Dodoma. Jumuiya ya Wazazi Chama cha Mapinduzi (CCM) imempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa msamaha kwa vijana waliokamatwa kwenye maandamano yaliyotokea Oktoba 29, 2025 na kuwataka vijana nchini kuachana na masuala yanayohatarisha amani ya Taifa kwenye mitandao ya kijamii.
Aidha jumuiya hiyo imewaomba vijana kuacha kufuata mkumbo wa kila kitu kinachoendelea kwenye mitandao ya kijamii kwani hata wakati maandamano ya Oktoba 29 yaliyohamasishwa mitandaoni yalimfikia kila mtu lakini kuna waliyoyapuuza na waliounga mkono.
Hayo yamesemwa leo Jumamosi Novemba 15, 2025 na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi (CCM), Maganya Rajabu wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kufuatia msamaha wa Rais alioutoa jana Novemba 14, 2025 wakati wa kufungua Bunge la 13 ya kuwasamehe vijana wote walioandamana kwa kufuata mkumbo.
Rajabu amesema uamuzi huo siyo uoga kwa Rais bali ni uamuzi wa kizalendo na unaonyesha ukomavu wa kisiasa na moyo wa mama.
“Sisi sote ni mashahidi kuna nchi kadhaa zimekumbwa na machafuko ya namna hii lakini hawakuchukua uamuzi kama aliouchukua Rais wetu wa kuwasamehe vijana kwa hiyo hatua hii si uoga bali ni ukomavu wa kisiasa na moyo wa mama ambao siku zote una huruma, maana tuna methali zetu za Kiswahili zinazosema mtoto akinyea mkono hauukati bali unausafisha na ndicho kilichofanyika,” amesema Rajab.
Kuhusu kuundwa kwa tume ya kuchunguza chanzo cha maandamano hayo ya Oktoba 29, Rajab amesema ni jambo jema kwa sababu tume hiyo itachunguza chanzo na kutoa hatua za kuchukua kwa wote waliohusika.
Amewataka Watanzania kuendelea kuienzi amani, utulivu na mshikamano wa Taifa kwa kuwa ndiyo tunu za nchi na kwamba kupitia siku nne za uvunjifu wa amani Watanzania wamejifunza kuwa amani siyo kitu cha kuchezea hata kidogo.
Mkazi wa Dodoma Innocent Chuwa ameitaka jamii kupaza sauti kuhusu umuhimu wa kuilinda amani kwa kutumia mitandao ya kijamii kwani mitandao hiyo imekuwa chanzo cha mmomonyoko wa maadili kutokana na watu wenye nia mbaya kuitumia kuwahamasisha vijana kufanya wanayoyataka.
“Tatizo watu wanaotakiwa kuwaelekeza vijana umuhimu wa amani wapo lakini wamenyamaza kimya na hivyo kutoa mwanya kwa watu wenye nia ovu kutumia mitandao hiyo kuwarubuni vijana kwa kuwa muda mwingi wanashinda kwenye mitandao ya kijamii bila wazazi na walezi kujua vijana wao wanajifunza vitu vya namna gani kutumia mitandao hiyo,” amesema Chuwa.
Amesema ni muda sasa wa wazazi, taasisi na watu binafsi kutoa elimu ya kulinda amani kupitia mitandao ya kijamii kwa kuwa huko ndipo vijana wengi wanapopatikana lakini wanapewa maudhui ambayo hayafai kwa mustakabali wa Taifa.
Naye Teddy Maringo amewataka Watanzania wote kwa ujumla kujifunza umuhimu wa kudumisha amani bila kujali kama ni kijana au mzee kwani amani ikipotea haichagui kama ni kijana au ni mzee wote wanashindwa kufanya shughuli zao za kila siku kutokana na machafuko yatakayotokea.
Amesema wananchi wana imani kubwa na serikali yao kuwa itawalinda wananchi na ghasia mbalimbali kama ilivyokuwa inafanya miaka ya nyuma kwani yaliyotokea Oktoba 29 yalimshtua kila mmoja kwa sababu hayakutarajiwa kama yangetokea.