Mbuni FC ina jambo lake Championship 2025/26

PAMOJA na kuanza vyema msimu mpya wa Ligi ya Championship, Kocha Mkuu wa Mbuni FC, Leonard Budeba amewataka nyota kutobweteka na msimu ujao ni kuzipeleka Yanga na Simba mkoani Arusha.

Arusha kwa muda mrefu haijawa na timu  Ligi Kuu tangu iliposhuka daraja JKT Oljoro msimu wa 2015/16 kisha kupigwa mnada na wamiliki wa Gwambina FC na sasa matarajio yao ni kwa Mbuni na TMA zinazoshiriki Championship.

Timu hizo zimeonekana kuwa na mwanzo mzuri kwani katika michezo minne zilizocheza, Maafande hao wamekusanya pointi 10 kwa TMA na kuwa nafasi ya tatu na Mbuni ikivuna tisa nafasi ya nne.

Budeba amesema matokeo waliyoanza nayo ni chachu kwao kuendelea kupambana kuhakikisha kila mchezo wanavuna pointi tatu ili kufikia malengo ya kucheza Ligi Kuu na kuwasogezea burudani mashabiki.

Amesema upinzani uliopo msimu huu wachezaji hawapaswi kubweteka akieleza kuwa mchezo ujao dhidi ya Barberian utakaopigwa Uwanja wa Mabatini, mkoani Pwani ni vita nyingine nzito kwao.

“Si matokeo mabaya na hatupaswi kubweteka kwa namna yoyote, kiu yangu ni kuona mashabiki wanapata burudani ya Ligi Kuu msimu ujao, ushindani upo ila lazima tukomae hadi mwisho,” amesema Budeba.

Kocha huyo bora wa mwezi uliopita aliongeza, anajivunia usajili na ubora wa nyota wake, akiomba sapoti kwa mashabiki kuhakikisha Mbuni inashiriki mara ya mwisho Championship na kupanda Ligi Kuu.

Amesema mkakati na mipango ya benchi la ufundi ni kukusanya pointi za kutosha mzunguko wa kwanza ili raundi ya pili iwe ni kufanya mahesabu na kuweza kupanda daraja moja kwa moja.

“Hatutaki play off wala kusbiri presha ya mwisho, tunahitaji kumaliza kazi mapema na kupanda moja kwa moja, tutacheza kwa nidhamu na kuwaheshimu wapinzani.”