Maelekeo ya Rais Mwinyi kwa mawaziri akiwaita ACT kuunda Serikali

Unguja. Wakati Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi akiwaapisha mawaziri aliowateua amesema siyo wakati wa kwenda kufanya sherehe badala yake ni muda wa kujitathmini, kutafakari namna gani watakidhi matakwa ya wananchi.

Katika kuliendea hilo amewatwisha zigo la mambo 12 mbayo wanatakiwa kuyafanyia kazi kwa kasi zaidi ili kuleta mabadiliko katika kipindi cha pili cha utawala wake kama Rais wa visiwa hivyo maarufu kwa utalii na uzalishaji wa karafuu.

“Kuna mawaziri wapya lakini wengi mlikuwepo, kuanzia sasa tutawapima nimeshawaambia tunataka kasi zaidi ya ile ya kipindi kilichopita, huu siyo wakati wa sherehe bali nendeni mkatafakari na kujitathmini namna ya kukidhi matakwa ya wananchi, amesema Dk Mwinyi akiwaapisha leo Novemba 15, Ikulu Zanzibar.

Mbali na kutoa maagizo hayo, Pia Rais Mwinyi amekiomba Chama cha ACT Wazalendo kuona umuhimu wa kuunganisha nchi na watu wake kwa kuingia ndani ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).

Rais wa Zanzibar akimwapisha Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman katika hafla iliyofanyika viwanja vya Ikulu Zanzibar.



“Tumeacha nafasi za wizara nne ili kuwasubiria wenzetu ambalo ni takwa kikatiba, naendelea kuwaomba waone umuhimu wa kuunganisha nchi na watu wake ya kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa,” amesema Dk Mwinyi.

Kwa nyakati tofauti tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Othman Masoud katika mikutano ya kuwashukuru wananchi kisiwani Pemba amekuwa akisema kipaumbele chao kwa sasa siyo kuingia SUK bali ni kuangalia namna ya kushughulikia changamoto zilizojitokeza wakati wa uchaguzi kwa madai ulikuwa uchaguzi ambao haukuwa na haki.

Amesema kwa sasa wanaangalia namna ya kwenda mahakamani kupinga ushindi huo. Hata hivyo kwa mujibu wa katiba na sheria za Zanzibar matokeo ya Rais hayapingwi mahakamani isipokuwa ya uwakilishi na ubunge.

Dk Mwinyi amewataka mawaziri hao kuwa wabunifu kushughulikia changamoto za wananchi kwa kuwafuata kwenye maeneo yao badala ya kukaa ofisini.

Kiongozi huyo amesema katika kipindi kilichopita mawaziri walikuwa wakimpelekea changamoto zote yeye azishughulikie.

“Changamoto msinipe mimi, nimewateua mnisaidie sasa inakuwa haina maana kuniletea tena changamoto zote kwangu,” amesema.

Hata hivyo, amewaeleza iwapo wakiona mambo yanakuwa magumu kuliko uwezo wao wasikae kimya wakamweleze au wamfuate Makamu wa Pili wa Rais ili kupata ufumbuzi wa haraka.

Jambo jingine, Dk Mwinyi amewataka mawaziri hao kufanya mabadiliko ya sheria ambazo wanaona ni kikwazo katika utendaji kazi kwani katika kipindi kilichopita wapo baadhi yao ambao wamekuwa wakieleza shida ya sheria ilhali wana uwezo wa kufanya marekebisho barazani.

“Tusiwe watumwa wa sheria zetu, hili nawataka mkalifanye haraka sana iwezekanavyo,” amesema.

Dk Mwinyi amesema katika kipindi hiki watakuwa na mkataba nao wa kupima ufanisi na utendaji kazi wao ili kuona kasi ya utendaji kazi wao.

“Wekeni taratibu za utekelezaji wa kazi zenu kila robo mwaka kuonesha mliyofanya,” amesisitiza.

Katika kulitekeleza hilo pia Dk Mwinyi amewataka mawaziri hao kuwa na utaratibu wa kuzungumza na waandishi wa habari kila mara ili kueleza mafanikio na changamoto na namna ya kuzitatua.

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi (kushoto) akimkabidhi cheti cha kiapo Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Hamza Hassan Juma wakati wa kuwaapisha Mawaziri na manaibu Waziri hafla iliyofanyika Ikulu Zanzibar



“Wapo mawaziri ambao hawapendi kuzungumza na waandishi wa habari, hili sitaki kulisikia lazima muwe tayari kuzungumza kueleza mafanikio na changamoto na jinsi mnavyokwenda kuzitatua,” amesema Dk Mwinyi.

