Rais Samia aanika safari ya maridhiano

Dar es Salaam. Siku 17 baada ya machafuko yaliyosababisha vifo na majeruhi wakati wa uchaguzi, Rais Samia Suluhu Hassan ametoa mwelekeo wa Serikali katika kurejesha mshikamano wa kitaifa, akitangaza hatua mahususi iza kuchukua.

Miongoni mwa hatua hizo ni kuundwa kwa tume maalumu kuchunguza chanzo cha machafuko ya Oktoba 29, 2025 na kuanzisha mazungumzo ya maridhiano.

Akianza hotuba yake kwa wito wa kusimama dakika moja kuwaombea waliopoteza maisha, Rais Samia amesema Serikali ina wajibu wa kuhakikisha nchi inarejea kwenye utulivu, haki na umoja.

“Mimi binafsi nimehuzunishwa sana na tukio lile. Natoa pole kwa familia zote zilizopoteza wapendwa wao na tunamuomba Mwenyezi Mungu awapumzishe kwa amani. Aidha, kwa majeruhi tunawaombea wapone kwa haraka na kwa wale waliopoteza mali zao tunawaomba wawe na stahamala na uvumilivu.”

Rais Samia amesema hayo leo Novemba 14, katika hotuba wakati wa kufungua rasmi Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, jijini Dodoma.

Mbali ya hayo, ametangaza msamaha kwa vijana waliofikishwa mahakamani kwa kesi za uhaini kwa kufuata mkumbo wa kushiriki kwenye maandamano na vurugu.

“Kuna wakati vijana hufuata mkumbo wa uhalifu kwa ushabiki, ninatambua kwamba vijana wengi waliokamatwa na kushtakiwa kwa makosa ya uhaini hawakujua wanachokifanya. Nikiwa mama na mlezi wa Taifa hili, ninavielekeza vyombo vya sheria na hasa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuangalia kiwango cha makosa yaliyofanywa na vijana wetu,” amesema na kuongeza:

“Kwa wale ambao wanaonekana walifuata mkumbo na hawakudhamiria kufanya uhalifu wawafutie makosa yao.”

Oktoba 29, wakati wa uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na Rais yalifanyika maandamano yaliyoambatana na vurugu kuanzia Dar es Salaam na baadaye mikoa ya Arusha, Mwanza, Mara, Mbeya, Geita, Dodoma na Songwe. Zaidi ya watu 500 wengi wao wakiwa vijana wamefikishwa mahakamani kwa makosa mbalimbali yakiwamo ya uhaini.

Hata hivyo, Samia katika hotuba iliyodumu kwa saa 1:32 aliyoianza saa 9:48 jioni hadi 11:20 jioni, amesema Tanzania imejengwa kwenye misingi ya amani na utulivu wa kisiasa.

“Kwa wanangu, vijana wa Taifa hili la Tanzania, niseme kuwa nchi hii imejengwa kwenye misingi ya amani na utulivu wa kisiasa. Sisi wazazi wenu tungeshawishika kuyafanya mliyoyafanya wakati huu, nchi hii isingekuwa na neema na maendeleo mnayoyaona leo,” amesema na kuongeza:

“Niwasihi sana wanangu, nchi hii ni yenu, kwa shida zozote zile zinazowakabili, msikubali hata siku moja kushawishiwa kuichoma nchi yenu wenyewe. Msikubali kukata tawi la mti ambalo mmelikalia. Hili nawaomba mlikatae kwa nguvu zenu zote. Ninyi ndio walinzi na wajenzi wa Taifa hili, nawasihi kamwe msije kuwa wabomoaji wa Taifa lenu.”

Vilevile, amesema Serikali yake imefikiria kuanzisha wizara kamili itakayoshughulikia mambo ya vijana ndani ya Ofisi ya Rais, badala ya kundi hilo kuwa sehemu ya idara ndani ya wizara yenye mambo mengi.

Amesema kufanya hivyo, kunalenga kuwafanya vijana wapewe kipaumbele katika ushirikishwaji kwenye masuala ya maendeleo yao.

“Natambua kumekuwa na majukwaa mengi ya kuwafikia vijana, ila bado shughuli zao zinafifishwa na masuala ya kisiasa na majukwaa hayo kupoteza malengo na mvuto kwa vijana,” amesema.

Pamoja na kuwa na wizara hiyo, amesema anafikiria kuwa na washauri wa masuala ya vijana ndani ya ofisi yake.

Samia amesema: “Ndugu zangu Watanzania, tujifunze kutokana na mapito yetu, hapana shaka kwamba Tanzania ni nchi inayofuata misingi ya kidemokrasia, ila demokrasia kamili inaweza kutafsiriwa kwenye mitazamo tofauti”

“Kama Taifa tunaendelea kujifunza na kujirekebisha. Hivyo basi, sote kwa umoja wetu tunapaswa tuitumie fursa hii tuendelee kujifunza, tujirekebishe na tukubaliane jinsi ya kuiendesha nchi yetu kidemokrasia kwa kuzingatia tamaduni, mila na desturi zetu na siyo za kuletewa,” amesema.

Samia amesema ilani ya CCM ya mwaka 2025 hadi 2030, imeagiza moja ya hatua itakayofikisha kwenye maelewano hayo ni marekebisho ya Katiba.

“Serikali imeahidi kuanza kulifanyia kazi suala la mabadiliko ya Katiba ndani ya siku 100 za muhula wa pili wa awamu ya sita kwa kuanza na Tume ya Usuluhishi na Maelewano,” amesema.

Amesema ingawa dhamira yake ya maridhiano wakati wa muhula wake wa kwanza wa uongozi ilikatishwa na baadhi ya wadau, katika awamu hii hatachoka kunyoosha tena mkono wa kufanikisha hilo.

