UONGOZI wa Singida Black Stars umesema nyota wawili wa timu hiyo, Ayoub Lyanga na Eliuter Mpepo, bado wana mikataba ya kuendelea kukitumikia kikosi hicho msimu huu, licha ya kudaiwa kutokuwa kwenye mipango ya timu hiyo na huenda wakaachwa.
Ofisa Habari na Mawasiliano wa Singida, Hussein Massanza, aliliambia Mwanaspoti nyota hao wote wawili bado wana mikataba ya kuendelea kukitumikia kikosi hicho, japo taarifa zinaeleza katika dirisha dogo huenda wakafunguliwa mlango wa kutokea.
Taarifa zinaeleza, Singida ilikuwa na mpango wa kuwatoa Lyanga na Mpepo kwa mkopo katika dirisha kubwa lililopita, japo uhamisho wao haukukamilika kutokana na baadhi ya timu nyingi za Ligi Kuu Bara kutofikia mahitaji binafsi yaliyohitajika.
Mpepo aliyetamba na timu mbalimbali ikiwamo Mtibwa Sugar, alijiunga na Singida dirisha dogo la Januari 2025, akitokea Trident ya Zambia, ambako hadi sasa amekosa nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza, kutokana na ushindani mkubwa uliopo.
Mshambuliaji huyo aliyecheza pia Tanzania Prisons, Singida United na Mbeya Kwanza zote za Tanzania, Buildcon ya Zambia, Cape Umoya United ya Afrika Kusini na Interclube ya Angola, alijiunga na timu hiyo kwa mkataba wa mwaka mmoja na nusu.
Uwepo wa washambuliaji, Mkenya Elvis Rupia, Mkongomani Malanga Horso Mwaku aliyesajiliwa msimu huu akitokea FC Lupopo na Andrew Phiri aliyetokea Maestro United ya kwao Zambia, umemfanya nyota huyo kushindwa kuingia katika kikosi cha kwanza.
Kwa upande wa Lyanga aliyejiunga na timu hiyo Julai 9, 2024, akitokea Azam, amekuwa na kipindi kigumu cha kupata namba, tangu ujio wa winga, Mgambia Lamine Jarjou, aliyetua msimu huu akitokea Grenoble Foot 38 ya Ufaransa.