Kidato cha nne kuanza mitihani kesho, wanafunzi 311,986 wakiachia njiani

Dar es Salaam. Wanafunzi 595,816 wanatarajia kuanza mtihani wa kumaliza elimu ya sekondari kuanzia kesho Jumatatu, Novemba 17, 2025, ikiwa ni kukamilisha safari yao ya miaka minne.

Idadi ya watahiniwa wanaotarajiwa kuketi kesho kwenye mtihani ni sawa na asilimia 65.63 ya wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2022 ambao ni 907,802.

Hiyo ikiwa na maana kuwa, wanafunzi 311,986 hawakuweza kufikia udahili wa kufanya mtihani huo.

Januari 23, 2025, Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) lilipotangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha nne ya watahiniwa waliofanya mtihani 2024 ilisema jumla ya watahiniwa 557,706 walisajiliwa kufanya mtihani huo.

Hata hivyo, uchunguzi wa Mwananchi ulibaini mwaka 2021 wanafunzi hao walijiunga kidato cha kwanza wakiwa 759,706.

Taarifa iliyotolewa na Tamisemi ilionyesha wanafunzi 759,706 sawa asilimia 91.1 kati ya wanafunzi 759,737 waliokuwa na sifa za kujiunga na kidato cha kwanza, wamechaguliwa mwaka 2021.

New Content Item (1)


New Content Item (1)

Swali ni je, wanafunzi 201,910 walioanza kidato cha kwanza mwaka 2021 na kumaliza kidato cha nne mwaka 2024 wako wapi?

Kupotea kwenye mfumo kwa wanafunzi hao ni ongezeko la zaidi ya asilimia 50 ya wanafunzi waliopotea mwaka 2023.

Takwimu zinaonyesha jumla ya watahiniwa 572,338 walisajiliwa kufanya mtihani wa kidato cha nne 2023 japo walioanza kidato cha kwanza walikuwa 701,038.

Hii inamaanisha kuwa, jumla ya wanafunzi 128,700 walipotea kwenye mfumo kipindi cha 2023 swali likiwa lilelile, walipotelea wapi?

Taarifa ya Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Said Mohammed ya leo Jumapili, Novemba 16, 2025, inaeleza idadi ya watahiniwa wa mwaka huu ni ongezeko la asilimia 7.67 ikilinganishwa na wa mwaka 2024.

Watahiniwa hao wanatoka katika jumla ya shule za sekondari 5,868 na vituo vya watahiniwa wa kujitegemea 813, kati yao 569,914 ni watahiniwa wa shule na 25,902 ni watahiniwa wa kujitegemea.

Kati ya watahiniwa wa shule 569,914 waliosajiliwa mwaka 2025, wavulana ni 266,028 sawa na asilimia 46.68 na wasichana ni 303,886 sawa na asilimia 53.32.

“Pia wapo watahiniwa wa shule 1,128 wenye mahitaji maalumu ambapo kati yao, wenye uoni hafifu ni 860, wasioona ni 70, uziwi ni 58, wenye ulemavu wa akili ni watano na wenye ulemavu wa viungo ni 135,” amesema.

Kati ya watahiniwa wa kujitegemea 25,902 waliosajiliwa, wavulana ni 10,862 sawa na asilimia 41.93 na wasichana ni 15,040 sawa na asilimia 58.07.

“Pia katika watahiniwa wa kujitegemea wapo wenye mahitaji maalumu 56. Kati yao, wenye uoni hafifu ni 49 na wasioona saba,” amesema.

Alipotafutwa na Mwananchi, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Caroline Nombo amesema wanataka kutengeneza mfumo mzuri wa kukusanya takwimu ili kuondoa mkanganyiko uliopo sasa.

Amesema mfumo huo pia utasaidia kufanya ufuatiliaji wa mwanafunzi tangu anapoanza shule ya awali yoyote iwe ya Kiingereza, kimataifa au Serikali ili kurahisisha kujua wanafunzi wako wapi na wanafanya nini.

“Sitaki kuamini kuna mdondoko kwa kiasi hiki, tunatakiwa kuthibitisha hizi takwimu, lakini kupitia mfumo huu tutaweza kujua kwani tunatambua kuna wengine wanakariri, wengine wanahama nchini lazima tuzithibitishe. Hata akienda mfumo wowote lazima tujue,” amesema Profesa Nombo.

Amesema ujio wa namba ya jamii itakayokuwa ikisajili watoto tangu wanapozaliwa pia itakuwa na mchango chanya katika kurahisisha ufuatiliaji wa wanafunzi tangu wanapoandikishwa shule ili kusaidia kujua wanatoka wapi wanakwenda wapi.

“Lakini hata wanaoondoka, Serikali imeweka nafasi ya wao kurudi tena shuleni na wapo wengi waliorudi katika mfumo usio rasmi na wengine wamerudi katika mfumo rasmi, wengi wamerudi na wengine wameenda hata vyuo,” amesema.

Ameeleza kuwa Serikali pia inasaidiana na jamii ili kuhakikisha watoto wanaandikishwa shule, kufuatilia maendeleo yao kwa kuhakikisha vijana wanakwenda shule, wanabaki shule, huku wakitengenezewa mazingira mazuri.

“Sisi kama Serikali tunapunguza umbali wa wanafunzi kwenda shule kwa kujenga shule katika maeneo wanayoishi. Hii imekuwa na faida kwani watoto wanakwenda shule na kurudi kirahisi, sambamba na kujenga mabweni,” amesema.

