Mapendekezo ya wadau ya kuondoa uzuiaji wa maiti hospitalini

Dar es Salaam. Wakati uzuiaji wa maiti hospitalini kutokana na gharama za matibabu ukiwa ni mfupa mgumu nchini, ili kutokomeza tatizo hilo, wadau wameishauri Serikali kuhakikisha inaweka mifumo sahihi na thabiti ya ugharamiaji wa afya.

Wametaja bima ya afya, kuimarishwa kwa mfuko wa ustawi wa jamii, na Serikali kutenga fedha kama ruzuku za kulipia matibabu ya watakaopoteza maisha, yatasaidia zaidi na haraka kushughulikia suala hilo.

Septemba 18, 2021, mwili wa Zena Ramadhan ulizuiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kutokana na deni la Sh1.6 milioni la gharama za matibabu. Tukio kama hilo lilitokea Oktoba 2021 katika Hospitali ya Bugando mkoani Mwanza, mwili wa Rosemary Morumbe ulipozuiwa kwa deni la Sh2.4 milioni la gharama za matibabu.

Kama hiyo haitoshi, ndugu na jamaa wa Mohamed Hassan, aliyefariki dunia katika Hospitali ya Mount Meru mkoani Arusha, walishindwa kuuchukua mwili wake baada ya hospitali kuuzuia hadi lilipwe deni la Sh910,000 za matibabu.

Matukio hayo yalitokea licha ya maelekezo na waraka mbalimbali kutolewa na viongozi wa Serikali, wakitaka hospitali, hasa za umma, zisizuie maiti kwa ndugu na jamaa wasio na uwezo wa kulipa gharama za matibabu.

Sio hivyo tu, suala hilo liliendelea kutokea hata baada ya Serikali kutoa Waraka Namba Moja wa mwaka 2021 wa kutozuia maiti na kuweka utaratibu wa kulipa gharama za matibabu na madeni kwa miili.

Kulingana na kifungu cha 3.1.4 cha waraka huo, “Iwapo ndugu wa marehemu hawatakuwa na uwezo wa kulipa deni pale mgonjwa atakapokuwa amefariki, ndugu wataingia makubaliano ya maandishi na kituo cha kutolea huduma kuhusu namna ya kulipa deni na waruhusiwe kuchukua mwili.”

Uhalisia huo umeibua mashaka kwa wadau mbalimbali wa sekta ya afya, wanaoonesha shaka kuhusu mpango wa Serikali kukomesha uzuiaji wa maiti katika vituo vya huduma za afya, kama ilivyoelezwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Katika hotuba yake ya kufungua Bunge la 13 jijini Dodoma Novemba 14 mwaka huu, Rais Samia alisema ameshaielekeza Wizara ya Afya kusimamia maelekezo ya kutozuiwa kwa maiti kwenye vituo vya afya, wakati familia zikiendelea na taratibu za kulipa deni la matibabu kwa njia zinazolinda utu wao.

“Niseme kwamba ni kupitia mpango huu wa bima ya afya, kadhia hii inakwenda kukomeshwa. Gharama za matibabu zitalipwa na bima ya anayetibiwa,” alisema Rais.

Aliwasihi wananchi wote kuweka kipaumbele kwa afya zao kwa kuhakikisha kila mmoja ana bima ya afya, pamoja na wanaomtegemea.

Kauli hiyo ilitokana na ahadi yake wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 29, mwaka huu, aliposema kwamba ndani ya siku 100 za urais wake, atatokomeza uzuiaji wa maiti katika vituo vya kutolea huduma za afya vya Serikali.

Agizo hilo limewahi kutolewa na aliyewahi kuwa Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, alipokuwa katika ziara ya Makonda Januari 20, 2024, mkoani Tanga.

Agosti 22, 2018, aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Afya, marehemu Dk Faustine Ndugulile, aliwahi kuiambia Hospitali ya Muhimbili na Mloganzila kwamba, “Siyo jukumu la Serikali kuzika, maana kung’ang’ania mwili wakati ndugu wanahitaji kumhifadhi ndugu yao, inaleta maana gani?”

Pia, mara kadhaa aliyewahi kuwa Rais wa Awamu ya Tano, hayati John Pombe Magufuli, alikuwa akikemea suala hilo.

Mmoja wa viongozi wa hospitali za umma nchini (jina lake linahifadhiwa) anasema kilichokuwa kinakwaza utekelezaji wa hilo ni kukosekana kwa utaratibu mzuri wa wafiwa kulipa deni baada ya kupewa mwili.

Anasema sio dhamira ya kiongozi wa hospitali kuzuia maiti, lakini anafanya kazi chini ya miongozo, taratibu, vigezo na vipimo vya ufanisi. Baadhi ya vipimo hivyo ni utoaji wa huduma na kuingiza faida.

“Ukimruhusu mtu achukue mwili na hakukuwa na utaratibu mzuri wa kuhakikisha analipa deni, wewe kiongozi ndiye unabaki na changamoto kwa sababu hutaeleweka na bosi wako.

“Mara nyingi wakati wa ukaguzi wa mahesabu, ukiwaambia niliruhusu jamaa wachukue mwili wakiwa na deni la gharama za matibabu na hawakulipa hadi sasa, hakuna anayekuelewa na unaweza kupoteza kibarua chako,” anasema.

