Kocha Barberian ana kazi ya kufanya Championship

BAADA ya Barberian kuchapwa mechi nne mfulilizo za Ligi ya Championship msimu huu, kocha wa kikosi hicho, Moris Katumbo ‘Kamongo’, amesema tatizo kubwa linaloikabili timu hiyo ni kukosa balansi katika eneo la kujilinda na la ushambuliaji.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kamongo amesema wachezaji wa timu hiyo kijumla wanacheza vizuri, japo muunganiko baina ya mmoja na mwingine ndiyo tatizo, kwa sababu wengi wao ni wapya na itawachukua muda kidogo kuzoeana kwa haraka kikosini.

“Tunacheza vizuri ila kiwango hakiendani na matokeo tunayopata, sisi kama benchi la ufundi tunaendelea kupambana na hali hiyo inayotukabili, ni mwanzo ila tuna kazi kubwa ya kufanya kutokana na ushindani uliopo msimu huu,” amesema Kamongo.

Kocha huyo aliyezifundisha pia timu ya Wanawake ya Mashujaa Queens na Kituo cha Vijana cha Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), amesema jambo lingine analopambana nalo ni kuwajenga wachezaji wa kikosi hicho kiakili na kisaikolojia.

Timu hiyo ambayo zamani ilikuwa ikifahamika kwa jina la Kiluvya United, kabla ya pambano la jana Jumapili nyumbani dhidi ya Mbuni, imecheza mechi nne na kuchapwa zote na kikosi hicho kimefunga mabao mawili tu na kuruhusu mengine manane.