JKT v TP Mazembe… Dakika 90 za kuamua

ILE siku ndiyo leo. JKT Queens ina dakika 90 ngumu za kuamua hatma ya kwenda nusu fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake mbele ya TP Mazembe ya DR Congo.

Ni ushindi pekee ndiyo utakaoibeba JKT kuandika rekodi mpya binafsi katika michuano hiyo, kwani sare haitakuwa na msaada kwao kwa pointi ilizonazo kwa sasa.

Hii ina maana, dakika 90 za pambano hilo litakalopigwa kuanzia saa 1:00 usiku zina maana kubwa kwa JKT kwani ni kufa au kupona, la sivyo itarudi nyumbani kuanza msako wa kutetea taji la Ligi Kuu ya Wanawake (WPL), michuano iliyoanza rasmi jana.

Mazembe ndiyo watetezi wa taji hilo, hadi sasa ina pointi tatu, ikiwa ni moja zaidi na ilizonazo JKT yenye mbili, huku kila moja ikiwa imecheza mechi mbili na pambano hilo litakalopigwa kwenye Uwanja wa Suez Canal, mjini Ismailia, Misri utaenda sambamba na lile la vinara wa Kundi B, Asec Mimosas ya Ivory Coast yenye pointi nne dhidi ya vibonge Gaborone United yenye pointi moja tu.

JKT ilianza michuano hiyo ya pili baada ya ile ya mwaka 2023 kwa sare mfululizo dhidi ya Garobone waliotoka nao suluhu, kisha kutoka 1-1 na ASEC Mimosas, hii ikiwa na maana maafande hao wa kike wanahitaji ushindi ili kutinga nusu fainali kwa mara ya kwanzao kwao.

Mwaka 2023 JKT ilimaliza nafasi ya tatu katika msimamo wa kundi A ikikusanya pointi tatu mbele ya mabingwa wa zamani Mamelodi Sundown, Sporting Casablanca.

Hapa tumekuchambulia uchambuzi wa nini wanapaswa kufanya mabingwa hao wa ligi ya wanawake ili kuhakikisha wanaondoka na pointi tatu.

JK 04


Hii ni kama fainali kwa JKT kwani ni mechi ngumu na wanahitaji ushindi pekee ili ndoto yao ya kucheza nusu fainali itimie.

Katika mechi hiyo yenye presha ambayo pia Mazembe inahitaji pointi tatu, JKT inapaswa kuanza kwa kasi kutokana na aina ya mpinzani waliyekutana naye ambaye anaweza kubadilisha mechi muda wowote.

JKT inapaswa kuishambulia Mazembe mapema, kama ilivyofanya mechi iliyopita ilipotangulia kufunga bao la dakika ya nane dhidi ya ASEC Mimosas la Ester Maseke. Bao la mapema linaweza kuivuruga Mazembe na kuwapa JKT morali.

Mabeki wa Mazembe hupenda kupanda juu kusaidia mashambulizi hivyo Kocha wa JKT, Abdallah Kessy kama ataendelea kumtumia Winifrida Gerald na Alia Fikirini ambao wana kasi inaweza kuwa na faida kwenye shambulizi la kushtukia.

Mazembe imekuwa bora kwa mipira ya krosi na pasi za haraka. Wachezaji wa safu ya ulinzi Christer Bahera, Maseke na Anastazia Katunzi wanapaswa kuwa watulivu na umakini wa hali ya juu hasa wakati Mazembe wanaposhambulia na kuwadhibiti washambuliaji hao kwa akili kubwa.

JK 03


Mazembe inawategemea zaidi viungo walionao, hivyo kama JKT itatawala eneo hilo na kulivuruga inaweza kuwa na faida kwao kumaliza kazi mapema.

Donisia Minja, Janeth Pangamwene na Katunzi ambao wanaunda eneo la kiungo la JKT watakuwa na kazi ya ziada ya kuhakikisha viungo wa Mazembe hawapitishi pasi za hatari kwenye lango lao.

Changamoto kubwa iliyoonekana kwa JKT ni katika eneo la kumalizia nafasi wanazozitengeneza kwenye mechi na Gaborone ilizopoteza nafasi tatu za wazi ambazo kama ingezitumia vyema huenda leo presha isingekuwa kubwa.

Hivyo JKT kama itacheza kwa kasi na kupeleka presha kwa wapinzani kama Mazembe kila nafasi unayopata unapaswa kuitumia vyema wakati ambao wamepoteana kabla timu haijapata muunganiko tena.

JK 01


Hadi sasa katika kundi B, mabingwa hao wamecheza mechi mbili na kuonyesha sura mbili tofauti.

Mechi ya kwanza dhidi ya ASEC Mimosas, Mazembe ilianza vibaya ilicheza kwa tahadhari, ikaruhusu ASEC kumiliki mpira, pia ilishindwa kudhibiti eneo la ulinzi kukionekana kuwa na pengo hasa kwenye mipira ya pembeni.

Ilishindwa kutengeneza nafasi nyingi za wazi na mchezo ulionekana kuwa mgumu kwao, ilichelewa kurudi mchezoni baada ya kupitia presha ya Asec.

Mechi ya pili vs Gaborone United, ilioonyesha ubora na Mazembe ilirejea kwa kishindo ikiifunga mabao 3-0 mechi iliyotawaliwa na nidhamu, kasi na umakini.

Mabao waliyofunga walishambulia kupitia pembeni kwa kasi huku wakimiliki mchezo kwa asilimia kubwa ubora wao ulionekana hasa kwenye safu ya mbele.

JK 02


Kocha wa JKT, Abdallah Kessy alisema bado wana matumaini ya kuvuka hatua ya nusu fainali licha ya ugumu wa mechi hiyo.

“Tunajua tunakutana na mabingwa watetezi, lakini malengo yetu ni kuzifunga timu kubwa na kuvuka hatua hii haijalishi ni ugumu kiasi gani lakini tutapigana hadi dakika ya mwisho,” alisema Kessy

“Dosari katika eneo la umaliziaji limekuwa changamoto kubwa na nimezungumza na wachezaji kila nafasi tunayopata tuigeuze kuwa goli.”

Nahodha wa JKT Queens, Anastazia Katunzi alisema hawajakata tamaa na wana imani kuwa kwenye mchezo huo wao watapambana ili kupata matokeo na kusonga mbele hatua ya nusu fainali.

“Tutapambana mechi ya mwisho ili tuwe kwenye nafasi nzuri zaidi, tunajua tuna kazi kubwa ya kufanya na tumekuwa tukiambizana kambini tupambane ili kila mmoja atimize lengio lake.”

                                   P          W         D          L          F          A          PTS

1. ASEC Mimosas    2          1           1           0          2          1           4

2. TP Mazembe        2          1           0          1           3          1           3

3. JKT Queens          2           0          2          0          1           1           2

4. Gaborone United   2          0          1           1           0          3          1

JKT Queens     v TP Mazembe (Saa 1:00 usiku)

Asec Mimosas   v Gaborone Utd  (Saa 1:00 usiku)