Changamoto ya kisheria kwa watu wenye jinsi tata

Dar es Salaam. Wakati kukiwa na ongezeko la watu wenye jinsi tata au ulemavu wa via vya uzazi nchini, unyanyapaa na gharama kubwa za matibabu vimetajwa kuwa miongoni mwa changamoto zinazowakabili watu wa jamii hiyo.

Kutokana na hayo, kundi hilo limeiomba Serikali kutoa msaada kwao na elimu kwa jamii ili kupunguza mifumo ya kibaguzi na kuimarisha upatikanaji wa huduma zinazowahusu.

Akizungumza na Mwananchi Novemba 13, 2025, wakati wa maadhimisho ya Mwezi wa Watu Waliyozaliwa na Jinsi Tata Duniani, Mkurugenzi wa Taasisi ya Tanzania Voice of Humanity, Baby Musamba, anasema kukosekana kwa sheria za kuwalinda na uelewa wa watu wa jinsi hiyo kunachangia wengi kushindwa kujitokeza. Maadhimisho hayo hufanyika kati ya Oktoba 26 na Novemba 8 ya kila mwaka.

“Wakati mwingine mtu anatengwa kutokana na mwonekano wake. Pia, hakuna kifungu cha sheria ambacho kinawasemea mbele ya mamlaka husika kulingana na mahitaji yao ya kielimu, afya pamoja na sheria zinazolinda utu wao,” anasema Baby, ambaye ni kati ya wanaopitia hali hiyo.

Mtendaji Mkuu wa taasisi hiyo, Frank Musamba, anasema kwa takribani miaka mitano tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo mwaka 2021, wamewafikia watu wa jamii hiyo 63 ambao wamefanyiwa vipimo vilivyothibitisha kuwa na ulemavu katika via vyao vya uzazi. Miongoni mwa hao, idadi kubwa wanatoka mikoa ya Mbeya, Kagera, Kigoma na Dar es Salaam.

Takwimu zilizotolewa na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MHN) zinaonesha mpaka mwaka 2025, imetoa matibabu kwa watu wenye jinsi tata zaidi ya 100, huku asilimia 70 wakiwa watoto na asilimia 30 watu wazima.

Daktari bobezi wa upasuaji wa watoto katika hospitali hiyo, Zaitun Bokhari, anasema wanaona wagonjwa kuanzia mwaka 0 hadi zaidi ya miaka 18, na matibabu huanza baada ya miezi sita.

“Muhimbili tunapata watoto wenye changamoto hizi. Kliniki za matatizo ya homoni na vichochezi wakiwapata wakawafanyia vipimo wanawaleta kwetu,” anasema.

Dk Bokhari anasema baada ya kubaini kuwapo kwa ongezeko mwaka 2018, walitengeneza kamati maalumu chini ya aliyekuwa Mkurugenzi wa Hospitali hiyo, Profesa Lawrence Museru, na kuanza rasmi kurekodi takwimu.

“Ndani ya kamati tupo madaktari bingwa wa upasuaji watoto, kina mama na mfumo wa uzazi, mfumo wa mkojo kwa wanaume, wa vichochezi, magonjwa ya akili na wanasheria. Mpaka sasa tumerekodi zaidi ya wagonjwa 100,” anasema.

Anasema kati ya hao, wapo waliopatiwa tiba zikiwamo za upasuaji, vichochezi peke yake na wengine kupatiwa ushauri wa kitaalamu. Anataja changamoto kubwa ni gharama za matibabu na wengi hawana uwezo.

“Vipimo ni gharama. Ili kubaini huyu wa kike au wa kiume, kuna mlolongo wa vipimo, vingine vinapimwa nje ya hospitali, ikihusisha hata kipimo cha Mkemia Mkuu wa Serikali,” anasema na kuongeza:

“Kipimo cha Mkemia Mkuu kujua chromosomes XX na XY ni zaidi ya Sh200,000, huku laparascopic ikiwa jumla si chini ya Sh800,000 hadi Sh1 milioni, na hapo bado matibabu.”

Anasema takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinakadiria kati ya watoto 4,500 wanaozaliwa mmoja kuwa na tatizo hilo. Kwa Tanzania, kati ya vizazi hai milioni mbili kila mwaka, inaaminika kuna watoto 500 huzaliwa na changamoto hiyo.

Dk Bokhari anasema watu wazima wanaojitokeza wengi huwa na umri mkubwa na hufika wakiwa wamelelewa kama watoto wa kiume ilhali ndani wana mji wa uzazi na mayai na wengine wamelelewa kama watoto wa kike lakini mfumo ukaonyesha unafanya kazi vizuri wakiwa wa kiume.

“Kuna kijana amekuja akiwa na miaka 25, amelelewa kama mtoto wa kiume. Tulifanya vipimo vyote vya hali ya juu, tukashirikisha laparascopy, tukaona ana uterus (mji wa mimba) na mayai yote,” anasema na kuongeza:

“Nje ana kila kitu cha kiume, lakini ndani ana kila kitu cha kike na vinafanya kazi kwani alikuwa akipata hedhi. Bahati mbaya alikataa na alitaka kuendelea kubaki mwanamume.”

Vivyo hivyo, anasema wapo wanaofika wakiwa na maumbile yote mawili, mji wa mimba na korodani moja.

Dk Bokhari anasema bado kuna changamoto kubwa kisheria, hivyo wengi hufanya uamuzi wa jinsi wanayopenda wanapokuwa na umri wa zaidi ya miaka 18.

Anasema wakati wa ujauzito, homoni zina mchango mkubwa katika kuunda jinsi ya mtoto, hitilafu katika uzalishaji au matumizi ya homoni hizo husababisha kuongezeka kupita kiasi kwa homoni za kiume kwa wasichana.

Pia husababisha upungufu wa testosterone kwa wavulana, au Congenital Adrenal Hyperplasia (CAH) moja ya sababu inayoongoza ya watoto wa kike kuzaliwa na jinsia tata.

“Pia chromosomes za mtoto huamua jinsi, wa kike anabeba XX na wa kiume XY. Kukitokea kasoro katika vinasaba vya kutengeneza jinsi, mwanamke hawezi kukamilika,” anasema.

Anasema tatizo huonekana mtoto anapozaliwa akiwa na maumbile ya uzazi yasiyoeleweka moja kwa moja kama ya kiume au ya kike, au akiwa na kasoro fulani kama uume mdogo kupita kawaida, tundu la mkojo kuwa mahali pasipo kawaida, au via vya uzazi viwili kwa pamoja sehemu za siri.

Kwa upande wake, daktari bingwa wa fiziolojia ya homoni na mazoezi kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), Fredrick Mashili, anasema kuna vitu vinaweza kutokea, mbegu za mtoto wa kiume zikaleta wa kike na za kike zikaleta jinsi ya kiume, au mtoto akazaliwa na jinsi mbili.

“Ni somo refu kwa mfano mtu ambaye alikuwa na XY halafu kwa sababu fulani hii Y haikuwa imefanyika vizuri na mwanzoni X iliendelea sasa mambo yanatokea huko Y ilitengeneza sehemu za kiume na huyu mtoto atakuwa na uwezekano wa kuwa na sehemu za kike au sifa za kike hasa sauti, tabia, mienendo ambavyo husababishwa na homoni,” anasema.