Maniche afichua siri ya Mnigeria Mtibwa Sugar

KOCHA Msaidizi wa Mtibwa Sugar, Awadh Juma ‘Maniche’, amesema beki wa timu hiyo, Mnigeria Victor Chukwuemeka Collins, ameanza taratibu katika kikosi hicho kwa sababu kuu mbili, ambapo ya kwanza ni ugeni wake na ya pili ni kutozoea Ligi.

Akizungumza na Mwanaspoti, Maniche amesema beki huyo wa kati anahitaji muda zaidi wa kuzoeana na wachezaji wenzake ndani ya kikosi hicho, japo kadri anavyozidi kucheza mara kwa mara anatengeneza hali ya kujiamini jambo ambalo ni zuri kwake.

“Ndio kwanza anacheza Ligi ya Tanzania na sio kila mchezaji anaweza kuingia katika kikosi cha kwanza moja kwa moja, ni suala la muda kwake kwa sababu hata hizo dakika chache anazopata unaona kuna kitu anaongeza kikosini,” amesema.

Maniche amesema katika kipindi hiki ambacho Ligi Kuu imesimama, ndicho atakitumia kutoa nafasi ya kutengeneza muunganiko kwa baadhi ya nyota mbalimbali wa kikosi hicho ambao hawajacheza muda mrefu, kupitia mechi za kirafiki watakazozicheza.

Collins aliyezaliwa Novemba 2, 2024, amejiunga na Mtibwa kwa mkopo akitokea Singida Black Stars aliyojiunga nayo msimu huu kwa mkataba wa miaka miwili akitoka Nasarawa United ya Nigeria.

Ameungana na beki wa kushoto, Mghana Ibrahim Imoro.

Beki huyo wa kati aliyecheza Nasarawa United na Remo Stars za kwao Nigeria, ameichezea pia Amanat Baghdad SC ya Iraq, ambapo alisajiliwa Singida kama mbadala wa Mghana Frank Assinki aliyejiunga na Yanga, japo alipelekwa Mtibwa kwa mkopo.

Katika mechi tano za Ligi Kuu ambazo Mtibwa imecheza msimu huu hadi sasa, beki huyo ameanza moja tu dhidi ya Dodoma Jiji iliyoisha kwa suluhu (0-0), Oktoba 22, 2025, iliyopigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, huku akicheza kwa dakika 60.