Ushirikiano wa Tanzania na Comoro wazidi kuimarika, rushwa yalengwa

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Crispin Chalamila amesema Tanzania na Comoro zimeendelea kuimarisha uhusiano wao katika maeneo ya kikanda, kijamii na kiusalama, hatua inayochochea kasi ya maendeleo baina ya mataifa hayo.

Chalamila ameeleza hayo leo Jumatatu Novemba 17, 2025 jijini Dar es Salaam wakati akimkaribisha Rais wa Taasisi ya Kupambana na Rushwa ya Comoro ya Chambre Anti-Corruption, Fahamoue Youssouf aliyetembelea mamlaka hiyo kwa ajili ya ziara ya kikazi.

Amesema uhusiano wa Tanzania na Comoro umejengwa juu ya misingi ya kuheshimiana, tamaduni zinazofanana na dhamira ya pamoja ya kukabiliana na changamoto za kikanda.

“Ushirikiano umekuwa ukifanyika kupitia bodi ya ushirikiano wa kikanda, kupitia bodi ya ushauri ya Umoja wa Afrika dhidi ya Rushwa (AUABC) pamoja na Shirikisho la Eastern and Southern African Money Laundering Group.

“Tunashirikiana katika kubadilishana uzoefu kuhusu hatua za kudhibiti rushwa na mbinu za utendaji na mikakati ya kuelimisha umma kuichukia rushwa, pia kuimarisha mifumo ya kitaifa ya uadilifu, nyenzo za kutathmini vihatarishi vya uwepo wa rushwa na utekelezaji wa mapendekezo yanayotolewa na wadau ili kuziba mianya ya rushwa,” amesema.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Crispin Chalamila akimkaribisha Rais wa Takukuru Comoro,Fahamoue Youssouf (kushoto) alipowasili katika ofisi za TAKUKURU jijini Dar es Salaam,kwaajili ya mkutano.Picha na Michael Matemanga

Chalamila amesema hatua hiyo imechangia kuimarisha mifumo ya uadilifu na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa mapendekezo ya wadau na kuleta uwajibikaji.

Ameeleza kuwa, ushirikiano katika usalama umeendelea kuimarika, hususan kwenye masuala ya ulinzi wa mipaka na baharini.

“Tanzania, kwa kutumia miundombinu yake ya usafiri na bandari, imekuwa msaada muhimu kwa Comoro katika kuchochea biashara na muunganiko wa kiuchumi. Aidha, juhudi za pamoja katika usimamizi wa Bahari ya Hindi zimeongeza uwezo wa mataifa hayo kukabili changamoto za kiusalama,” amesema.

Katika sekta ya elimu, Chalamila amesema kumekuwa na programu za kubadilishana uzoefu kwa watumishi wa umma, ushirikiano kati ya taasisi za elimu ya juu pamoja na ufadhili wa masomo, hatua inayolenga kuongeza ujuzi na kukuza uongozi katika taasisi za Serikali.

Aidha, ameeleza mataifa hayo mawili yanaendelea kushirikiana katika masuala ya afya na maendeleo ya jamii, ikiwamo juhudi za pamoja za kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza na kuimarisha huduma za kijamii.

Kutokana na ushirikiano huo, Chalamila amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan, akisema ameendelea kuwa nguzo muhimu katika kuimarisha uhusiano wa Tanzania na Comoro.

 Rais wa taasisi  hiyo, Fahamoue amesema ujio wao nchini unaonesha uwazi uliopo baina ya taasisi za nchi hizo mbili katika kubadilishana uzoefu katika kudhibiti rushwa.

“Mkutano huu utafungua njia ya kuendeleza uhusiano wetu kupitia programu za mafunzo, kubadilishana uzoefu au kuanzishwa kwa mfumo rasmi wa ushirikiano baina ya pande mbili,” amesema Fahamoue.

Julai mwaka huu, Rais Samia akiwa mgeni rasmi katika sherehe za miaka 50 ya Uhuru wa Comoro zilizofanyika katika Uwanja wa Malouzini jijini Moroni, alisema Tanzania iko tayari kushirikiana na visiwa vya Comoro kukabili changamoto ikiwamo mabadiliko ya tabianchi, afya na usafirishaji.

“Comoro ni kisiwa ila Tanzania ni nchi yenye visiwa vidogo, hivyo mabadiliko ya tabianchi yanatukabili wote. Mabadiliko haya yamechangia kuongezeka kwa nyuzijoto na kuongezeka kwa maji ya chumvi ambayo yamekuwa yakila ardhi na kupoteza viumbe wa baharini. Tanzania iko tayari kushirikiana na Comoro ili kulinda ikolojia zetu kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo,” alisema.