Dar es Salaam. Ni msemo uliozoelekea mitaani kuwa wanawake wenye umri mkubwa ni benki za vijana.
Ukiwa umejaa utani na kejeli, msemo huo unaakisi mitazamo ya kijamii kuhusu vijana wa kiume wanaopenda wanawake wanaowazidi umri.
Wengi huamini vijana hao wanatafuta faraja ya kifedha, msaada wa kimaisha au hadhi, ikiwa ni utamaduni mpya uliojitokeza miaka ya karibuni kwa kundi hilo la vijana.
Oktoba 21, 2025 Makamu wa Rais mstaafu, Dk Philip Mpango, aliagiza kufanyika utafiti kubaini mzizi wa vijana kujihusisha na uhusiano wa kimapenzi na wanawake wanaowazidi umri.
“Inasikitisha kuona kuna ongezeko la vijana wetu wanaoingia kwenye uhusiano na mashangazi ambao wana pesa kama njia rahisi kwao kujikimu. Huu si utamaduni mzuri haupaswi kuendekezwa,” alisema Dk Mpango.
Huo ndiyo mtazamo uliobebwa na wengi kwamba, wanaingia kwenye mapenzi ya aina hiyo ili waweze kujikimu kiuchumi. Hata hivyo, simulizi za vijana wenyewe zinaonyesha picha tofauti, ndani ya uhusiano huo kuna mambo ya ziada zaidi ya fedha.
Kwa baadhi ya vijana, wao huvutwa na aina hiyo ya uhusiano ili kutafuta utulivu wa kihisia, hufuata ukomavu wao wa kifikra na aina ya upendo unaojengwa juu ya heshima, uaminifu na mawasiliano ya wazi.
Kwa mujibu wa wanasaikolojia na tafiti zilizopatikana kwenye mitandao zilizofanyika Afrika Kusini na Kenya, wanawake wenye umri mkubwa wanatajwa kuwa na ukomavu wa kihisia, ni waelewa na wazoefu wa maisha, hivyo vijana hujiona wakiwa na usalama wa kiuchumi na kimaisha, huku wakihisi kuthaminiwa na kuungwa mkono.
Akiwa na miaka 26, kijana aliyejitambulisha kwa jina moja la Nelson alikuwa na uhusiano na mwanamke wa miaka 38.
Anasema mwanamke huyo hakuwa tajiri, bali alikuwa na uwezo wa kawaida wa maisha. Hata hivyo, kilichomvutia ni namna alivyokuwa akimsikiliza, kumtia moyo na kumfanya ajisikie salama.
“Wanawake wenye umri mkubwa hawahitaji kuonyeshwa vitu vya kipuuzi ili kujua unawapenda. Wanathamini uaminifu, mazungumzo ya kweli na heshima. Vilevile, alikuwa na utulivu na mwenye kujiamini. Kwa kifupi, wanawake wa aina hii wanajua wanachokitaka,” anasema.
Nelson mwenye mwili uliojengeka na sura ya utu uzima, anasema wajihi wake unampa faida ya kuingia kwenye ulimwengu wa wanawake watu wazima bila kuwapo maswali mengi.
Anasema: “Wanawake wa aina hii wanasikiliza siyo kama hawa wanaojiona wajanja. Hawapotezi muda. Kama amekasirika, hatakukwepa au kukuzimia simu, atakwambia moja kwa moja. Uwazi na ukomavu huo hunifanya nitamani kuwa mwanamume bora zaidi.”
Akizungumzia uhusiano huo, anasema ulimvutia zaidi na kumpa amani kwa sababu alikuwa na mtu anayejielewa, tofauti na alivyowahi kuwa kwenye uhusiano wa watu wa rika lake.
“Ni uhusiano bora zaidi niliowahi kuwa nao. Hakuna kubahatisha, wanajua wanachotaka na watakwambia wazi,” anasema huku akitabasamu.
Anasisitiza kuwa, uhusiano wake na wanawake wenye umri mkubwa hauhusiani na kutafuta kulelewa au msaada wa kifedha kama ambavyo inatazamwa na vijana wengi.
“Wanawake hawa ni wataalamu, wanajitegemea na wana malengo. Mimi sipo kwa ajili ya misaada kama ni fedha na mimi nazitafuta zangu, unakuwaje na mwanamke utegemee yeye ndio akupe, hata nilipokuwa naye sikuwahi kuomba wala kupokea fedha zake, nilikuwa pale kwa ajili ya uhusiano wa kweli, upendo na heshima,” anasema.
Kwa upande wake, Juma Makata (30), yuko kwenye uhusiano na mwanamke aliyemzidi miaka 11.
