Mwanuke azitaja Simba, Singida BS

KIUNGO mshambuliaji wa Fountain Gate, Jimmyson Mwanuke amezitaja Simba na Singida Black Stars kuwa ndizo timu ambazo zimemuongezea ubora wa kiwango licha ya kukosa nafasi ya kucheza mara kwa mara wakati akizichezea.

Mwanuke aliyezitumikia timu hizo kwa nyakati tofauti ameliambia Mwanaspoti kuwa amepata faida kubwa ya kufanya mazoezi na nyota wengi bora ambao wana uwezo mkubwa kiuchezaji.

“Ukiondoa thamani kubwa niliyoipata kujiunga kwenye timu hizo, kuna faida ya kiuchezaji nimepata na naamini nikifanyia kazi nje ya timu hizo nitarudisha ubora wangu wa misimu niliyokuwa napata nafasi ya kucheza mara kwa mara,” alisema.

“Nimefanya mazoezi na wachezaji wengi wenye uwezo mkubwa ndani ya Simba na Singida Black Stars, mazuri mengi nimeyabeba na naahidi kuyafanyia kazi nikiwa Fountain Gate nitakapopata nafasi ya kucheza.”

Mwanuke usajili wake kufanikiwa ndani ya timu hiyo, alisema anatambua umuhimu wake kwenye kikosi hicho na matarajio yake ni kuipambania Fountain Gate ifikie malengo ya kubaki Ligi Kuu Bara tena msimu ujao.

“Ni kweli usajili wetu (Fountain Gate) ulichelewa kutokana na changamoto ambazo zipo nje ya uwezo, viongozi wamefanyia kazi na sasa tumerudi uwanjani tupo tayari kuipambania nembo ya timu iweze kumaliza nafasi bora za juu na kuwa timu shindani,” alisema mchezaji huyo.

“Baada ya usajili kukamilika timu ipo tayari na matarajio ni makubwa sana kwani tuna kikosi kizuri na wachezaji wengi wenye ubora, sasa ni kazi kwetu kuhakikisha tunapata kile uongozi unakitarajia.”

Akizungumzia ligi kwa ujumla, alisema licha ya kwamba baadhi ya wachezaji wa timu hiyo hawakuanza nayo mwanzo, lakini alikuwa anafuatilia na kubaini kuwa huu ni msimu mgumu ambao anatakiwa kupambana ili awe bora zaidi kiushindani.