti, kila mchezaji ana nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza, kutokana na kiwango atakachokionyesha mazoezini na kuzaa matunda mechi za mashindano.

PANT 01


Kocha huyo aliyetambulishwa na mabosi wa Msimbazi kama Meneja, japo katika makabrasha akisomeka tofauti anafanya kazi akishirikiana na Seleman Matola, alisema kila mchezaji ana nafasi sawa na mwingine, jambo analoamini litatengeneza ushindani wa kweli.

“Hatutoi nafasi kwa mchezaji kutokana na ukubwa wa jina lake, kinachoangaliwa ni utendaji wake wa kazi utakaofanikisha timu kufikia malengo yake, kifupi hakuna mwenye uhakika wa namba katika kikosini changu,” alisema Pantev na kuongeza;

“Jambo lingine tunaangalia mechi inayokuwa mbele yetu inahitaji wachezaji wa aina gani ambao watahakikisha timu inavuna pointi tatu, hivyo tutaandaa timu kulingana na mipango halisi na si kitu kingine.”

PANT 02


Katika mechi ya Ligi Kuu dhidi ya JKT Tanzania, Pantev aliwaanzishia benchi mfungaji bora wa msimu uliopita, Jean Charles Ahoua na Jonathan Sowah kabla ya kuwaingiza kipindi cha pili na kuisaidia timu hiyo kushinda mabao 2-1, la ushindi likiwekwa kimiani na Sowah mwenyewe.

Kocha huyo raia wa Bulgaria na aliyetua Msimbazi akitokea Gaborone United ya Botswana iliyotolewa na Simba katika mechi za raundi ya kwanza msimu huu alisisitiza;

“Kila mtu unayemwona katika timu lengo ni moja tu, la kupigania nembo ya Simba kuwa mfano wa kufanya vizuri Ligi ya ndani na michuano ya CAF, ndiyo maana tunatengeneza ushindani ambao kila mechi itakuwa rahisi kufanikisha mipango yetu.”

PANT 03


Pantev alisema usawa kwa wachezaji ndiyo silaha ya umoja wao, kuhakikisha kila mmoja anajisikia ni muhimu katika timu, hilo analiamini litatengeneza ushindani halisi.

“Ndiyo maana ni muhimu kwa makocha kumjua kila mchezaji uwezo alionao na namna ya kumsaidia ili kuwa katika ubora, kuwajenga kiakili kupambania ndoto zao ziwe katika uhalisia, hivyo Simba tunajenga kwa pamoja,” alisema Pantev katika mechi tatu alizoiongoza timu hiyo imeshinda zote na kuiingiza timu makundi na katika ligi ikishika nafasi ya pili ikiwa na pointi 9.