Musoma. Shirika lisilokuwa la kiserikali la Vi Agroforestry limepanda miti zaidi ya milioni 163 katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda katika kipindi cha miaka kumi iliyopita huku lengo kuu likiwa ni kukabiliana na athari zinazoendelea kutokea kutokana na mabadiliko ya tabianchi.
Takwimu hizo zimetolewa na Ofisa Mazingira, Bioanuai na Mabadiliko ya Tabianchi kutoka shirika hilo, Rashidi Malya wakati wa uzinduzi wa msimu wa 11 wa upandaji miti wa shirika hilo, shughuli iliyofanyika leo Novemba 15,2025 katika Shule ya Msingi Mkiringo wilayani Butiama.
Malya amesema miti hiyo imepandwa katika taasisi za umma ikiwemo shule za msingi na sekondari, vyuo na ofisi zingine pamoja na taasisi za kijamii kama vile makanisani.
Amesema upandaji wa miti hivi sasa unafuata kanuni za kilimomisitu ambapo miti yenye rutuba hupandwa katika maeneo yanakolimwa mazao hivyo kusaidia kuwa na tija katika kilimo ikiwa ni pamoja na kuongeza mavuno wakati huohuo miti hiyo ikileta faida zaidi kama vile matunda na mbao.
“Shirika liliamua kuanzisha kampeni ya upandaji miti katika hizi nchi tatu kutokana na athari zinazoendelea kuikumbuka dunia kutokana na mabadiliko ya tabianchi, tunaamini kampeni hii kwa namna moja ama nyingine imesaidia kupunguza athari hizo,” amesema.
Amesema changamoto wanazokutana nazo ni pamoja na miti mingine kushindwa kukua kutokana na athari hizo za mabadiliko ya tabia nchi ikiwemo ukame na mafuriko ambayo wakati mwingine hukumba maeneo yalikopandwa miti.
Mwakilishi wa Vi Agroforestry Kanda ya Afrika Mashariki, Dk Monica Nderuti amesema kwa msimu huu wamepanga kupanda miti zaidi ya 800 katika shule ya Msingi Mkiringo iliyopo wilayani Butiama.
Ameitaka jamii kushirikiana na wadau pamoja na Serikali katika kukabiliana na athari hizo kwa kupanda miti na kuitunza huku akisema kuwa jamii ina wajibu mkubwa wa kuhakikisha lengo hilo la upandaji miti linatumia kwa ufanisi mkubwa.
Amesema kampeni ya upandaji miti inafanywa mashuleni ikiwa ni sehemu ya kuwajengea uelewa wanafunzi juu ya umuhimu wa upandaji wa miti na utunzaji wa mazingira kwa ujumla ili kuwa na kizazi kijacho kitakachokuwa kina thamini uhifadhi wa mazingira kwa ujumla.
Dr Nderuti amesema sambamba na hilo pia wanalenga kuwaelimisha wanafunzi kuhusu suala zima la kilimomisitu ili watakapokuwa wakubwa waweze kuendeleza kilimo hicho kwa ufanisi.
“Mbali na kilimomisitu lakini pia hii miti inayopandwa hapa itakuwa chanzo cha kivuli, matunda na hata mbao kwaajili ya kutengeneza madawati au ujenzi wa madarasa hivyo hili jambo lina manufaa mengi kwa jamii,” amesema.
Akizindua kampeni hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Thecla Mkuchika amewaagiza viongozi wilayani humo kusimamia suala zima la upandaji miti huku akitoa onyo kwa watu wenye mifugo wanaoacha mifugo yao iharibu miti iliyopandwa.
Ameziagiza shule zote za umma kufanya kilimomisitu katika maeneo ya shule ili kuwezesha upatikanaji wa chakula angalau mara moja kwa wakati wa masomo jambo ambalo pamoja na mambo mengine litasaidia kuboresha kiwango cha taaluma wilayani humo.
“Kilimomisitu kinahusisha kilimo cha miti ya aina mbalimbali ikiwepo ya matunda sambamba na mazao hivyo tutumie fursa hiyo ili tuweze kupata mazao na matunda kwa wakati mmoja hivyo kuweza kuboresha lishe ya watoto wetu na taaluma kwa pamoja,” amesema.