KIKOSI cha Azam FC kinatarajiwa kuondoka nchini keshokutwa Jumatano kwenda DR Congo kuiwahi mechi ya kwanza ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya AS Maniema Union, huku kocha wa timu hiyo ya Chamazi, Florent Ibenge akitambia maandalizi waliyofanya.
Mechi hiyo itapigwa Jumapili kwenye Uwanja wa Stade des Martyrs, Kinshasa DR Congo, huku timu nyingine za Kundi B zikiwa ni Wydad Casablanca ya Morocco na Nairobi United ya Kenya inayoshiriki kwa mara ya kwanza michuano ya CAF katika historia ya klabu hiyo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ibenge amesema hadi sasa maandalizi yanaenda vizuri na morali ya wachezaji wa kikosi hicho ni kubwa, licha ya baadhi ya nyota wa timu hiyo kuwa ni majeruhi, lakini jopo la madaktari linaendelea kuhakikisha wanakuwa fiti.
“Licha ya kuwafahamu vizuri wapinzani wetu, siwezi kusema itakuwa mechi nyepesi kwetu, hatua tuliyofikia ni ngumu zaidi na kila mpinzani amejipanga, sisi ni lazima twende kwa tahadhari hususani ukiangalia tunaanzia ugenini,” amesema Ibenge.
Kwa upande wa Daktari wa Azam, Mbaruku Mlinga, amesema nyota wawili wa kikosi hicho, Adolf Mtasingwa na Cheickna Diakite tayari wameanza mazoezi na timu hiyo, japo suala la wao kucheza katika pambano hilo litabakia kwa benchi lao la ufundi.
“Feisal Salum ‘Fei Toto’ aliumia goti huku Yahya Zayd akipata majeraha eneo la ugoko, lakini hali zao zinaendelea kuimarika. Ila hadi sasa suala la kucheza mechi hiyo bado ni mapema kulizungumzia,” amesema Mlinga.
Azam iliyofika hatua ya makundi ya michuano ya CAF kwa mara ya kwanza, ilianza kwa kuitoa EL Merriekh Bentiu ya Sudan Kusini kwa jumla ya mabao 4-0, kisha raundi ya pili kuwatoa mabaharia wa KMKM ya visiwani Zanzibar kwa jumla ya mabao 9-0.
Kwa upande wa Maniema, iliitoa Pamplemousses ya Mauritius kwa jumla ya mabao 4-3, kisha hatua iliyofuata ikaitoa Royal Leopards ya Eswatini kwa penalti 4-3, baada ya mechi baina ya miamba hiyo kuisha kwa sare ya kufungana jumla ya mabao 2-2.