Kiongozi huyo anaeleza baadhi ya hospitali, ikiwemo anayoiongoza, wamewahi kutoa mwili kwa ndugu kwa makubaliano ya kulipa baadaye, wengi hawakulipa wala kupatikana tena.

“Unafanya utu, wenzio wanaona haki yao, wanapotea kabisa na hawawaoni tena. Kwa sababu unafanya kazi kwa vipimo vya ufanisi, wakati mwingine unajikuta unalipa deni kwa mshahara wako au posho yako ili uzibe pengo. Haya ndio tuliyokuwa tunapitia,” anasema.

Kwa kutambua uhalisia huo, anasema ndio maana haikuwahi kusikika Serikali au kiongozi yeyote akitangaza kuchukulia hatua kiongozi wa hospitali iliyozuia maiti.

“Viongozi wenyewe wanajua uhalisia, kama yangekuwa makosa ya uwajibikaji, ungeona wakuu wa hospitali wakichukuliwa hatua,” anasema.

Wakati hali ikiwa hivyo, anasema mpango wa Rais Samia unaweza kuja kwa njia tofauti na hatimaye ukazaa matunda tarajiwa, tofauti na ilivyokuwa kabla, ikiwa mambo yafuatayo yatazingatiwa:

Kuharakishwa kwa bima ya afya kwa wote na kila mwananchi kuhamasishwa kuwa na bima, hiyo itaepusha madeni ya gharama za matibabu kabisa.

Ukiacha bima, kiomgozi huyo anapendekeza makubaliano ya ndugu na hospitali wakati wa kuchukua mwili unaodaiwa gharama za matibabu yafanywe kwa kuhakikisha anayeandika anaacha taarifa zake muhimu ili apatikane.

Lingine, anasema katika ruzuku zinazotolewa na Serikali kwa hospitali, iwepo ya dharura inayolenga kulipia madeni ya watu watakaopoteza maisha.

“Kama mfuko wa ustawi wa jamii uimarishwe na kurahisisha kufikika au Serikali yenyewe iwe inatenga fungu kwa kila hospitali kwa ajili ya kulipia madeni ya wagonjwa watakaofariki,” anasema.

Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Mugisha Nkoronko, anasema huduma za afya kiutaratibu zina gharama, hivyo yeyote anapoumwa anapaswa kulipa ili apate matibabu.

Bila kujali mgonjwa amepoteza maisha au amepona na kurudi nyumbani, hatua ya kuruhusiwa kutoka hospitali itatokana na hakikisho kwamba amelipa gharama za matibabu.

Kwa aliyepona, anasema haruhusiwi kuondoka hospitali hadi alipie matibabu, huku aliyefariki, mwili hauondolewi bila kulipiwa ikiwa kuna deni.

“Huu ndio ukweli, kwa sababu matibabu yanalipiwa. Ukisema usizuie maiti katika mazingira hayo, utafanya leo lakini kesho utajikuta umerudia,” anasema.

Namna ya kufanikisha kuondoa changamoto ya uzuiaji wa maiti hospitalini, anasema ni Serikali kuhakikisha inaweka mifumo sahihi na thabiti ya kugharimia afya za wananchi wake.

“Kuwe na mazingira yanayoifanya Serikali yenyewe ilipie gharama za matibabu, ili kusitokee mazingira ya mgonjwa kubaki na deni, hilo litakuwa muarobaini,” anasema.

Anasisitiza ziwepo njia za kugharimia matibabu ya wananchi ama kupitia bima ya afya kwa wote au vinginevyo.

“Muhimu kabisa ni watu watibiwe na kiongozi atangaze kuwatibu bure wananchi. Hiyo itafanya watu wasiwe na madeni na haitatokea maiti kuzuiwa,” anasema.

Inatekelezeka ni utashi tu

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Profesa Abel Makubi, anasema hakuna ugumu katika utekelezaji wa hilo, hasa kama hospitali husika itakuwa na utashi wa kufanya hivyo.

Sio vigumu, kwa sababu kupotea kwa maisha ya mgonjwa ni kubwa na lina utu ndani yake, hivyo Rais Samia ana nia njema na inatekelezeka.

Alipoulizwa iwapo hospitali zinaweza kushindwa kutekeleza kwa hofu ya kupoteza mapato, Profesa Makubi anasema hakuna hasara ya fedha mbele ya utu wa mtu, akisisitiza linatekelezeka.

“Hakuna hasara ya kupoteza mapato mbele ya utu wa mtu. Sioni kama hilo lina shida, mfano kwetu hapa Benjamin Mkapa haukuwahi kusikia malalamiko ya wananchi. Ni jambo linalotekelezeka,” anasema.

Hata hivyo, Profesa Makubi anssema utekelezaji wa hilo utakuwa rahisi zaidi hasa ukizingatia Serikali ipo katika hatua nzuri za kuanza utoaji wa bima ya afya kwa wote.

“Bima ya afya kwa wote maana yake, kila mwananchi atakuwa na bima au idadi kubwa watakuwa na bima. Mtu akiwa na bima, akiumwa, bima yake ndiyo inayolipa, hata kama amefariki, bima yake ndiyo italipa, haiwezekani awe na deni,” anasema.