RAIS SAMIA AONYESHA DIRA YA YA KUMARISHA KASI YA UTEKELEZAJI MAENDELEO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesisitiza umuhimu wa kuimarisha kasi ya utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya Taifa ili kutimiza kwa wakati malengo ya kitaifa.

Taarifa iliyotolewa na Naibu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu Bw. Shaaban Kissu imesema Rais Dkt. Samia ameyasema hayo leo wakati wa hafla ya kumuapisha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb.) kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, iliyofanyika Ikulu Chamwino.

Katika hotuba yake, Rais Dkt. Samia amempongeza Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba, akibainisha kuwa uteuzi wake umefanyika kufuatia tathmini ya kina ya sifa na uwezo alionao, hususan ufanisi wake katika kuwahudumia wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Vilevile, amemtaka Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba kusimamia kikamilifu utekelezaji wa miradi na programu za maendeleo zilizopo na kuongeza kasi ya utekelezaji na ufuatiliaji wa karibu wa shughuli za Serikali ili malengo ya Serikali yatimie kwa muda uliopangwa.

Halikadhalika, Rais Dkt. Samia amemtaka Waziri Mkuu kufanya kazi kwa kutanguliza maslahi ya nchi na bila upendeleo.