Dar es Salaam. Wakati Serikali ikiwa mbioni kuanzisha wizara maalumu ya vijana, wenyewe wamesema hatua hiyo inapaswa kuanza na kukusanya maoni yao, ili wapendekeze muundo utakaokidhi matarajio yao.
Lakini, baadhi wanaona kabla ya kuanza na hatua ya kuunda wizara yao, kuna haja ya Serikali kutazama katika mifumo yake ya uwajibikaji, ili wizara hiyo isijikute ikiingia katika mkumbo wa utendaji usiowagusa vijana.
Pia, wapo wanaosema hiyo ni nia njema lakini haitakuwa safari rahisi. Changamoto kama upatikanaji wa rasilimali za kutosha, uratibu wa taasisi za Serikali zilizozoea mfumo wa zamani na dhana kwamba masuala ya vijana yanaweza kusubiri, zinaweza kupunguza kasi ya mabadiliko yanayotarajiwa.
Mitazamo hiyo ya vijana na wadau wengine, inakuja siku moja baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kutangaza mpango wa kuanzisha wizara ya vijana, badala ya kuwa kama idara kwenye wizara yenye mambo mengi.
Katika hotuba yake ya kulifungua Bunge la 13, jijini Dodoma Novemba 14, 2023, Rais Samia mbali na kutangaza kusudio la kuanzisha wizara hiyo mpya, alisema anafikiria kuwa washauri wa masuala ya vijana ndani ya ofisi yake.
Alisema anafanya hivyo kwa sababu zaidi ya asilimia 60 ya watu wa Tanzania ni vijana, hivyo shabaha yake ni kuweka kipaumbele kwenye sera na programu zitakazopanua fursa za kiuchumi, kutengeneza kazi na ajira, kuongeza wigo wa hifadhi za jamii na kuwajengea kesho iliyo bora.
Akizungumzia benki hiyo, Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana wa Chama cha ACT – Wazalendo, Abdul Nondo amesema pengine uamuzi huo una nia njema ndani yake, lakini kabla ya kufika huko, Serikali inapaswa kutazama upya mifumo yake ya upatikanaji wa viongozi na uwajibikaji.
Amesisitiza kuwa na waziri na washauri wa Rais katika masuala ya vijana pekee hakutoshi, kwa sababu hawatabadilisha chochote kama hakutakuwa na kiongozi anayeumizwa na yanayowasibu vijana.
“Inapaswa mtu anapopata nafasi ya kuwa mbunge, ajue wazi kabisa kwamba asipotimiza mahitaji fulani ya vijana wa eneo fulani, hatapata tena nafasi ya ubunge. Kuwe na uwajibishanaji,” ameeleza.
Mbali na hilo, Nondo anaona hakuna kitakachobadilika kama mifumo hairuhusu ustawi na masilahi ya vijana kutekelezwa na kuheshimiwa.
Kama ilivyo kwa Nondo, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirikisho la Vijana Tanzania (TYC), Lenin Kazyoba anaona kuwa na wizara ni mbali zaidi. Ni muhimu kuanza na hatua ya awali ili wizara na washauri hao, wakidhi matarajio.
Amependekeza kabla ya kufika huko, ama iundwe tume au kamati ya kukusanya maoni ya vijana, waseme wangependa wizara yao iweje, mambo gani hasa mahususi yasimamiwe na kwa namna gani.
“Lazima tuwe na majadiliano ya pamoja kuhusu namna gani tunapaswa kuwa na wizara inayoweza kukidhi matarajio ya vijana. Iundwe kamati itakayokusanya maoni ya vijana na waeleze mapendelezo yao kuhusu mfumo na muundo wa wizara iweje ili iendane na matakwa yetu,” amesema.
Amesema kumekuwa na changamoto za kimifumo kuhusu ushughulikiaji wa masuala ya vijana, hivyo hata wizara pengine itakumbwa na hali hiyo na hatimaye isiwe na tija.
“Fikiria tumekuwa na mikopo ya asilimia 10 kwa ajili ya makundi mbalimbali wakiwemo vijana. Kwa sehemu kubwa hawakunufaika kwa sababu za kimifumo. Leo hii unapotaka kuwapa vijana mikopo ukubali kufanya uwekezaji wa muda mrefu,” amesema.
Itakuwa mtetezi wa vijana
Kwa Mchambuzi wa Masuala ya Vijana na Ajira, Nimrod Mameo mambo ni tofauti, yeye anaiona hiyo ni hatua muhimu katika wakati ambao vijana wamekuwa fursa kwa upande mmoja, lakini tishio kwa upande mwingine.
Ameeleza vijana ndio walioshuhudiwa wakianzisha mavuguvugu yanayosababisha kuvunjika kwa amani na wakati mwingine hata mabadiliko ya uongozi.
Ripoti ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), inaonyesha pengo kubwa katika ajira, ujuzi, ushiriki wa maamuzi na fursa za kiuchumi.
Ukosefu wa ajira kwa vijana wa kike utafika hadi asilimia 16.7, zaidi ya mara mbili ya vijana wa kiume ambao wapo kwenye wastani wa asilimia 8.3.
Amesema mamilioni ya vijana wanahitimu vyuoni kila mwaka, lakini hawapati jukwaa la kuingia kwenye soko lenye ushindani linalohitaji ujuzi, mitaji na mtandao wa kiuchumi ambao wao wanaanza kuutafuta kwa hatua ya kwanza.
“Ndiyo maana taarifa ya Rais Samia inaonekana kama mwanga mpya juu ya anga lililokuwa limetanda kwa ukungu wa sintofahamu. Kuundwa kwa wizara maalumu kunatoa tumaini kwamba hatimaye masuala ya vijana hayatakuwa masimulizi kwenye hotuba za kitaifa, bali yatapewa muundo, bajeti na uwajibikaji wa wazi,” amesema.
