Nactvet yahamasisha waliokosa vyuo kuomba tena

Dodoma. Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Nactvet) limewataka wanafunzi waliokosa sifa za kujiunga na vyuo kwa mwaka wa masomo 2025/2026, kuomba tena kulingana na kozi zenye sifa zao kabla dirisha la udahili halijafungwa, ifikapo Desemba 12, 2025.

Wito huo umetolewa kufuatia asilimia mbili ya wanafunzi walioomba kujiunga na vyuo vya kati kushindwa kusajiliwa na Nactvet kutokana na kukosa sifa za kujiunga na kozi walizoomba.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 17, 2025, Katibu Mtendaji wa Nactvet, Dk Mwajuma Lingwanda amesema majina ya wanafunzi walioomba kusajiliwa kupitia vyuo vinavyosajili wanafunzi moja kwa moja kwa vyuo visivyo vya afya kwa mwaka wa masomo 2025/2026 ni 108,109.

Hata hivyo, amesema waliosajiliwa na Nactvet ni 106,022 ambao ni sawa na asilimia 98 ya walioomba huku wengine 2,087, sawa na asilimia mbili wakikosa sifa za kujiunga na vyuo hivyo.

Dk Lingwanda amewataka wanafunzi waliokosa sifa za kusajiliwa kuomba nafasi upya kwenye vyuo ambavyo wana sifa za kusoma kabla dirisha la usajili halijafungwa.

“Kuna wanafunzi waliiomba kusoma kwenye kozi ambazo hawana sifa za kusomea kwa mfano mtu anaomba kusomea uhandisi lakini hajasomea masomo hayo, hao walikosa sifa za kujiunga na vyuo walivyoomba.

“Lakini wanaweza kuomba tena kwenye vyuo ambavyo masomo waliyosoma yanawaruhusu kusoma kozi hizo wafanye hivyo kabla dirisha la usajili halijafungwa,” amesema Dk Lingwanda.

Ametoa onyo kwa vyuo ambavyo vinapokea wanafunzi ambao hawana sifa ya kusomea kozi zinazotolewa kwenye vyuo vyao, na kusema kuwa watakaobainika kufanya hivyo watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Amesema wanafunzi walioomba kusomea kozi za afya na sayansi shirikishi walikuwa 49,148 lakini waliochaguliwa walikuwa ni 30,553 sawa na asilimia 80 ya wanafunzi wote walioomba, ambapo wasichana ni 20,131 sawa na asilimia 51 na wavulana ni 19,422 sawa na asilimia 49.

Aidha, Katibu Mtendaji huyo ametoa wito kwa vyuo vyote vya kati nchini kuwasajili wanafunzi wote waliojiunga na vyuo vyao kabla ya Desemba 12, 2025, na kuwataka wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na vyuo kuhakiki usajili wao kupitia Nactvet kabla hawajaanza masomo ili kuepusha usumbufu utakaojitokeza baadaye kwa kutokusajiliwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Udahili, Utahini na Utunuku kutoka Nactvet, Dk Marcelina Baitilwake amesema yapo makosa ambayo yamekuwa yakifanyika wakati wa usaili wa wanafunzi hasa ambao wanasajiliwa na vyuo, ambayo husababisha wanafunzi kukosa sifa za kuendelea na masomo ikiwemo vyuo kuomba usajili kwa niaba ya wanafunzi.

Amesema anayetakiwa kuomba usajili ni mwanafunzi lakini kuna baadhi ya vyuo ambavyo huomba usajili bila ridhaa ya wanafunzi na matokeo yake mwanafunzi anakuwa amesajiliwa kwenye kozi ambayo hataki kuisoma, na kushindwa kusomea kile anachokipenda kutokana na vyuo kuwasajili bila ridhaa zao.

Mbali na hilo amewataka wanafunzi wote wa mwaka wa kwanza kuwasili vyuoni kuanzia leo Novemba 17, 2025 kwa ajili ya kuanza mwaka wa masomo hasa kwa wale wa mwaka wa kwanza, na kwa wale waliokuwa wanaendelea na masomo waripoti vyuoni kuanzia Novemba 24, 2025.