Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi leo anawaapisha mawaziri wapya aliowateua hivi karibuni.
Katika kiapo hicho, Wizara nne kati ya 20 hazitakuwa na Mawaziri ambao bado wanasubiri mchakato wa Chama cha ACT – Wazalendo iwapo kitaamua kuingia ndani ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) au vinginevyo.
Wizara ambazo mawaziri wake bado hawajateuliwa ni pamoja na ya Afya, Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais.
Hafla hiyo itafanyika leo Jumamosi Novemba 15, 2025 saa 8:00 mchana katika viwanja vya Ikulu ya Zanzibar.
Mawaziri hao waliteuliwa na kiongozi huyo Alhamis, Novemba 13, 2025 alipowatangaza mbele ya waandishi wa habari Ikulu Vuga.
Wakati akitangaza uteuzi huo, Dk Mwinyi alieleza sifa zilizotumika kuwapata ikiwa ni pamoja na kuzingatia usawa wa kijinsia, uwiano wa mikoa ili kila Mkoa kuwapo na mwakilishi, elimu na uzoefu wa mhusika.
“Unapanga unapangua, lakini tunazingatia vigezo hivi na vingine vya ziada alivyonavyo mhusika mwenyewe,” amesema Dk Mwinyi.
Wanaotarajiwa kuapishwa ni pamoja na Dk Saada Mkuya ambaye ameteuliwa kuwa Waziri Ofisi ya Rais Ikulu, awali alikuwa Waziri wa Fedha na Mipango.
Katiba, Utumishi na Utawala Bora ataapishwa Haroun Ali Suleiman ambaye amerejeshwa katika wizara hiyo na Ofisi ya Rais Tamisemi ameteuliwa kuwa Idrissa Kitwana ambaye alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi.
Katika Wizara ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais ataapishwa Hamza Hassan Juma, Wizara ya Fedha na Mipango Waziri ni Dk Juma Ali Akil ambaye katika kipindi kilichopita alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo na Naibu Waziri atakuwa Dk Hamad Omar Bakar.
Wizara ya Kazi na Uwekezaji waziri wake ni Shariff Ali Shariff, awali wizara hii ilikuwa Wizara ya Kazi, Ajira na Uwekezaji. Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ameteuliwa waziri yuleyule Rahma Kassim Ali na Naibu Waziri wake Salha Mwinjuma.
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali amerejeshwa Waziri yuleyule Lela Mohamed Mussa na Naibu Waziri atakuwa Khadija Salum Ali.
Wizara ya Habari Sanaa Utamaduni na Michezo Waziri wake ni Riziki Pembe Juma ambaye alikuwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto. Naibu Waziri katika wizara hii atakuwa Ali Abdugulam Hussein ambaye awali alikuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali.
Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo ameteuliwa Masoud Suleiman Makame ambaye katika kipindi kilichoisha aliwahi kuteuliwa Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi lakini baadaye uteuzi wake ukatenguliwa. Katika Wizara hii Naibu Waziri atakuwa Dk Salum Soud Mohamed (ni mpya ndani ya Baraza).
Wizara ya Maji, Nishati na Madini ameteuliwa Nadir Abdulatif ambaye alishindwa katika kura za maoni lakini ameteuliwa na Rais kuwa mjumbe wa baraza. Katika Baraza lililopita Nadir alikuwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi. Naibu waziri katika wizara hii atakuwa Seif Kombo Pandu.
Masoud Ali Mohamed ameteuliwa kuwa Waziri wa Uchumi wa Buluu ambaye katika mchakato wa kura za maoni alipigwa chini na chama lakini akateuliwa kuwa mjumbe na Rais, na katika Baraza lililopita alikuwa Waziri Ofsi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za SMZ. Katika Wizara hii Naibu waziri ameteuliwa Mboja Ramadhan Mshenga
Wizara nyingine ni Ujenzi na Uchukuzi ambaye ameteuliwa kuwa Dk Khalid Salum Mohamed akireeja wizara hiyo ambayo imondolewa Mawasiliano huku Naibu Waziri wake ni Badria Natai Masoud.
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Waziri wake ni Anna Athanas Paul ambaue awali alikuwa naibu Waziri katika wizara hiyo. Katika kipindi hiki amemteua Zawad Amour Nassor ambaye katika baraza lililopita alikuwa Naibu waziri wa Maji, Nishati na Madini.
Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ameteuliwa Mudrick Ramadhan Soraga na Naibu Waziri atakuwa Mohamed Sijiamin Mohamed huku Wizara ya Vijana Ajira na uwezeshaji ambayo ni mpya akiteuliwa Shaaban Ali Othman ambaye alikuwa Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi na Naibu Waziri atakuwa Hassan Khamis Hafidh ambaye katika baraza lililopita alikuwa Naibu Waziri wa Afya.