Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Dodoma
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan ametoa rai kwa vijana wa Taifa hili wasikubali hata siku moja kushawishiwa kuichoma nchi yao wenyewe na kusisitiza wasikubali kukata tawi la mti ambao wameukalia.
Akizungumza leo Bungeni Mjini Dodoma alipokuwa akizindua Bunge la Tanzania la 13,Rais Dk.Samia ambaye ametoa muelekeo wa masuala mbalimbali yatakayotekelezwa na Serikali ya Sita ametumia nafasi hiyo kuelezea uvunjifu wa amani uliotokea Oktoba 29 mwaka huu.
“Pamoja na kuwa uchaguzi umefanyika kumewepo na uvunjifu wa amani ambao umesababisha uharibifu wa mali na upotevu wa maisha na kuharisha usalama wa nchi.
“Tunapoenda mbele niwasihi sana watanzania tuongozwe na dhamira ya maelewano ,ushirikishwaji ,kujirekebisha na umoja.
“Kwa wanangu vijana wa Taifa hili la Tanzania nchi hii imejengwa kwenye misingi ya amani na utulivu wa kisiasa.Sisi wazazi wenu tungeshawishika kufanya mliyofanya wakati huu nchi hii isingekuwa na neema na maendeleo mnayoyaona leo.
“Nataka kurudia hilo kwa wanangu vijana wa Taifa la Tanzania sisi wazazi wenu kama tungefanya mliyoyafanya ninyi nchi hii isingekuwa na neema na maendeleo mnayoyaona .
“Hivyo niwasihi sana wanangu vijana wa Tanzania .Nchi hii ni yenu ,shida zozote zinazowakabili msikubali hata siku moja kushawishiwa kuichoma nchi yenu wenyewe .Msikubali kukata tawi la mti ambao umekalia.”



