NYOTA wa zamani wa Azam, Mkenya Kenneth Muguna amesema licha ya kucheza Ligi mbalimbali katika fani yake ya soka hadi sasa, ila hajaona Ligi bora na yenye kuvutia sana zaidi kama ya Tanzania, kwenye Ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati.
Kiungo huyo aliyewahi kuitumikia Azam kwa miaka miwili kuanzia Julai 2021 hadi 2023, akitokea Gor Mahia ya kwao Kenya, ametoa kauli hiyo baada ya mahojiano aliyofanya na kituo cha Redio cha Sporty FM cha nchini mwao na kuelezea ubora huo.
“Unapotaja Tanzania unazungumzia moja ya nchi yenye Ligi bora sana kwa Ukanda wetu wa Afrika Mashariki, mashabiki zao wanapenda sana klabu wanazoshabikia, miundominu yao ni mizuri jambo ambalo linavutia wachezaji wengi,” alisema Muguna.
Nyota huyo alisema katika kipindi cha miaka miwili alichocheza Ligi ya Tanzania moja ya jambo lililomshangaza ni kuona mashabiki huwa hawataki kuangalia zaidi ya kile ulichokifanya ulipotoka, isipokuwa kwa wakati husika kwa klabu uliyopo.
“Mchezaji anaweza akafanya vitu vikubwa sana huko alipotoka kwa maana ya takwimu zake zinaweza zikambeba, ila akija tu Tanzania watu wanataka kuona uwezo wako halisia na wala sio kile ulichokifanya, kiukweli ilinishangaza sana,” alisema.
Muguna anayeichezea kwa sasa Township Rollers ya Botswana, alikuwa ni miongoni mwa viungo bora wa kikosi cha Azam, huku akiwahi pia kuzichezea timu za Western Stima, Gor Mahia na Kenya Police zote za kwao Kenya na KF Tirana kutokea Albania.