Wanaofanya ukatili kidijitali waonywa | Mwananchi

Dar es Salaam. Wakati zikiwa zimesalia siku chache kabla ya kuanza kwa siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia duniani zinazoanza Novemba 25 hadi Desemba 20, Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), kimeonya ukatili wa kijinsia mtandaoni unaofanywa na watu wenye nia ovu.

Ukatili kwa wanawake na wasichana mtandaoni kama kusambaza picha/video za faragha bila ridhaa, kufichua taarifa binafsi kama namba za simu, kuunda kurasa feki, kauli za chuki, matusi na ubaguzi umetajwa kusababisha madhara kwa kundi hilo.

Hayo yote yamebainishwa leo Ijumaa Novemba 14,2025 jijini Dar es Salaam katika hafla ya uzinduzi wa mradi wa #SautiZetu ambao ni mradi wa Tamwa kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Ujerumani GIZ.

Mradi huo wenye lengo la kupaza sauti ili kuzuia, kupunguza ukatili wa kijinsia na kutoa elimu kwa kutumia vyombo vya habari utatekelezwa katika maeneo ya Temeke, Kinondoni, Tanga na Dodoma kwa kutoa elimu kwa kinamama pamoja na wanafunzi na jamii kwa ujumla.

Akizungumza Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Dk Rose Reuben amesema ipo haja kubwa ya kuwasaidia wanawake na watoto dhidi ya madhila ya ukatili unaofanyika mtandaoni ambapo Tamwa na GIZ kwa pamoja wanapaza sauti, ili kuwasaidia wanawake na watoto dhidi ya ukatili huo wa kidijitali.

“Ukatili wa mtandaoni unawaathiri wanawake na watoto sambamba na makundi mengine kwa kiasi kikubwa kwani kundi hili bado halina uelewa wa kutosha wa kujilinda na kulinda taarifa zao.

“Tamwa kwa uzoefu na kwa tafiti tulizowahi kufanya tumebaini kuwa faida na hasara za matumizi ya dijitali ni sawa na shilingi yenye pande mbili, kwani wanawake na watoto wanatumia vifaa vya kidijitali na kupata faida lukuki lakini kwa upande mwingine mitandao ya kidijitali inawaathiri,” amesema.


Kiongozi huyo amesema ikirejewa kauli mbiu ya maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, mwaka huu inasema: Siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia 2025: Maliza ukatili wa kijinsia kupitia majukwaa ya kidijitali kwa wanawake na wasichana wote’.

Amesema Tamwa inasisitiza wanawake na watoto wanapaswa kulindwa dhidi ya ukatili huu wa kidijitali kwa kuwa kumeshuhudiwa madhara ya afya ha akili na kimwili yanayosababishwa na matumizi yasiyo sahihi ya mitandao.

Tamwa hata hivyo imesema wasichana wadogo wanaotumia mitandao ya  WhatsApp, TikTok na Snapchat wapo katika hatari kubwa zaidi huku athari zake zikiwa ni kifo, kutengwa, kukosa haki athari za kisaikolojia.

Wakati Dk Rose akizungumza hayo, Mkuu wa huduma za ustawi wa jamii jijini Dar es Salaam,  Waziri Nashiri amesema jamii inapaswa ikumbuke kuwa ipo sheria ya makosa ya mtandao ya mwaka 2015 ambayo kimsingi inashughulika na wale wote wanaotenda makosa ya namna hiyo.

Akieleza zaidi amesema upo mpango kazi wa Serikali unaoenda hadi mwaka 2029 ambao unasisitiza kuimarisha malezi, kukuza kipato cha kaya ili kuondoa njaa kwa watu kwa sababu imegundulika chanzo cha watu kufanya ukatili mtandaoni wengine wanashawishiwa kutokana na njaa waliyonayo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Wanawake katika maendeleo la Wajiki, Janeth Mawinza amesema kila mmoja anapaswa kutoa mchango wake ikiwemo kuelimisha jamii ili kupambana na ukatili.

“Kuna vituo vya One stop Center wapeleke huko matukio ya ukatili kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi. Tunataka kuhakikisha kila mtu anakuwa na furaha anatumia jinsia yake bila ubaguzi kutoka kwa mwingine.

Kwa upande wake Meneja mtekelezani wa mradi huo ambaye ni mwakilishi wa GIZ, Nora Loehr amesema katika utekelezaji wa mradi huo vyombo vya habari vina jukumu kubwa la kuelimisha jamii sambamba na kuinua uelewa juu ya vitendo vya ukatili wa kijinsia hasa vinavyofanyika mitandaoni.

Amesema mradi unahitaji juhudi za wanahabari, wanaharakati, pamoja na watu wote katika kumaliza ukatili wa kijinsia wenye athari hasi kwa watendewa ambazo zinaanzia kwenye kuumiza hisia.

Amesema ukatili wa kijinsia kwenye mitandao ya kijamii athari zake zinaenda hadi kiafya na wakati mwingine kusababisha kifo.