Sowah, Mutale wampa Xavi jina jipya Simba

BAADHI ya mastaa wa Simba, wakiwamo Jonathan Sowah na Joshua Mutale wamemtungia jina jipya kocha anayesimamia mazoezi ya viungo, Mohamed Mrishona ‘Xavi’ wakimuita kwa sasa ‘Mr Quickly Quickly’ kutokana na kufanya mambo yake kwa uharaka.

Xavi amesema kiongozi wa utani huo ni mshambuliaji Sowah kila anapomwona anamwita kwa jina hilo, wengine ni Shomari Kapombe, Joshua Mutale na kiungo mpya Alassane Kante.

“Mastaa wote wa Simba ni wacheshi na wananipenda sana, kama unavyojua mpira wa miguu ni burudani na wananiona ni kijana, ndiyo maana wapo huru kunitania ili mradi wanazingatia mazoezi ninayowapa, mfano nikianza kujitokeza mbele yao Sowah anaanza kusema Mr Quickly Quickly anakuja,” amesema Xavi na kuongeza;

SOW 01


“Mazoezi yangu mchezaji lazima awe na ufiti na pumzi, hivyo inakuwa ngumu kama hawana vitu kama hivyo.

“Kuhusu ninavyojigawa kufanya kazi timu kubwa nafanya nao mazoezi asubuhi, Simba B jioni na mazoezi ya wachezaji binafsi nafanya usiku, hivyo muda wangu wa kumzika nikuanzia saa tatu usiku hadi saa moja asubuhi.”

Amesema kitendo cha kufundisha mazoezi ya viungo kwa timu kubwa kimemuongezea ari ya kuendelea kutamani kusoma na malengo yake ni kuwa kocha mkubwa Afrika.

SOW 02


“Nina Diploma A ya CAF katika mambo ya ukocha pia nimesoma kwa kiasi ukocha wa viungo na naendelea kusoma, ili mbele ya safari nije nifanye vitu vikubwa Afrika.”

Alipoulizwa kuhusiana na tetesi za kutakiwa na timu nyingine za Ligi Kuu alijibu: “Ninachoamini siku zote katika maisha yangu ni muda ndio unazungumza ukweli, hivyo siwezi kulizungumzia hilo kwa sasa, jambo la msingi ninatamani kutoka sehemu moja kwenda nyingine.”