Mfaransa wa Azam aponzwa na kibali Angola

MAMBO si mazuri kwa kocha wa zamani Azam FC, Bruno Ferry baada ya kuondolewa nchini Angola kwa hati ya dharura kutokana na kukosa kibali cha kuishi.

Bruno ambaye msimu uliopita alikuwa kocha msaidizi wa Azam, baadaye alitimkia Wiliete ya Angola ambako alikuwa akipiga mzigo akiwa kocha mkuu na kuiwezesha kutinga Ligi ya Mabingwa Afrika ilikoishia hatua ya awali.

Mwanaspoti linafahamu kuwa baada ya Bruno ambaye ni raia wa Ufaransa kusepa Azam alitua Wiliete ambako timu aliyokuwa akiifundisha imekuwa ikicheza soka la kuvutia ndani ya muda mfupi aliodumu nayo.

Septemba, mwaka huu, Mfaransa huyo alirejea Bongo akiwa na Waangola hao ambapo walicheza mechi ya pili ya hatua za awali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Yanga.

Licha ya kwamba walipoteza kuanzia ugenini mpaka nyumbani kwa jumla ya mabao 5-0, lakini ubora wa kikosi hicho cha Mfaransa ulionekana kuwavutia mashabiki wengi wa soka nchini wakiamini kwamba kiliangushwa kwa kukosa uzoefu katika mashindano ya kimataifa.

Taarifa zilizolifikia Mwanaspoti kutoka Angola zinadai Bruno ameondolewa nchini humo kwa hati ya dharura ndani ya saa 24 na Wizara ya Uhamiaji kutokana na kutokamilisha matakwa ya kibali cha kuishi nchini humo.

“Klabu ya Wiliete ilishindwa kumtafutia kibali cha kufanya kazi kocha Bruno, hivyo alitakiwa kuondoka Angola ndani ya saa 24 akiwa kwenye usimamizi, ambapo kama angechelewa angeweza kuwekwa rumande,” kilisema chanzo cha gazeti hili.

“Hata hivyo Bruno amefanikiwa kuondoka Angola na kurejea salama kwao Ufaransa, hivyo Wiliete sasa inatakiwa kumtafutia upya usajili wa ajira ili arudi kuendelea na majukumu yake.”

Ikumbukwe kuwa, kocha huyo wa zamani wa Azam ameondoka wakati timu yake ikiwa katika nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu Angola.