Arusha. Mahakama ya Rufaa iliyoketi Dodoma, imetupilia mbali ombi la John Ngonda, aliyehukumiwa kifungo cha maisha jela, aliyekuwa akiomba kuongezewa muda wa kuwasilisha maombi ya mapitio ya uamuzi wa awali wa Mahakama ya Rufaa.
Ngonda alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela na Mahakama ya Wilaya ya Kiteto baada ya kukutwa na hatia ya kumbaka mtoto wake wa kambo aliyekuwa na umri wa miaka minane.
Hata hivyo, katika rufaa yake ya kwanza adhabu iliongezwa hadi kifungo cha maisha jela, rufaa yake ya pili (Mahakama ya Rufaa) ilitupiliwa mbali na jopo la majaji watatu, Februari 15, 2023 kwa kukosa sifa.
Katika maombi ya sasa, Ngonda alikuwa na sababu tatu za rufaa ambapo alidai alichelewa kuomba mapitio kwa sababu hakuwa na uelewa na muda unaotakiwa kisheria na uamuzi wa awali una makosa.
Sababu ya tatu alidai alinyimwa haki ya kusikilizwa kimakosa hivyo mwombaji anatarajia kutegemea Kanuni ya 66(1) (a)(b) ya Kanuni za Mahakama ya Rufani ya mwaka 2009 kama ilivyorekebishwa.
Mwombaji huyo alikiri kupokea nakala ya hukumu Februari 24, 2023 lakini hakueleza mahakama hatua alizochukua baada ya hapo hadi alipowasilisha ombi hilo Desemba 21, 2023.
Uamuzi wa maombi hayo ya jinai namba 13/2024 umetolewa na Jaji Zainab Muruke, Novemba 14, 2025 na nakala yake kuwekwa kwenye mtandao wa Mahakama.
Baada ya kupitia hoja za pande zote mbili, Mahakama hiyo ilitupilia mbali maombi hayo kutokana na mwombaji kushindwa kuwasilisha sababu za kisheria zinazojitosheleza kumuongezea muda wa kuwasilisha maombi ya mapitio.
Wakati wa usikilizwaji wa maombi hayo, Ngonda alijiwakilisha mwenyewe bila kuwa na wakili huku Jamhuri akiwakilishwa na Wakili wa Serikali, Neema Mbwana.
Akijibu maombi hayo, Wakili Neema alianza kwa kueleza msimamo wake kwamba haungi mkono maombi hayo ya kuongeza muda, ambapo mwombaji anapaswa kuonyesha sababu za kuchelewa kuwasilisha maombi.
Alisema mahakamani hapo kuwa hukumu ilitolewa Februari 14, 2023 na Ngonda alipewa nakala ya uamuzi huo Februari 24, 2023 na kuwa kwa mujibu wa sheria alipaswa kuwasilisha maombi hayo ndani ya siku 60 na sababu ya kutojua muda wa kuwasilisha mapitio haijitoshelezi, kwa vile kutojua sheria si utetezi.
Wakili huyo aliiomba mahakama kutupilia mbali maombi hayo kwa kuwa hayana sifa kisheria.
Mwombaji huyo alisisitiza akiwa gerezani hakuwa na ufahamu wa muda wa kuwasilisha mapitio kwa wakati na kuiomba Mahakama kukubali maombi yake, ili awasilishe mapitio yake yaliyokusudiwa.
Jaji Muruke amesema baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, suala la uamuzi ni kama mwombaji ametoa sababu za kutosha kuitaka Mahakama kutumia uamuzi wake wa kuongeza muda.
Alisema katika kutekeleza uamuzi wake, kama kuongeza au kutoongeza muda Mahakama inatakiwa kuzingatia ikiwemo mwombaji lazima aeleze na kuthibitisha sababu za kuchelewa ikiwa ni pamoja na bidii aliyotumia, lakini siyo uzembe na ucheleweshaji usiwe wa kupita kiasi.
Jaji Muruke aliongeza misingi ya kisheria inaelekeza kuwa Mahakama inaweza kuongeza muda kama kuna hoja nzito ya kisheria au uharamu wa uamuzi unaotakiwa kupingwa.
Jaji alisema kwa mujibu wa hati ya kiapo ya mwombaji sababu ya kuchelewa kuwasilisha maombi hayo ni mwombaji kutojua lini anapaswa kuyawasilisha.
“Aya iliyo hapo juu inaelezea sababu za kuchelewa. Kwa maoni yangu na kwa macho ya sheria sababu hazijitoshelezi kwa sababu zifuatazo: Kwanza, mwombaji hakutoa maelezo yoyote juu ya hatua gani alichukua baada ya uamuzi wa Februari 14, 2023 hadi alipopewa nakala ya hukumu ya Mahakama Februari 24, 2023,” alisema Jaji.
“Ilitarajiwa mwombaji awe ameandika hata barua kwa Msajili amkumbushe kupewa nakala ya hukumu. Nakala ya barua hiyo ingeweza kuambatishwa katika hati ya kiapo kuunga mkono notisi ya maombi. Kinyume chake, hakuna kitu katika hati ya kiapo kuelezea hatua alizochukua kipindi chote hicho,” aliongeza.
Jaji Muruke alisema mwombaji ameshindwa kueleza hatua alizochukua kipindi anasubiri nakala ya hukumu, hakutoa ushahidi au barua yoyote kuonyesha alijitahidi kufuatilia suala hilo akiwa gerezani, hakuthibitisha makosa ya wazi kwenye rekodi kama alivyowasilisha ambalo lingeweza kuhalalisha mapitio.
Jaji Muruke amesema mwombaji ameibua suala la kutojua muda wa kuwasilisha mapitio kama msingi wa kuongeza muda na kuwa imeamuliwa kisheria kwamba mtu ambaye hajui sheria hawezi kuepuka dhima kwa kukiuka sheria kwa kutojua maudhui yake.
Jaji Muruke alihitimisha kwa kueleza kuwa kutojua sheria hakuwezi kuzingatiwa kama sababu ya kutosha na kukataa ombi hilo kwani mwombaji hajatoa sababu za kujitosheleza na kutupilia mbali.