Wabunge wakunwa na kauli ya Rais kuanzisha Wizara ya Vijana

Dodoma. Wabunge wa Bunge la Muungano wametoa maoni kuhusu hotuba ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoitoa leo, Ijumaa, Novemba 14, 2025, wakati akilizindua Bunge la 13, huku wengi wao wakieleza kuwa dhamira ya kuunda wizara mahsusi ya vijana ni hatua muhimu itakayotoa majibu ya changamoto zinazowakabili vijana nchini.

Akizungumza na Mwananchi katika viunga vya Bunge, Mbunge wa Tunduma, David Silinde amesema hotuba hiyo imeleta matumaini makubwa kwa vijana kwa kuonesha mwelekeo mpya wa Serikali katika kushughulikia masuala yao.

Amesema vijana ndiyo kundi kubwa linalopaswa kupewa kipaumbele kutokana na majukumu na changamoto wanazokutana nazo katika kizazi cha sasa.

Wakati akihutubia, Rais Samia amesema asilimia 60 ya Watanzania ni vijana ambao Serikali inapaswa kuwawekea mpango maalumu wa sera na programu zitakazosaidia kuwaendeleza katika nyanja zote.

Hivyo, Silinde amefafanua kuwa kuanzishwa kwa Wizara ya Vijana kutarahisisha utatuzi wa changamoto nyingi zinazowakabili ambazo awali zilikuwa zikishughulikiwa kupitia idara na wizara tofauti.

“Rais ameonesha mwelekeo chanya wenye kuivusha Tanzania. Nimefurahishwa sana na mpango wa kuanzisha Wizara ya Vijana, naamini sasa masuala ya vijana yatashughulikiwa moja kwa moja bila kupotea katika mifumo mingine,” amesema Silinde.

Ameongeza kuwa viongozi watakaoteuliwa kuongoza wizara hiyo wanapaswa kuwa makini katika kutekeleza maono ya Rais Samia ili taifa liendelee kusonga mbele, huku akiwataka kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa ufanisi na uadilifu.

Mbunge wa Manyoni, Dk Stephen Chaya amesema hotuba ya Rais Samia imejaa matumaini, hasa katika kipindi ambacho Watanzania wengi wanatafuta mwanga wa kuboresha maisha yao.

Ametaja kauli ya Rais ya kutamani kuona nyuso za Watanzania zikiwa na tabasamu kama mojawapo ya misimamo iliyomgusa zaidi.

Pia ameunga mkono mpango wa kuanzishwa kwa Wizara ya Vijana akisema utasaidia kupunguza changamoto zilizokuwa zikiongezeka na kuleta wasiwasi kwa jamii.

Kwa upande wake, Mbunge wa Kilosa, Profesa Palamagamba Kabudi amesema hotuba hiyo imejikita katika kujenga umoja, mshikamano na maadili ya kitaifa.

Amesema imeweka wazi mwelekeo wa kulinda mipaka ya nchi na maslahi ya Watanzania, hatua ambayo inajenga heshima na kuimarisha umoja wa kitaifa.

Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari, amesema amefurahishwa na uamuzi wa Serikali kuwatambua vijana kwa kuunda wizara maalumu itakayoshughulikia masuala yao.

 Ametahadharisha kuwa wizara hiyo inapaswa kuongozwa na vijana kuanzia ngazi ya waziri hadi watendaji, ili iweze kutatua changamoto kwa uhalisia na kuelewa mazingira halisi ya maisha ya vijana.

“Wizara ya Vijana isije ikaongozwa na wazee. Vijana ndiyo wanajua kinachoendelea mitaani na watakuwa rahisi kuwafikia wenzao,” amesema Nassari.

Ameongeza kuwa hotuba ya Rais imeonesha kutambua changamoto za ajira miongoni mwa vijana, ambazo kwa sehemu kubwa zilichangia baadhi yao kuvutiwa na matukio ya uvunjifu wa amani wakati wa chaguzi.

Ametoa wito wa kuharakisha uundaji wa wizara hiyo ili vijana na wadau wengine watoe ushauri utakaosaidia katika kupanga mipango yenye tija.

Mbunge wa Nanyumbu, Yahya Mhata amesema kitendo cha Rais Samia kuwaomba wabunge kusimama kwa dakika moja kuwaombea waliopoteza maisha wakati wa maandamano yaliyozua vurugu kimedhihirisha kuwa ni kiongozi mwenye huruma na anayejali wananchi wake.

Amesema amefurahishwa pia na jinsi Rais alivyowakumbuka majeruhi wa vurugu hizo zilizotokea Oktoba 29, 2025, wakati wa uchaguzi mkuu na kuwasamehe baadhi ya waliohusika kutokana na kushawishiwa na kujikuta wakiingia kwenye mkumbo wa kutekeleza vurugu hizo.

Mhata amepongeza pia dhamira ya Serikali ya kutaka kuimarisha Wakala wa Barabara Vijijini (TARURA) ili kuboresha miundombinu ya barabara, hususan maeneo ya vijijini, akisema hatua hiyo itasaidia kuongeza ufanisi katika maeneo ambayo bado hayajafikiwa vizuri na huduma za msingi.

Kwa upande wake, Mbunge wa Ikungi Mashariki, Thomas Kitima amesema hotuba ya Rais Samia imejikita katika kutatua changamoto za vijana, hususan suala la ajira.

Amesema maelezo ya Rais kuhusu uboreshaji wa sekta ya uchukuzi, ikiwemo viwanja vya ndege, yameonyesha namna Serikali ilivyojipanga kuongeza fursa za kiuchumi kwa Watanzania.

Kitima ameongeza kuwa matarajio ya Rais ni kuona Singida inakuwa na uwanja wa ndege ni jambo linaloweza kufungua shughuli nyingi za kiuchumi mkoani humo.

Mbunge wa Simanjiro, James Milya amesema hotuba ya Rais imeelekeza wazi namna ajira milioni nane zitakavyopatikana ndani ya miaka mitano ijayo, jambo ambalo ni faraja kwa vijana wengi wanaotafuta fursa za kujiajiri na kuajiriwa.

Amesema pia hotuba hiyo imegusia kwa kina umuhimu wa kudumisha amani ya nchi kwa kuwataka vijana kutotumika vibaya na watu wenye nia mbaya.

Amepongeza pia mwendelezo wa mjadala wa Katiba mpya na maridhiano ya kitaifa kupitia ajenda ya 4R, akisema ni muhimu kwa wanasiasa kuepuka kupotosha dhamira njema ya Serikali.

Mbunge wa Sengerema, Hamis Tabasamu amesema hotuba ya Rais imebeba masuala mengi muhimu, ikiwemo mapendekezo ya kuboresha maeneo ya kiutawala katika baadhi ya mikoa na wilaya zilizo na ukubwa mkubwa wa kiutendaji.

Amesema Wilaya kama Sengerema yenye kata 47 inahitaji maboresho ili kuongeza ufanisi wa utoaji huduma kwa wananchi, huku akizitaja mikoa ya Tabora, Morogoro, Geita na Kigoma kuwa na changamoto kama hizo.

Kwa ujumla, wabunge hao wameungana kueleza kuwa hotuba ya Rais Samia imeweka dira mpya ya kuimarisha umoja, uchumi na maendeleo ya vijana, huku wakitarajia utekelezaji wake utaleta matokeo chanya kwa Taifa.