Uhusiano kati ya wawili hao ulianzia kwenye mtandao wa Instagram, ambako walianza kutumiana maudhui mbalimbali hadi pale ukaribu wao ulipokomaa zaidi wakakubaliana kuonana.
“Tulipokutana kwa mara ya kwanza, nilijua moja kwa moja huyu ndiye mtu ninayemuhitaji kwenye maisha yangu. Anajua anachokitaka na ana uwezo wa kujieleza kwa uwazi,” anasema.
Imepita miezi 16 tangu walipoingia katika uchumba wakijiandaa kufunga ndoa.
Hata hivyo, anasema mambo si rahisi, anazungukwa na watu ambao hawaelewi uhusiano huo, wakiwemo marafiki zake.
“Cha kufurahisha ni kwamba, wakishakutana naye, wao huanza kuniuliza nifanyeje kumpata mtu kama yeye. Ukweli ni kwamba kujiamini kwao, wanavyotembea, wanavyofahamu wanachotaka… hakuna kubahatisha. Ukiwa nao, unakuwa makini, mtulivu na mwenye mwelekeo,” anasema.
Anaeleza uhusiano na wanawake wenye umri mkubwa siyo kwa ajili ya faida binafsi, bali ni upendo wa kweli.
Kijana mwingine wa miaka 28 ambaye hakutaka jina lake litajwe anasema aliwahi kuwa na mwanamke wa miaka 38, uhusiano uliomfundisha kuwa mwanamume mwenye msimamo.
“Nilikuwa na hasira nyingi, nisingependa maoni ya mtu. Lakini yeye alinifundisha kusikiliza na kutafakari kabla ya kuzungumza. Aliniambia mwanamume anajengwa na uwezo wake wa kutulia, siyo makeke,” anasema.
Anasema wanawake wakubwa kwa umri wana uwezo wa kuwatuliza wanaume vijana kwa njia ya hekima.
“Hawapigani kwa maneno, hawajifanyi wajuaji. Wanaongea kwa heshima, lakini maneno yao yanaingia hadi moyoni. Ukiwa nao, unajifunza kuwa mtulivu na mwenye nidhamu,” anasema.
Akizungumzia hilo kwa mtazamo wake, mwanasaikolojia Christian Bwaya, anasema hali hiyo ni matokeo ya mabadiliko ya kizazi cha sasa ambacho kinakwenda kuondoa utamaduni wa zamani, kwamba mwanamume ndiye anapaswa awe mwenye umri mkubwa.
Anasema kizazi kipya kinaanza kuvunja kanuni za kijamii kuhusu nani anapaswa kuwa mkubwa katika uhusiano.
“Kihistoria, jamii nyingi zilihusianisha mwanamume mkubwa ambaye ndiye aliyeonekana ana mamlaka na ndiye aliyekuwa mlinzi kwenye mahusiano. Inaonekana watu wameanza kuelewa dhana ya usawa wa kijinsia, hivyo hawajali tena mambo ya miaka au mila,” anasema.
Bwaya anasema sababu nyingine inayowafanya wanaume au vijana kutamani kuwa na wanawake wenye umri mkubwa ni usalama.
“Hii inaitwa emotional safety, imani kwamba mpenzi wako anaelewa, hatetereki kirahisi na ana uwezo wa kushughulikia migogoro vizuri. Kuna ukweli kuwa wanawake wakubwa kwa umri mara nyingi wamepitia changamoto za maisha zinazowasaidia kujitambua, kujithamini na kuwasiliana kwa uwazi zaidi. Ukongwe huu unawavutia vijana wanaochoshwa na mahusiano yasiyo na mwelekeo,” anasema.
Vilevile, anasema ni kutokana na ukomavu wa wanawake kadiri umri wao unavyosonga mbele, hivyo anakuwa na uwezo wa kukabiliana na mambo mbalimbali.
Anasema wanawake wa namna hiyo huwa hawashindani na vijana wa kiume kuonyesha nani ana hela au uwezo wa kiuchumi kuliko mwenzake.
Anaeleza, hawa wamevuka hatua hiyo, kwao kilicho muhimu ni penzi, urafiki na ukaribu wa kihisia.
“Unaweza kusema hii ‘mishangazi’ tayari inajua inachotaka na kwa vile imepitia mengi haiogopi kukataliwa. Kijana anayetafuta utulivu wa kihisia hapa anaona ndio kwenyewe,” anasema na kuongeza:
“Kwa hiyo, inaonekana vijana wengi wanawakimbilia ili wasiendelee kupambana na mashindano na vijana wenzao wa kike wanaojitafuta na kupenda mahusiano na wanaume wenye hela. Tafiti za saikolojia ya uhusiano zinaonyesha kuwa, baadhi ya wanaume vijana huchoshwa na mtu anayeshindana naye.”