KONA YA MZAZI: Wajibu wa wazazi malezi ya kizazi cha Gen Z

Katika dunia ya leo yenye mabadiliko ya kasi, vijana wa kizazi kipya kinachojulikana kama Generation Z wanakabiliwa na changamoto nyingi za kimaisha, kijamii, kiteknolojia na kimaadili.

Kizazi hiki ambacho kimekulia katika mazingira yanayotawaliwa na teknolojia, mitandao ya kijamii na utandawazi, kinaonekana kuwa na mtazamo tofauti kabisa kuhusu maisha, maadili na imani, ikilinganishwa na vizazi vilivyotangulia.

Wazazi, walezi na jamii kwa ujumla wanapaswa kutambua hali hii na kuchukua hatua makini za kuhakikisha vijana wao wanalelewa katika misingi imara ya kumcha Mungu na kuepuka mmomonyoko wa maadili.

Hivi karibuni nilipata wasaa wa kuzungumza na mtaalamu wa malezi, Joshua Mbwile ambaye alisema wazazi ndiyo wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuwasaidia vijana na watoto wao, kwa kuwa ndiye mlezi namba moja.

Mbwile anasema wazazi wanapaswa kurejea jukumu lao la msingi la malezi. Zamani, malezi yalikuwa jukumu la familia nzima; mtoto akifanya kosa, kila mtu katika jamii aliona anao wajibu pia wa kumkemea na kumrekebisha.

Lakini leo, mfumo huo unakosekana kwa kiwango kikubwa kutokana na mabadiliko ya maisha ya kisasa, majukumu mengi na upotevu wa muda unaosababishwa na matumizi ya teknolojia.

Wazazi wengi wanajikuta wakiwa na muda mdogo wa kuzungumza au kuwasikiliza watoto wao, jambo linalosababisha pengo la mawasiliano baina yao.

Ili kurekebisha hali hiyo, mtaalamu huyo wa malezi anasema wazazi wanapaswa kujenga utamaduni wa mawasiliano ya wazi na ya upendo na ya mara kwa mara na watoto wao.

Mazungumzo ya familia, sala za pamoja, au hata chakula cha jioni cha familia kila siku vinaweza kuwa nyenzo muhimu ya kujenga uhusiano wa karibu unaochochea uelewano na ushauri wa kimaadili, anasisitiza Mbwile.

Nami nikapata wazo kuwa kumbe ni muhimu wazazi wawe mfano wa kuigwa. Vijana wa Gen Z hawafundishwi kwa maneno pekee, bali hujifunza zaidi kwa kuona mwenendo wa watu wazima wanaowazunguka.

Kama mzazi anasema jambo moja na kutenda kinyume chake, mtoto ataamini kitendo zaidi ya maneno. Hivyo basi, ili watoto wakue wakimcha Mungu, lazima wazazi waoneshe maisha ya kiimani, uadilifu na heshima kwa wengine. Watoto wanaposhuhudia wazazi wao wakimwomba Mungu, kushiriki ibada, kuishi kwa uaminifu na kuheshimu watu wote bila ubaguzi, nao hujifunza kuishi kwa namna hiyo.

Katika enzi hii tuliyonayo ya mitandao ya kijamii, wazazi wanapaswa kuwa na uelewa wa kina kuhusu teknolojia na athari zake. Lakini wengi wamekuwa wakilalamika kuhusu matumizi mabaya ya mitandao kama TikTok, Instagram, na X (zamani Twitter), lakini hawajui namna bora ya kuwasaidia watoto wao kuyatumia kwa manufaa.

Badala ya kukataza tu, wazazi wanapaswa kuwafundisha vijana kutumia teknolojia kwa tija, hivyo ni jukumu la mzazi kuweka mipaka, lakini pia kuwasaidia vijana kuelewa sababu za mipaka hiyo, ili wajifunze kuwajibika kwa hiari.

Changamoto nyingine kubwa ni mmomonyoko wa maadili unaochochewa na tamaduni za kigeni na maisha ya anasa yanayochagizwa na vyombo vya habari.

Wapo baadhi ya watu husema vijana wanapokosa msingi wa kiroho, ni rahisi kuiga kila kinachoonekana cha kisasa, hata kama kinapingana na maadili ya jamii.

Hapa ndipo umuhimu wa elimu ya dini na maadili unapojitokeza. Wazazi wanapaswa kushirikiana na taasisi za dini kuhakikisha watoto wanapata elimu ya kiimani tangu wakiwa wadogo.

Elimu hii siyo tu kufundisha kusali au kuhudhuria ibada, bali kuwajenga katika maadili kama uaminifu, unyenyekevu, huruma na kujituma.

Zaidi ya hayo, wazazi wanapaswa kuwahimiza vijana kuwa na malengo ya maisha yanayozingatia thamani na huduma kwa wengine.

Nasema hivyo kwa sababu kizazi cha leo kimezidi kutawaliwa na tamaa ya umaarufu wa haraka na maisha ya kifahari, jambo linalosababisha wengi kukata tamaa au kuchukua njia zisizo sahihi ili kufikia matamanio yao.

Hivyo wazazi wanapaswa kuwasaidia watoto kutambua kuwa mafanikio ya kweli yanatokana na bidii ya kazi, nidhamu na kumtegemea Mungu.

Kwa jumla, kizazi cha Gen Z si kizazi kilichopotea, bali ni kizazi chenye uwezo mkubwa wa kubadilisha dunia, endapo kitapata malezi sahihi.

Hivyo, wazazi wanapaswa kutambua kuwa kumcha Mungu na kuwapendeza watu ni matokeo ya malezi yanayoanzia nyumbani.

Ni wakati sasa wa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kusimama kidete kuhakikisha vijana wanakua katika mazingira yanayowajenga kiroho, kiakili na kimaadili.