Akizungumzia mdondoko wa wanafunzi, mchambuzi wa elimu, Ochola Wayoga, amesema kupungua kwa asilimia 34 ya wanafunzi ni kama kuwafelisha watoto, hivyo ni vyema kufanyika utafiti ili kujua wako wapi na wanafanya nini.

“Walioacha shule tungeweza kufanya utafiti kwa sababu watoto hawawezi kuacha masomo ikiwa hakuna viashiria vya awali, lazima viwepo kwa mtoto yeyote tuangalie namna ya kushughulika navyo,” amesema.

Hilo lifanyike wakati mfumo wa elimu ukiangaliwa kama unawavutia wanafunzi, huku akishauri kuangaliwa njia nyingine ndani na nje ya mfumo wa elimu ambazo watoto wanaweza kwenda na kuwa salama.

“Tunategemea elimu ili kumfungua mtoto kiufahamu kuliko wale ambao hawajasoma, lakini ni vyema kuangalia mfumo mzima kuanzia ngazi za chini na wote wanaohusika, ikiwemo wazazi, walimu, vyombo vya sheria, kata, tarafa. Hii inaonesha mfumo wetu umefeli, huwezi kuwa na wanafunzi zaidi ya 900,000 wakamaliza 500,000,” amesema.

Amesema ni vyema kuboresha mifumo na miundombinu ya shule kama madarasa, vyoo, walimu, ili wanafunzi waweze kukaa madarasani.

“Ni vyema kufanya mapitio kuangalia nini hakifanyi kazi katika mfumo wa elimu kuendana na elimu ya karne ya 21, kwa kuweka vipaumbele sawa ili kuhakikisha mazingira mazuri ya kujifunzia yanawekwa, ili wanafunzi wakae darasani,” amesema.

Mtafiti wa elimu, Muhanyi Nkoronko, amesema asilimia hiyo 30 huenda inaonyesha kuna wanafunzi wameacha, wamerudia au hawajasajiliwa, ikiwa na maana mfumo wa elimu hauwawezeshi wanafunzi kuanza kidato cha kwanza hadi kumaliza kidato cha nne bila kurudia darasa au kuacha.

“Namna bora ya kupunguza hali hii ni kuwepo kwa juhudi za makusudi kuhakikisha sababu zinazomfanya mwanafunzi kuacha masomo zinatatuliwa, kutoa elimu zaidi kwa jamii ili kuona elimu ina mchango mkubwa katika maisha ya sasa kwani kuna baadhi yao wanaona mtoto kukaa shule ni kupoteza muda,” amesema.

Hiyo ni kutokana na kushuka kwa thamani ya elimu katika jamii, na ili kukabiliana na suala hilo ni vyema kuhakikisha jamii inashirikishwa kikamilifu.

Dk Mohammed amesema mtihani wa kidato cha nne ni muhimu kwani hupima umahiri wa watahiniwa katika yale yote waliyojifunza kidato cha kwanza hadi kidato cha nne.

Matokeo ya mtihani huo pia hutumika katika uchaguzi wa watahiniwa wanaojiunga na kidato cha tano pamoja na fani mbalimbali za utaalamu wa kazi kama afya, kilimo, ufundi.

“Hivyo, mtihani huu ni muhimu kwa wanafunzi, wazazi, jamii nzima na taifa kwa ujumla. Maandalizi yote kwa ajili ya kuendesha mtihani wa kidato cha nne yamekamilika, ikiwa ni pamoja na kusambazwa kwa mtihani, vijitabu vya kujibia na nyaraka zote muhimu zinazohusu mtihani katika Halmashauri/Manispaa zote Tanzania Bara na Zanzibar,” amesema.

Maandalizi hayo yalienda sambamba na yale ya wenye mahitaji maalumu, huku akiweka bayana kuwa kamati za mitihani za mikoa na halmashauri zimefanya maandalizi yote muhimu, ikiwa ni pamoja na kutoa semina kwa wasimamizi wa mtihani na kuhakikisha mazingira ya vituo vya mtihani ni salama.

“Pia kamati za mitihani zimeweka mikakati ya kuzuia mianya yote inayoweza kusababisha kutokea kwa udanganyifu. Pamoja na maandalizi yote muhimu yaliyofanyika, kamati za mitihani za mikoa na halmashauri zihakikishe kuwa usalama wa vituo vya mtihani unaimarishwa na kwamba vituo hivyo vinatumika kwa kuzingatia mwongozo uliotolewa na Baraza la Mitihani la Taifa.

 “Wasimamizi wahakikishe watahiniwa wote wanafanya mtihani kwa muda uliopangwa na katika hali ya utulivu. Kwa watahiniwa wenye mahitaji maalumu, wasimamizi wahakikishe wanapata haki zao za msingi,” amesema.

Haki hizo ni pamoja na kuwapa mitihani yenye maandishi ya nukta nundu kwa watahiniwa wasioona na maandishi yaliyokuzwa kwa watahiniwa wenye uoni hafifu. watahiniwa wote wenye mahitaji maalumu waongezewe muda wa dakika 20 kwa kila saa, kwa somo la hisabati waongezewe dakika 10 kwa kila saa kwa masomo mengine, kama mwongozo wa baraza unavyoelekeza.