BEKI wa kulia wa Kagera Sugar, Yusuph Iddy ‘Kiba’, amesema licha ya kucheza kwa mara ya kwanza na timu hiyo msimu huu, ila amefurahia mwanzo mzuri na ushirikiano anaoupata kutoka kwa wachezaji wenzake, jambo linalompa matumaini makubwa.
Nyota huyo aliyejiunga na timu hiyo msimu huu akitokea Mbeya Kwanza inayoshiriki pia Ligi ya Championship, amesema moja ya malengo yake ni kuhakikisha wanapambania kikosi hicho na wachezaji wenzake, ili kirejee tena katika Ligi Kuu Bara.
“Nimekuwa na mwanzo mzuri jambo ambalo kwangu linanipa motisha ya kuendelea kupambana zaidi, ushindani ni mkubwa kama ilivyo kila msimu, ila ubora wa wachezaji waliopo hapa na benchi la ufundi naamini tutafikia malengo,” amesema Yusuph.
Beki huyo aliyewahi pia kuichezea Pan Africans, alisajiliwa na kikosi hicho msimu huu kwa lengo la kuchukua nafasi ya aliyekuwa nyota mwenzake katika timu hiyo, Datius Peter, ambaye aliondoka na kujiunga na ‘Wakata Miwa’ Mtibwa Sugar.
Kikosi hicho kilichodumu Ligi Kuu Bara kwa miaka 20, tangu kilipoanza kushiriki 2005, kilishuka daraja msimu wa 2024-2025, baada ya kushinda mechi tano, sare minane na kupoteza 17, kikishika nafasi ya 15, kufuatia kukusanya pointi 23.
Kagera inayofundishwa na Juma Kaseja aliyeichezea akiwa mchezaji na kocha wa makipa, sambamba na Simba, Yanga na timu ya taifa ya Tanzania, imecheza mechi tano hadi sasa, ikishinda nne na kutoa sare moja, ikiwa nafasi ya kwanza na pointi 13.