Leo tutaongelea ubinafsi na uchoyo. Kwenye ndoa, sawa na kwenye maisha mengine, kuna wanandoa wabinafsi na wachoyo. Hii ni tabia chafu na mbaya sana.
Japo, kwa asili yake, binadamu ni mbinafsi, na wakati mwingine mchoyo, si jambo jema na linapaswa kuepukwa kwa gharama yoyote. Ubinafsi na uchoyo ni tabia mbaya isipokuwa kwenye eneo moja tu au mawili.
Katika tishio la kuondelewa uhai wake, binadamu ana haki ya kuwa mchoyo au kujihami kiasi cha kuondoa maisha ya yule anayetaka kuondoa wake.
Kadhalika, katika kummiliki mwenza wake. Na eneo hili ni kwa mwenza wake tu. Mfano, hakuna anayekubali mwenzi wake achukuliwe na mwenzake.
Ndiyo maana, visa vingi vya wanandoa kufumaniana na kuuana au kuachana si vigeni machoni mwa walio wengi. Hapa ndipo utata wa mitala hujitokeza hata tukiukandamiza, kuutetea, kuutafutia sababu na kuuhalisha.
Kwa hulka ya binadamu, kila mmoja hupenda upekee fulani. Awe na nyumba yake pekee ikiwa na maana ya mke na mume na vitu kama hivi. Awe na gari lake. Afaidi mambo au vitu vyake bila kuchangia wala kubughudhiwa na wengine.
Binadamu anapaswa kuchunga hata kuepuka sana ubinafsi na uchoyo katika maisha na nyanja zote isipokuwa kwenye tishio la maisha na umilki wa mwenza wake na mali zake.
Tofauti, katika mali, binadamu anaweza kugawa, kuuza, kuhonga, kuazima hata kuziharibu. Kwenye ndoa na uhai, hana chaguo isipokuwa kuwa mbinafsi na mchoyo.
Kwa mfano, kwa wanandoa, ubinafsi tofauti na ulioonyeshwa hapo juu, unatosha kuiyumbisha hata kuihatarisha ndoa. Hakika, wanandoa hawapaswi kuwa na changu katika ndoa bali chetu.
Hawapaswi kuwa na mimi bali sisi. Kwa wanaomkumbuka marehemu Malkia Elizabeth wa Uingereza, watakumubuka namna alivyokuwa ameolewa na mume Philip ambaye hakuwa mfalme kama yeye.
Hata hivyo, kutokana na dhana ya kuchangia na kumiliki kila kitu pamoja kwa wanandoa, Malkia alimpandisha cheo mumewe asiyetoka kwenye ukoo wake wa kifalme na kuwa mwana wa mfalme.
Kuna vitu ambavyo wanandoa wanaweza kudharau hata kutokumbuka. Kwa mfano, mmoja kati ya wanandoa kujaaliwa kipato kuliko mwenziwe. Kama ndoa yako imo kwenye hali hii, basi adui yako namba moja ni mafanikio unayoyaita yako badala ya yenu.
Je, huwa unasema pesa yetu, gari letu, nyumba yetu au mali zetu au zangu? Je, ulishamuuliza mwenzio hujisikiaje unapoonyesha wazi kuwa kila mtu ana chake na siyo chenu kama wanandoa?
Kujibu maswali hayo, vaa viatu vya mwenzio au jiweke kwenye nafasi yake. Jiulize ungejisikiaje kama mwenza wako angeendekeza tabia ya changu badala ya chetu?
Kunapokuwa, na changu na si chetu, basi kuna hatari kubwa kwa wahusika. Tunapoongelea hatari, madhara, na ubaya wa ubinafsi na uchoyo ni hapa. Mali na vitu vyote vinaweza kumilkiwa pamoja na kusiwe na tatizo.
Isitoshe, tunaweza kuvitumia kuwasaidia wengine wasio navyo lakini siyo ndoa. Japo ndoa umeikuta na kuifungia hapa duniani, ni tofauti na vitu vingine. Hii ni kwa sababu, hata ulipende lako vipi, huwezi kulala nalo wala kushindwa kuwapa lift wenzako kwa kutumia gari hilo hilo ulipendalo.
Hata upende vipi mashamba na wanyama wako, huwezi kulala navyo wala kuvitumia peke yako. Unaweza kuvinunua na kuviuza hata kuviazima kwa wengine.
Unaweza kuvigawa hata kuvirithisha. Unaweza kuajiri mtu au watu wengine kuvihudumia. Je unaweza kuajiri mtu mwingine kuhudumia mwenza wako awe wa kike au kiume kindoa?
Kwenye ndoa ya kweli, hakuna changu wala chako bali chetu. Hata hivyo, katika mfumo dume, tabia hii mara nyingi huwa nayo wanaume. Utamsikia mtu akisema, “nitakufukuza kwenye nyumba yangu” au “unafanya kiburi utafikiri wewe ndiye uliyejenga nyumba hii! Naweza kukuacha na kuingiza mwanamke mwingine.”
Yapo mengi yanayosemwa kuhusiana na umiliki wa mali. Kama nyumba yako au gari lako lilikuwa na thamani, kwanini hukuvioa? Kama una haki na jeuri hiyo, kwanini ulipoteza muda hata fedha zako kwenda kumtafuta, tena kwa kumbembeleza huyo unayemtishia maisha kwa sababu ya vitu?