“Katika muhula wa kwanza wa awamu ya sita, tulikuja na falsafa ya R4 ili kuliunganisha Taifa. Serikali ilionyesha utayari wakati wote kuleta maridhiano ili kwa pamoja tujenge na kulitunza Taifa letu,” amesema na kuongeza:

“Serikali ilinyoosha mkono na kuwakaribisha vyama vya siasa, sekta binafsi na hata jumuiya za kimataifa ili kwa pamoja tuijenge Tanzania.”

Ameeleza mkono huo ulileta matumaini kwa nchi kabla ya baadhi ya wadau kuamua kuachilia au kuutupa mkono huo.

“Kwa kuwa wananchi wa Tanzania wamenipa ridhaa ya kuendelea kuiongoza nchi hii, sitachoka kunyoosha tena mkono wa maridhiano. Ni matumaini yangu kuwa wadau wa kisiasa wataupokea kwa dhati mkono wa maelewano ili kwa pamoja tujenge mazingira mwafaka kwa Taifa letu,” amesema.

Samia amesema: “Tutajifunza kutokana na makosa na mapungufu ya taasisi zetu za kidemokrasia, Tanzania ina uzoefu wa miongo mingi ya demokrasia na amani. Tanzania ina demokrasia iliyokomaa. Hata hivyo tunaendelea kuboresha kulingana na mazingira wakati. Ni jukumu letu kujielekeza kwenye maboresho hayo kwa utashi wetu bila shinikizo lolote,” amesema.

Katika hatua nyingine, Rais Samia amewatangazia hali ya tahadhari watumishi na watendaji wa Serikali watakaoshindwa kwenda na kasi ya kuleta mabadiliko chanya kwa wananchi.

Amesema hatasita kuwabadilikia wale wote watakaokwenda kinyume cha kasi ya utendaji wa Serikali yake, inayolenga kuleta maendeleo kwa wananchi. Amesema ahadi zilizotolewa na chama chake wakati wa kuomba kura ni nyingi, hivyo zinahitaji watu wenye kasi kuzitekeleza.

“Niliahidi Serikali nitakayoiunda itawajibika na kuendelea na mageuzi ya sera zinazogusa masilahi na ustawi wa maisha ya wananchi moja kwa moja. Hivyo basi, ni lazima viongozi wa Serikali kwa ngazi zote kuanzia mawaziri hadi maofisa tarafa wawe karibu na wananchi, ili kuweza kufahamu changamoto zao na kuwajibika kwao,” amesema.

Amesema kwa kuwa ahadi zilizotolewa na chama chake ni nyingi, matamanio na matarajio ni makubwa na muda wa kuyatimiza ni mchache, hivyo ipo haja ya Serikali kuongeza kasi ya utekelezaji wa mipango ili kufikia malengo.

“Nayasema haya mapema kwa watendaji waliopo serikalini na wale nitakaowateua wajitayarishe kisaikolojia na wajipange vyema kufanikisha malengo hayo. Wananchi wanahitaji mabadiliko chanya ili kupata maendeleo, hivyo watendaji msipobadilika kuendana na matarajio ya wananchi tutawabadilikia,” amesema.

Ahadi ya Rais Samia kuhusu maridhiano, imekuja simu moja baada ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), kuitaka Serikali iwe tayari kufanya maridhiano kwa masilahi mapana ya Tanzania na wananchi.

Aidha, Baraza hilo katika tamko lake limeeleza kusikitishwa na vurugu zilizotokea Oktoba 29, zilizosababisha watu kupoteza maisha na uharibifu wa mali za umma na za binafsi.

Bakwata kupitia Baraza la Ulamaa, limesema Oktoba 29 kulizuka kundi lililokuwa likiwatisha watu, kupora na kuharibu mali, miundombinu mbalimbali ikiwamo kuchoma vituo vya mafuta, ofisi za umma na za Chama cha Mapinduzi (CCM).

Tamko lililotolewa Novemba 13, 2025 na kusainiwa na Katibu wa Baraza la Ulamaa, Sheikh Hassan Chizenga, limeeleza uhalifu huo uligawanyika katika makundi, wakiwamo waliofurahia na waliochukizwa.

“Kutokana na vitendo vya kihalifu, ililazimu vyombo vya ulinzi na usalama kudhibiti hali na ndani yake kukatokea vifo vya watu wasiokuwa na hatia,” lilieleza tamko hilo na kuongeza:

“Wengine walipata ulemavu wa kudumu, pamoja na uharibifu, wizi na upotevu wa mali, yote haya yakisababishwa na kundi hilo lililokuwa likifanya fujo, wizi na uharibifu mkubwa wa miundombinu.”

Baraza hilo limeitaka Serikali kufanya uchunguzi kwa kina kuhusu vurugu hizo ili kubaini vinara wa kuchochoa vijana wa Tanzania kufanya uhalifu uliosababisha maisha ya watu kupotea.

“Tunaiomba Serikali kuwaangalia kwa jicho la huruma wale wote ambao kwa namna moja au nyingine wamekumbwa na maafa haya na wala hawakuhusika… Katika kipindi hiki tunaisihi Serikali iangalie panapohitajika, kwa masilahi mapana ya nchi yetu. Panapohitaji suluhu pafanyike,” linaeleza Baraza hilo.

Vilevile limesema panapohitaji maridhiano basi Serikali iwe tayari kufanya hivyo kwa masilahi mapana ya Tanzania na wananchi wake.

“Ingawa tunaisihi Serikali suluhu na maridhiano, isiwe ni zawadi wanayopewa wale wanaohusika na kushiriki katika uhalifu huu uliosababisha maafa haya,” linaeleza tamko hilo.