TAIFA Stars iliyo chini ya Kocha Miguel Gamondi leo Jumamosi itashuka uwanjani kwa mara ya kwanza kuvaana na Kuwait katika mechi ya kimataifa ya kirafiki itakayopigwa jijini Cairo, Misri.
Kuwait inayokutana kwa mara ya kwanza na Taifa Stars, inashika nafasi ya 135 katika nafasi za viwango vya soka duniani vilivyotolewa na FIFA Oktoba 17, 2025 huku Tanzania ikishika nafasi ya 107.
Gamondi anayeinoa pia Singida Black Stars aliyoivusha makundi ya Kombe la Shuirikisho Afrika kwa mara ya kwanza msimu huu, ni kaimu kocha mkuu wa Stars akichukua nafasi ya Hemed Suleiman ‘Morocco’ aliyeondolewa hivi karibuni na leo ndo anatesti mitambo na timu hiyo.
“Wazo kubwa la kambi hii na mchezo huu wa kirafiki ni kujitambulisha kwa wachezaji, wao kunijua mimi, nami kuwajua wao, pamoja na shirikisho kuona namna tunavyofanya kazi. Ni nafasi nzuri kwangu kufanya tathmini ya baadhi ya wachezaji,” amesema Gamondi na kuongeza;
“Baada ya kurejea mwezi Desemba, tutafanya mchujo mkubwa wa kikosi, tutaendelea kuwaangalia baadhi ya wachezaji kisha tutatoa orodha ya mwisho kuelekea Fainali za Kombe la Mataifa Afrika.”
Katika mechi tano za mashindano yote, Taifa Stars haijashinda hata moja, imefungwa mechi nne kati ya hizo moja ya kirafiki dhidi ya Iran kwa mabao 2-0, mbili zikiwa za kufuzu kombe la Dunia dhidi ya Zambia na Niger bao 1-0 kwa kila mechi huku ya mwisho ikiwa ya CHAN dhidi ya Morocco nayo kwa bao 1-0.
Mechi ambayo Taifa Stars imeambulia sare kati ya tano zilizopita dhidi ya Congo ikiwa ni katika kinyang’anyiro cha kuwania nafasi ya kucheza Kombe la Dunia.
Kama ilivyo kwa Taifa Stars, Kuwait nayo kutoka Asia haijashinda mechi hata moja, imechapwa nne na kutoa sare moja. Katika mechi nne ambazo wamepigwa ya mwisho ilikuwa ya kirafiki dhidi ya kikosi B cha Morocco kwa bao 1-0.
Kuwait imewahi kushika nafasi ya 24 (Desemba 1998) katika viwango vya FIFA ndio nafasi ya juu zaidi kuwahi kushika huku Tanzania 65 (Februari 1995).