TAIFA Stars chini ya Kocha Miguel Gamondi, juzi usiku ilikumbana na kipigo cha mabao 4-3 kutoka kwa Kuwait, huku kikimchefua kocha huyo akiwatupia lawama wachezaji kwa kushindwa kulinda ushindi wa mabao 2-0 ya kipindi cha kwanza.
Kaimu kocha mkuu huyo wa Stars, amesema amechukizwa na makosa ya kujirudia yaliyotokea juzi, Jumamosi, wakati akiiongoza timu hiyo kwa mara ya kwanza kwenye mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Kuwait iliochezwa jijini Cairo, Misri.
Stars ilianza vizuri mechi hiyo, ikitawala sehemu kubwa ya kipindi cha kwanza na kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 2-0 kupitia kwa Charles M’Mombwa na Tarryn Allarakhia, hali iliyowapa Watanzania tumaini ya kuiona timu ikipata ushindi wa kwanza chini ya Gamondi.
Hata hivyo, mambo yalibadilika kipindi cha pili na Stars ilijikuta ikiruhusu mabao manne ndani ya dakika 24, hali iliyoonyesha kupungua kwa umakini. M’Mombwa alifunga bao lake la pili ambalo lilikuwa la tatu kwa Stars, lakini halikutosha kuzuia kipigo cha mabao 4-3.
Gamondi amesema makosa yaliyofanyika hayapaswi kuonekana kwenye timu ya taifa, hasa baada ya kuonesha kiwango bora dakika 45 za kwanza.
“Tulicheza vizuri kipindi cha kwanza, tulikuwa watulivu na tulijua tunachokitafuta. Lakini dakika chache za mwanzo za kipindi cha pili ziliharibu kila kitu. Hatuwezi kuruhusu mabao matatu au manne kwa makosa yanayojirudia. Hili ni jambo ambalo lazima tulimalize mara moja.”
Kocha huyo aliongeza tatizo halikuwa uwezo wa wachezaji, bali ni kupoteza umakini, amesema kiwango cha kipindi cha kwanza kinaonyesha mwanga mzuri wa timu hiyo, lakini kupotea kwa dakika tano hadi 10 kumewagharimu.
“Timu ililegea, ikapungua kasi na ikaanza kufanya maamuzi yasiyo sahihi. Huko ndiko mchezo ulipoanza kugeuka. Katika mashindano ya kimataifa, huwezi kucheza kwa kuamini mabao mawili yanakutosha. Lazima ubaki makini hadi mwisho,” amesema.
Gamondi ameeleza pamoja na matokeo hayo, amejifunza mengi kuhusu tabia ya timu hiyo katika muda mfupi, hususani katika maeneo ya ukomavu wa kiushindani, mawasiliano kati ya safu za ulinzi na kiungo, pamoja na uamuzi wa kubadilika kulingana na presha ya mechi.
Hata hivyo, licha ya kukerwa na makosa yaliyotokea, Gamondi alikiri kuwepo kwa mambo chanya na kiwango cha kipindi cha kwanza kimemuonesha kuwa timu ina uwezo mkubwa wa kucheza soka la kuvutia endapo itakuwa na nidhamu ya mchezo kwa muda wote.
Kipigo hicho cha Stars ambayo ni moja ya timu zilizofuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 zitakazoanza Desemba 21 huko Morocco ikiwa kundi moja na Tunisia, Nigeria na Uganda ni cha nne mfululizo, kwani awali ikiwa chini ya Hemed Suleiman ‘Morocco’ ilipoteza tatu zikiwamo mbili za mashindano na moja ya kirafiki.
Ilianza kwa kupoteza katika mechi za kuwania fainali za Kombe la Dunia 2-26 kwa kuchapwa bao 1-0 na Niger kabla ya kutandikwa pia 1-0 na Zambia na kupoteza 2-0 mbele ya Iran zilipovaana kirafiki kwenye Uwanja wa Al Rashid uliopo Dubaim, UAE.
Katika viwango vya ubora wa soka vya Fifa Stars inakamata nafasi ya 107 huku Kuwait ikiwa ya 135.