Kesi ya ‘Dk Manguruwe’, yaiva, DPP aruhusu isikilizwe Kisutu

Dar es Salaam. Upelelezi katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili, Mkurugenzi wa Kampuni ya Vanilla International Ltd, Simon Mkondya(40), maarufu   Dk Manguruwe, umekamilika.

Wakili wa Serikali, Frank Rimoy ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo Novemba 14, 2025 wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Mkondya na mwenzake, Rweyemamu John(59), ambaye ni Mkaguzi wa fedha wa kampuni hiyo, wanakabiliwa na mashtaka 28 yakiwemo ya kuendesha biashara ya upatu na utakatishaji fedha linalomkabili Mkondya peke yake.

Kwa upande wa mshtakiwa wa pili ambaye ni John, yupo nje kwa dhamana baada ya kwenda kuomba dhamana Mahakama Kuu na pia hana mashtaka ya kutakatisha fedha.

Rimoy ametoa taarifa hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki baada ya kesi hiyo kuhamishiwa kwa hakimu huyo.

“Mheshimiwa hakimu, kesi hii imeitwa leo kwa ajili ya kutajwa na upande wa mashtaka tunapenda kuitaarifu Mahakama yako kuwa, upelelezi umekamilika na tunaomba itupangie tarehe kwa ajili ya kumsomea hoja za awali( PH), na kisha tuanze kusikiliza ushahidi wa upande wake wa mashtaka” amesema Wakili Rimoy.

DPP awasilisha hati ya kuruhusu Mahakama ya Kisutu isikilize kesi hiyo.

Wakati huohuo, upande wa mashtaka umeieleza Mahakama hiyo kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini( DPP) amewasilisha mahakamani hapo hati ya kuiruhusu Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kusikiliza kesi ya uhujumu inayomkabili Mkondya na mwenzake.

Kwa kawaida kesi zote za uhujumu uchumi husikiliza Mahakama Kuu, pindi upelelezi unapokamilika kwenye mahakama ya chini, ambapo washtakiwa/ mshtakiwa husomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo( Committal Proceedings) na kisha kesi hiyo huamishiwa Mahakama Kuu, ambapo hupangiwa tarehe ya usikilizwaji na Msajili wa Mahakama Kuu.

Lakini kama DPP atawasilisha hati ya kuiruhusu Mahakama husika kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi, basi kesi husika haitapelewa Mahakama ya Juu ( Mahakama Kuu), badala yale  itasalia Mahakama husika kwa ajili ya usikilizwaji na ndicho kitakachofanyika katika kesi ya ‘Dk Manguruwe’.

Hakimu Nyaki baada ya kusikiliza taarifa hiyo, alipanga Novemba 17, 2025 kwa ajili ya Jamhuri kuwasomea hoja za awali( PH).

“Pia siku hiyo ya Novemba 17, 2025 baada ua Jamhuri kuwasomea washtakiwa hoja za awali, siku hiyohiyo tutaanza kusikiliza ushahidi, hivyo ni vizuri mkatambua siku hiyo mje na shahidi” amesema Hakimu Nyaki.

Kesi kusikilizwa mfululizo siku 14

Awali kesi hiyo ilikuwa inasikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Anna Magutu, lakini leo kesi hiyo imehamishiwa kwa Hakimu Nyaki.

Hakimu Nyaki aliwapa taarifa washtakiwa hao kuwa kwa sasa kesi hiyo itakuwa inasikilizwa kwake na sio kwa hakimu Magutu.

” Hakimu Magutu amekuwa na kesi nyingi za mrundikano ambazo zinatakiwa kusikilizwa mfululizo na kikao cha Mahakama kilichokaa hivi karibuni kilielekeza baadhi ya kesi zilizopo kwake zihamishiwe kwa mahakimu wengine ili ziweze kusikilizwa mfululizo” amesema Hakimu Nyaki na kuongeza.

“Hata kesi ya kwenu imepangwa kusikilizwa mfululizo kwa siku 14 kuanzia Novemba 17 hadi Novemba 28, 2025 na huu ni utaratibu uliyowekwa kwa kesi zote za muda mrefu za  kuanzia mwaka 2024 kurudi nyuma” amesema hakimu Nyaki.

Mshtakiwa Simon Mkondya, maarufu kama ‘Dk Manguruwe ‘ akiwa chini ya ulinzi wa askari Magareza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Picha na Hadija Jumanne



Mkondya aomba Jamhuri imtafutie wakili wa kumtetea

Baada ya upande wa mashtaka kudai kuwa upelelezi umekamilika, mshtakiwa Mkondya amedai kuwa leo ameandika barua ya 11 ya kuomba kufanya majadiliano na DPP ya kuimaliza kesi hiyo.

