Mashabiki wa soka sasa meno yote nje baada ya CANAL+ na SuperSport kutangaza rasmi kuwa wataonesha mubashara michuano ya CAF Total Energies Morocco 2025, moja ya michuano mikubwa kabisa ya soka barani Afrika.
Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa kwa pamoja na CAF, CANAL+ ns SuperSport, msimu huu wa 35 wa mashindano hayo utakaotimua vumbi nchini Morocco utakuwa mubashara kwenye chaneli za CANAL+ na SuperSport baada ya kampuni ya CANAL+ kupata haki za kurusha michuano hiyo kwa kwa nchi za Kiafrika zinazozungumza Kifaransa, Kiingereza, Kireno, na lugha za kienyeji.
Akizungumza baada ya makubaliano hayo Mkurugenzi Mtendaji wa CANAL+ Africa, David Mignot, alisema uhusiano huo una lengo la kuwaletea burudani wapenzi wa soka.

Naye Rais wa CAF, Dkt. Patrice Motsepe, alisema, “Hii ni siku ya kusisimua kwa CAF na kwa soka la Afrika.
Wakati wa michuano hii mikubwa barani Afrika, Waafrika kila mahali — ndani ya bara na katika mataifa ya nje watatazama kwa fahari mashindano haya ambayo ni alama ya ukuu na ubora wa soka la Afrika.
“Msimu uliopita wa michuano hii nchini Côte d’Ivoire, michuano ya AFCON ilivutia takriban watazamaji bilioni 1.5 duniani kote. Tunatarajia msimu huu kuwa na mafanikio makubwa zaidi, na kutazamwa na watu wengi zaidi kote ulimwenguni.”
Watazamaji wataweza kufuatilia matangazo kupitia SuperSport ndani ya DStv, huku wateja wa CANAL+ wakifurahia mechi kupitia CANAL+ Sport na pia kwa huduma ya mtandaoni kupitia programu ya CANAL+ app.
Cha kufurahisha zaidi, michuano hiyo itatangazwa kwa lugha adhimu ya Kiswahili kwa watazamaji wa maeneo ya Afrika Mashariki ambapo kuna wazungumzaji wengi wa Kiswahili.
Matangazo ya CANAL+ na SuperSport ya mashindano haya yatakuwa na safu bora ya wachambuzi maarufu, watangazaji, waelezaji, na nguli wa soka la Afrika, ambao watawasilisha mitazamo yao ya kipekee kuhusu michuano hii.
Mamilioni ya watazamaji wataweza kuwaona mashujaa wao wa Kiafrika wakiwa uwanjani, wakiwemo wachezaji kama Victor Osimhen (Nigeria), Mohamed Salah (Misri), Sadio Mané (Senegal), Ronwen Williams (Afrika Kusini), Riyad Mahrez (Aljeria) na Achraf Hakimi (Morocco).
