KWA mara nyingine Wabongo wawili wanaokipiga FC Masar ya Misri, Hasnath Ubamba na Violeth Nickolaus, wameandika rekodi ya kutinga nusu fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kutoka sare ya 1-1 na USFAS kwenye mechi ya kundi A.
Mechi hiyo ilipigwa kwenye Uwanja wa Right to Dream, Masar wakiwa wenyeji wa mashindano hayo walitanguliwa kipindi cha kwanza kabla ya kusawazisha dakika za mwisho.
Hii ni rekodi nyingine wanaandika nyota hao kuipeleka timu nusu fainali ikiwa ni mara yao ya pili kwenye historia ya maisha ya soka.
Nyota hao wamekuwa na msaada mkubwa kwa timu hiyo wakicheza mechi zote na kuonyesha kiwango kikubwa kilichowafanya baadhi ya mashabiki waliohudhuria mechi hiyo kuwashangilia.
Katika usiku ule Ubamba aliondoka na tuzo ya Woman of the Match na sio kwa kubahatisha kutokana na kiwango bora alichoonyesha akiiwezesha timu kusawazisha bao na kupata pointi moja iliyowapeleka nusu fainali. Kwa matokeo hayo sasa Masar itakutana na bingwa mtetezi, TP Mazembe katika nusu fainali na hiyo ni baada ya kumaliza katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi B ikiwa na pointi sita nyuma ya vinara Asec Mimosas ya Ivory Coast waliomaliza na pointi saba.
Akizungumza baada ya kunyakua tuzo hiyo, Ubamba amesema: “Nashukuru kwa tuzo hiyo nawa-shukuru wenzangu kwa kushirikiana pamoja na kuisaidia timu ifuzu hatua inayofuata.”