Katika hafla hiyo iliyofanyika viwanja vya Ikulu Zanzibar, Dk Mwinyi amesema safari na mafuta ni maeneo ambayo yanachukua fedha nyingi za Serikali bila kuwa na tija kwenye wizara hivyo amewataka kukomesha safari hizo na kudhibiti mafuta yanayotumika bila sababu.

“Kumekuwapo na safari ambazo hazina tija, mtu anapanga safari ya Dola za Marekani 5,000 zaidi ya Sh12 milioni, sasa nasema safari hizi basi kama huwezi kuamua safari gani yenye tija nitaamua mimi,” amesema Dk Mwinyi.

Pia, Dk Mwinyi amesema zipo wizara ambazo watendaji wake walikuwa wakigombana ofisini, hivyo hataki kusikia jambo hilo katika kipindi hiki cha pili.

“Mafanikio ya wizara yanategemea ushirikiano wa pamoja, hakuna sababu ya kugombana maana kazi haziendi,” amesema Dk Mwinyi.

Maagizo mengine Dk Mwinyi amesema bado katika kipindi kilichokwisha hawakufanya vizuri katika nidhamu ya makusanyo na matumizi ya fedha, akisisitiza, “Nataka tubadilike kwa wizara zinazohusika katika sekta hizo.”

Dk Mwinyi pia amewataka wateule hao kutengeneza mpango kazi wa kutekeleza ahadi alizotoa kwenye kampeni, Mpango wa Maendeleo na Dira ya Maendeleo ya Zanzibar.

“Ninataka mpango huu uandaliwe haraka sana iwezekanavyo na wala sio kuanza kujipanga maana makatibu wakuu wapo watasaidia,” amesema.

Katika hilo amewaondolea hofu makatibu wakuu waliopo waendelee kuchapa kazi kwani hajapanga kuwaondoa kwenye nafasi zao.

Ameeleza wajibu mwingine ambao wanataka kuzingatia ni kutambua miradi inayotekeleza katika wizara husika, kuangalia ubora wake, thamani ya fedha na muda ambao miradi hiyo inatakiwa kutekelezwa.

“Safari hii nataka tuwe site, wananchi wanataka waone changamoto zao zinapatiwa ufumbuzi nendeni kwa wananchi, jipange vilivyo,” amesema Dk Mwinyi.

Pia, amewaagiza mawaziri hao kuhakikisha wanasimamia uwajibikaji wa watumishi akisema bado kuna tatizo kubwa la uwajibikaji katika wizara mbalimbali hivyo kila mmoja anatakiwa kusimama kidete.

Pia, amesema wanatakiwa kusimamia misingi ya utawala bora, kudhibiti ubadhirifu wa fedha na kukomesha rushwa katika taasisi ambazo zipo chini ya Wizara zao.

Dk Mwinyi amerudia kutoa ufafanuzi sababu ya kuongeza wizara mbili. Kuhusu Wizara ya Vijana, Ajira na Uwekezaji, amesema ameamua kuitenganisha ili kuwasaidia vijana katika kupata ajira na kushughulikiwa changamoto zao.

“Tuliahdi vijana kushughulikia changamoto zao wakati wa kampeni, hivyo tumeona ni lazima tuwe na wizara inayojitegemea kumaliza matatizo ya ajira na uwezeshaji,” amesema.

Kuhusu Wizara ya Mawasiliano, Tehama na Ubunifu, pia Dk Mwinyi amesema katika ulimwengu wa sasa inakwenda kidijitali hivyo lazima kwenda sambamba na mabadiliko hayo.

“Hatuwezi kuendelea kizamani, lazima twende kisasa tunapotaka uchumi wa kidijitali lazima tuwe na miundombinu na mifumo ambayo inatuwezesha kufika huko,” amesema Dk Mwinyi.

Awali Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amesema wamejipanga kuongeza kasi zaidi katika kipindi hiki cha pili ili akifika mwisho wa utawala wake yale aliyokusudia yatimie.

“Nakuhakikishia tutafanya kazi kwa bidii kubwa, naamini wengi wao wanaelewa ‘spirit’ yako na tutakwenda kutimiza uliyoahidi,” amesema.

“Sina mashaka hii ni timu ya ushindi na kamwe hautashindwa, tunakwenda kufanya makubwa zaidi hata wale ambao hawakuamini katika kipindi kilichopita basi wataamini na kuelewa azma yako ya kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar,” amesema.