Mameo amefafanua kuwa kwa mara ya kwanza, Serikali inasema kwa vitendo kuwa inataka kusikia sauti ya vijana bila kuipitisha kwenye milolongo ya urasimu.
Kupitia washauri maalumu watakaoketi karibu na mamlaka ya juu nchini, amesema vijana watakuwa na njia ya moja kwa moja ya kufikisha maoni yao, kuchangia sera na kuunda mustakabali wanaoutamani.
“Wataalamu hao hawatakuwa tu waleta dokezo, bali watakuwa daraja la kuunganisha kilio cha vijana na masikio ya mamlaka. Hili pekee linaweka alama mpya katika historia ya utawala, kwamba kundi kubwa la wananchi linastahili kusikilizwa si kwa hisani, bali kwa sababu lina wajibu na mchango mkubwa kwenye maendeleo ya Taifa,” amesema Mameo.
Hoja inayofanana na hiyo, imetolewa pia na Neema Mliga, mwanaharakati wa vijana aliyesema katika miaka ya karibuni, Tanzania imekuwa ikijitahidi kuongeza fursa kwa vijana kupitia programu mbalimbali ndani ya wizara zilizopo, lakini mchanganyiko wa majukumu aghalabu umezua changamoto.
Amesema masuala ya vijana yamekuwa yakichanganywa na michezo, utamaduni au ajira, kiasi kwamba mahitaji mahususi ya kundi hilo yalikuwa hayapati nafasi ya kutosha.
“Wizara mpya inaweza kubadilisha dhana hiyo. Inaweza kuleta mkondo mpya wa kufikiri kwamba vijana wanahitaji sera zao, tafiti zao na hatua zao za utekelezaji zilizoainishwa kwa lugha ya matatizo yao,” amesema.
Amesema Serikali inaweza kutengeneza programu zinazolenga moja kwa moja kuunganisha vijana na ajira, kuanzisha vituo vya ubunifu, kubuni mafunzo ya muda mfupi yenye tija na kuratibu mahusiano ya karibu na sekta binafsi.
Neema amesema ukiacha takwimu za ukosefu wa ajira na uwiano wa idadi ya vijana, kuna swali linalopaswa kujibiwa na wizara hiyo, kwamba vijana wanaandaliwa kuwa sehemu ya utajiri wa Taifa au wanaachwa kuwa watazamaji.
Ripoti ya Tume ya Vyuo Vikuu mwaka 2024, inaonyesha zaidi ya vijana 400,000 huingia kwenye soko la ajira kila mwaka, huku fursa rasmi za ajira zikiwa chini ya kiwango hicho.
Kwa mujibu wa taarifa za bajeti mwaka 2024/2025, programu za Serikali kwa ajili ya mikopo na mafunzo kwa vijana bado ziko chini ya uhitaji halisi, hivyo wizara maalumu itapaswa kubadili sura hiyo, si kwa nadharia bali kwa hatua zinazoonekana.
“Hatua hizo zinaweza kujengwa juu ya msingi kwamba vijana wanahitaji ujuzi wa kisasa, teknolojia, mazingira wezeshi ya ujasiriamali, upatikanaji wa mitaji midogo na ya kati, na mfumo rafiki wa kuingiwa na sekta binafsi. Kuanzisha wizara ni hatua ya kwanza, kuhakikisha inafanya kazi kwa viwango vinavyotarajiwa ndilo jaribio kubwa zaidi,” amesema Neema.
Mwanazuoni wa uchumi, Dk Josephat Werema amesema nchi yenye idadi kubwa ya vijana ina fursa ya kupata kile kinachoitwa faida ya idadi ya watu ambayo hutokea tu pale ambapo vijana huwezeshwa, hufundishwa na huchangiwa kuwa wachangiaji wa uzalishaji.
“Kuanzishwa kwa wizara hii ni ishara kwamba Tanzania inataka kutumia fursa hiyo kabla dirisha halijafungwa. Umri wa wastani wa Mtanzania ni miaka 18. Ukishindwa kuwaandaa vijana hawa leo, utalazimika kuwalipia gharama za kijamii, kiuchumi na kisiasa kesho,” amesema Dk Werema.
Amesema wizara hiyo itagusa takriban kila kona ya maisha. Kwa upande wa elimu, inaweza kuweka mkakati wa kuhakikisha mafunzo ya ufundi na stadi yanalingana na mahitaji ya soko, jambo ambalo limekuwa tatizo kwa muda mrefu.
Kwa upande wa ajira, amesema inaweza kutengeneza mpango wa kitaifa wa mafunzo kazini, kuwashirikisha waajiri kutoa nafasi za mafunzo ya vitendo kwa vijana na kuweka utaratibu wa uwajibikaji kwa taasisi zinazoshindwa kutekeleza hilo.
Dk Werema amesema washauri watakaoketi karibu na ikulu wanaweza kuratibu majadiliano ya mara kwa mara kati ya vijana na viongozi, kutoa mrejesho wa sera na kuhamasisha vijana kushiriki kwenye siasa bila woga.
“Kwa mantiki hiyo, hatua hii haipaswi kuonekana tu kama kuanzishwa kwa taasisi, bali kama kuundwa kwa mfumo mpya wa kufikiri kuhusu mustakabali wa taifa,” ameeleza.
Hata hivyo, amesema haitakuwa safari rahisi. Changamoto kama upatikanaji wa rasilimali za kutosha, uratibu wa taasisi za Serikali zilizozoea mfumo wa zamani na dhana kwamba masuala ya vijana yanaweza kusubiri, zinaweza kupunguza kasi ya mabadiliko yanayotarajiwa.