YANGA inaendelea kujiimarisha kabla ya kuanza kwa mechi za hatua ya makundi itakapoanzia nyumbani na kama unataka kujua nini kinachoendelea, basi ishu iko hivi. Huko kambini kwa sasa Kocha Pedro Goncalves amekuja kivingine akisaka dawa ya kuwanyoosha Waarabu.
Wawakilishi hao wa Tanzania katika Ligi ya Mabingwa Afrika imepangwa Kundi B na timu tatu kutoka Ukanda wa Afrika Kaskazini maarufu kama Waarabu, Far Rabat ya Morocco, JS Kabylie ya Algeria na Al Ahly ya Misri na itaanza kibarua wiki ijayo dhidi ya Far, visiwani Zanzibar.
Katika kuhakikisha wanafanya vyema dhidi ya timu hizo za Waarabu, Pedro ambaye ni raia wa Ureno amewabana mastaa wa timu hiyo kwa mazoezi makali kisha kinapigwa uwanjani huko akiwasilisha ombi moja muhimu kwa mabosi wa klabu hiyo.
Iko hivi. Kocha Pedro ameendelea kukomaa na kikosi hicho na anachofanya kwanza ni kuendelea kuishibisha pumzi na stamina timu yake ikipata dozi kale inayosimamiwa na yeye mwenyewe pamoja na wasaidizi wake wawili.
Yanga inaendelea na mazoezi bila ya kocha wa viungo Tshephang Mokaila aliyerudi kwao Botswana kumuuguza mama mzazi ambaye hata hivyo, alipoteza maisha na jamaa alibaki huko kumalizia msiba huo mzito.
Hata hivyo, wakati Yanga ikiendelea kupiga hesabu namna ya kumleta kocha mpya wa viungo au kurejea kwa Mokaila, mambo hayajasimama kwani Pedro ameendelea kushusha dozi akiwa na wasaidizi wa Filipe Pedro na Patrick Mabedi.
Jana asubuhi kikosi hicho kilirudi gym asubuhi katika mwendelezo wa mazoezi hayo na kilijifua huko kwa takribani saa mbili na nusu, wakiimarisha miili zaidi, kisha jioni kinapigwa uwanjani wakihamia eneo lingine.
Uwanjani Pedro amekuwa anataka kuona mipango ya kucheza soka lao ikiendelea kuimarishwa huku akiwa mkali akitaka kuona hesabu za kufika langoni na kufunga zinafanyika sawasawa bila uzembe.
Mazoezi hayo ya kuucheza sana mpira yameonyesha kuwavutia zaidi wachezaji wa Yanga wakionekana kama wanainjoi sana, huku kocha huyo na wasaidizi wake wakitaka kuona pasi zinapigwa lakini mara mpira unapopotea unatafutwa kwa nguvu.
Pedro baada ya kuwapigisha kazi wachezaji ili kupata stamina na mbinu za kuikabili FAR Rabat itakayoumana nao kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar fasta amewaomba mabosi wa timu hiyo kumtafutia mechi moja wa kirafiki wa kuwapima wachezaji kwa mazoezi waliyofanya hadi sasa tangu wacheze mara ya mwisho dhidi ya KMC na kupata ushindi wa mabao 4-1.
Mechi hiyo mbali na kutaka kupima mazoezi hayo, lakini Pedro anataka kuwarudishia ubora wa ushindani ambao anataka uchezwe kesho Jumapili na siku hiyo kutakuwa na ratiba ya mechi hiyo pekee kisha wachezaji watapumzika.
Hesabu za Yanga ni kutaka kuondoka Jumanne ijayo Novemba 18 ili kwenda Zanzibar kuendelea na maandalizi zaidi kabla ya kukutana na AS FAR Rabat.
Taarifa kutoka Yanga zinadokeza, wachezaji wanne waliopo kikosi cha Taifa Stars watarejea nchini kesho mara baada ya mechi dhidi wa Kuwait, kisha kundi la pili litarejea Jumanne wakati kikosi hicho kikiondoka na wengine wawili kumalizia Jumatano.