Dar es Salaam. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), limekemea vurugu zilizotokea Oktoba 29, 2025, huku likitoa wito wa uchunguzi huru utakaoshirikisha wadau mbalimbali wakiwemo wa kidemokrasia ufanyike.
Mbali na hilo, TEC limetaka watu wote waliokamatwa kabla, wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi kuachiwa huru. Sambamba na hilo, baraza hilo, limekumbushia kuanza kwa mchakato wa Katiba Mpya.
Hata hivyo, jana Ijumaa Novemba 14, 2025 akizindua Bunge na kutoa mwelekeo wa Serikali kwa miaka mitano ijayo, Rais Samia Suluhu Hassan alilani matukio hayo, akisema tayari Serikali imechukua hatua ya kuunda Tume ya kuchunguza yaliyotokea ili kubaini kiini cha tatizo.
“Taarifa hiyo itatuongoza kujielekeza kwenye mazungumzo ya kuleta maelewano na amani,” amesema Rais Samia akiwa bungeni jijini Dodoma.
Leo Jumamosi Novemba 15, 2025 akisoma tafakuri ya pamoja ya Maaskofu wa Kanisa hilo, kufuatia tafakari na sala walizofanya kwa siku nne kuanzia Novemba 11 hadi 14, Rais wa baraza hilo, Askofu Askofu Wolfgang Pisa amesema kanisa linakemea yaliyotokea.
Kwa mujibu wa Askofu Pisa, maandamano hayo yaliyosababisha vurugu yaliyozaa mauaji, watu kujeruhiwa, uharibifu na upotevu wa mali binafsi na za umma, hali iliyowaumiza na kuwasononesha jamii ya Watanzania.
“Tunasikitishwa na kulaani hali hii, haya mauaji … kifupi sote tumejeruhiwa. TEC inatoa pole nyingi sana kwa familia zilizopoteza wapendwa wao, familia hizi zina maumivu,” amesema.
“Tunaendelea kuwaombea majeruhi wapate nafuu haraka na kurudi katika majukumu yao. Neno la Mungu liwe faraja na tulizo, tunawaombea uponyaji wa ndani wale wote walioathirika kiroho, kisaikolojia na kiuchumi,” amesema Askofu Pisa.
Askofu Pisa amesema TEC imetafakari, limefuatilia kwa ukaribu hali halisi ya nchi kabla na baada ya uchaguzi na kubaini Taifa limegubikwa na manung’uniko na kutokuridhika jambo ambalo limewagawa Watanzania ambao wanasifika kuwa kisiwa cha amani na utulivu.
“Hali hii haijengi Taifa letu, hivyo kunahitajika juhudi za makusudi za kulileta Taifa pamoja na kuponya maumivu yaliyopo katika familia zilizopoteza wapendwa wao na sisi sote,” ameeleza.
Katika tafakuri hiyo, Askofu Pisa amesema TEC imeungana na wadau wengine kuomba watu kupatiwa miili ya wapendwa wao ili wakaipumzishe kwa heshima, imani ya dini, mila na desturi na tamaduni zao.
Baada ya tafakuri hiyo, TEC imeziomba mamlaka zinazohusika kuendelee kukemea mauaji yaliyotokea na kukiri ukweli waliouawa ni ndugu wa Watanzania.
“Jitihada za makusudi zifanyike ili haki na ukweli utawala katika Taifa letu. Uchunguzi huru utakaoshirikisha wa ndani na nje ya nchi ufanyike,” amesema.
“Tunapendekeza wadau watoke kwenye Tume Huru isiyofungamana na upande wowote, kama jumuiya na taasisi za kimataifa, taasisi za dini, asasi za kiraia na wataalamu wa haki na mambo ya kidemokrasia,” amesema Askofu Pisa.
Aidha Askofu Pisa ameisihi Serikali kuwa tayari kupokea na kuyafanyika kazi maoni ya ripoti itakayotolewa, akisema mchakato huo unaweza kuwa moja ya hatua muhimu ya kuponya Taifa.
Pia, Askofu Pisa amesema TEC inasisitiza maisha ya uadilifu na uwazi kwa viongozi waliopewa dhamana kuongoza, kuishi maisha ya uadilifu na uwazi, ukweli na uwajibikaji ili kujenga misingi ya kuamiana.
“Wote waliokamatwa kwa hila, kabla, wakati wa uchaguzi na kuwekwa mahabusu kuachiwa huru bila ya masharti yoyote,” amesema Askofu Pisa.
Kuhusu suala hilo, Rais Samia ameshaagiza vyombo vya sheria hasa ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka kuangalia kiwango cha makosa yaliyofanya na vijana hao.
“Kwa wale wanaonekana wamefuata mkumbo, lakini hawakuonekana na dhamira ya kufanya uhalifu, wawafutie makosa yao. Pia, walionekana kufuata mkumbo, lakini hawakudhamiria kufanya uhalifu, wawafutie makosa yao,” alisema Rais Samia.
Katika ya masuala hayo, TEC imekumbushia mchakato wa Katiba Mpya na utawala wa sheria, ikisema kimekuwa kilio cha muda mrefu nchini hivyo unapaswa kuanza.
“Mchakato wa Katiba Mpya yenye kujali utu na usawa, ukweli kwa wote uanze kwa kushirikisha wadau wote ili tusirudi kwenye machafuko na nchi iongozwe kwenye misingi ya utawala wa sheria,”
“Tusikilize wananchi, siku sote ni muhimu kuwasikiliza na kujali matashi yao, wasiposikilizwa watazungumza kwa namna wanayojua wao,” amesema Askofu Pisa.