Mkondya ambaye anaonekana kupungua mwili wake tofauti na siku aliyofikishwa mahakamani hapo.

Leo akiwa amevalia fulana ya mikono mirefu rangi ya bluu yenye mistari miwili myeupe na udongo iliyozunguka kifuani hadi mgongoni huku mkononi akiwa ameshika daftari kubwa linalotumiwa na wanafunzi wa sekondari pamoja na karatasi na kalama, Mkondya alionyoosha mkono juu mara kadhaa akiomba kapewe nafasi ili kuwasilisha maombi yake kwa hakimu.

Hakimu alipompa nafasi ya kuongea, mshtakiwa huyo alianza kwa kuomba ameshaandika barua 10 za kufanya majadiliano na DPP ya kuimaliza kesi lakini barua hizo hazijajibiwa mpaka sasa.

“Mheshimiwa hakimu, wiki iliyopita Mwanasheria aliniambia upelelezi ukikamilika niandike barua nyingine, hivyo leo nimeandika barua ya 11 ya kufanya majadiliano na DPP ya kuimaliza kesi na nimeshaikabidhi kwa watu wa Magereza,”amedai   Mkondya na kuongeza:

“Na tayari nimeshaandika barua sita za kuomba majibu ya barua zangu nilizoandika za kukiri mashtaka na kupunguziwa adhabu na DPP,  lakini mpaka sasa hazijajibiwa” amedai Mkondya.

Hakimu Nyaki amemueleza mshtakiwa huyo kuwa licha ya kuandika barua hiyo, kesi hiyo inaedelea na usikilizwaji huku mshtakiwa huyo akiendelea kufanya majadiliano na DPP ya kuimaliza kesi hiyo.

Mbali na hilo, Mkondya ameiomba Mahakama hiyo kama kuna uwezekano asaidiwe kupatiwa wakili wa kumtetea katika kesi yake.

“Mheshimiwa hakimu, kama kuna uwezekano wowote Jamhuri  inisaidie kunipatia wakili, ambaye atanitetea katika kesi yangu, kwa sababu sina hela ya kumlipa wakili” amedai.

Vilevile mshtakiwa huyo ameomba apewe dhamana ili awe wakati wa usikilizwaji wa kesi yake.

Akimjibu maombi yake, Hakimu Nyaki alimueleza kuwa kesi inayomkabili ina mashtaka ya kutakatisha fedha ambayo hayana dhamana kwa mujibu wa sheria. Hivyo hawezi kupata dhamana.

Kuhusu Serikali kumtafutia wakili wa kutetea, Hakimu Nyaki alimueleza kuwa Serikali inatoa wakili wa kumtetea mshtakiwa kama anakabiliwa na kesi ya mauaji na si  ya uhujumu uchumi aliyonayo mshtakiwa huyo.

Kwa mara ya kwanza washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Novemba 5, 2024 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi namba 31523 ya mwaka 2024.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, kati ya mashtaka hayo 28,  19 ni ya kuendesha biashara ya upatu na mashtaka tisa ni ya kutakatisha viwanja.

Katika moja ya mashtaka hayo kuendesha biashara ya upatu, washtakiwa wanadaiwa  kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba Mosi,2023, jijini Dar es Salaam, walitenda makosa hayo

Inadaiwa kuwa Mkondya akiwa kama Mkurugenzi wa kampuni hiyo na John akiwa  Mkaguzi wake waliendesha  biashara ya upatu kwa kuwaahidi watu watapata pesa mara mbili hadi  tatu kama faida zaidi ya waliyotoa.

Washtakiwa hao wanadaiwa kujipatia kiasi cha Sh92.2milioni kutoka kwa watu 19 tofauti ambao walitoa kiasi tofauti cha fedha kwa kuwaahidi kuwa watapata faida mara mbili hadi tatu ya fedha walizotoa.

Katika mashtaka tisa ambayo ni ya utakatishaji fedha yanayomkabili Mkondya pekee yake, inadaiwa kuwa kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba Mosi, 2023 akiwa katika mkoa wa Dar es salaam na akiwa kama Mkurugenzi wa Kampuni hiyo alijipatia jumla ya viwanja tisa vilivyopo katika kitalu namba AB eneo la Idunda mkoani Njombe.

Pia, Mkondya anadaiwa kujipatia viwanja hivyo huku akijua viwanja hivyo ni mazalia ya makosa tangulizi ya kuendesha biashara ya upatu.