LICHA ya kuanza msimu kwa kusuasua katika Ligi Kuu Bara, Kocha Mkuu wa Namungo, Juma Mgunda amesema timu ina mabadiliko, tofauti na msimu uliopita kutokana na wachezaji walioongezwa kikosini kuonyesha ubora.
Namungo haijawa bora kwa misimu miwili mfululizo ikiponea tundu la sindano msimu ulioishi na pia haijaanza vizuri, lakini Mgunda amewatoa hofu mashabiki wa timu hiyo kuwa imeimarika na ina wachezaji wenye uchu wa mafanikio.
Namungo imekusanya pointi sita kwenye mechi sita za ligi msimu huu ikishinda moja, sare tatu na kupoteza mbili.
Akizungumza na Mwanaspoti, alisema malengo ni kuwa timu shindani na kumaliza katika nafasi tano za juu kwenye msimamo.
“Hatujaanza vizuri, lakini mambo mazuri yanakuja kwani wachezaji wangu wapo vizuri na wanaonyesha kuwa na uhitaji wa kushindana na timu pinzani, makosa machache tu ndio yanatugharimu. Matarajio ni kufanya vizuri na itakuwa hivyo,” alisema.
“(Kutoanza vizuri) nafikiri ni kwa sababu ya aina ya timu tulizokutana nazo hadi sasa zilikuwa na mwanzo mzuri. Lakini, pia timu imesajili wachezaji wengi wapya, hivyo muunganiko umeanza kupatikana ikikaa vizuri itakuwa nzuri na shindani.
“Tuna malengo makubwa, bado ni mapema sana kukubali kushindwa licha ya kupoteza mchezo mmoja na sare mbili. Hii haituondoi kuwa kati ya timu shindani,” alisisitiza kocha huyo wa zamani wa Coastal Union na Simba.
Baada ya mchezo wa mwisho dhidi ya Azam FC ikiwa nyumbani kuambulia sare ya kufungana bao 1-1, Namungo inaendelea kujifua tayari kwa ajili ya mchezo unaofuata dhidi ya Dodoma Jiji utakaochezwa Novemba 21, mwaka huu.
Kabla ya hapo ilianza kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Pamba Jiji, ikaichapa Tanzania Prisons 1-0 kisha ikafungwa 3-0 na Simba na kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Mashujaa FC.