Unguja. Chama cha ACT- Wazalendo kimefungua mashauri 25 Mahakama Kuu kupinga matokeo ya uchaguzi wa uwakilishi Zanzibar huku kikisisitiza sio kipaumbele chake kuingia au kutokuingia ndani ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).
Kesi hizo zinahusisha majimbo ya uchaguzi 25 kati ya 50 yaliyopo Unguja na Pemba.
Uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025, chama hicho kilishinda majimbo 10 na Chama cha Mapinduzi (CCM) kikishinda majimbo 40 kati ya 50 yaliyopo Zanzibar.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu, Novemba 17, 2025 makao makuu ya chama hicho, Vuga Unguja Zanzibar, Mwanasheria Mkuu wa ACT- Wazalendo, Omar Said Shaaban amesema kati ya hizo, Pemba ni kesi nane na Unguja kesi 17.
“Tumechukua hatua hii tukiongozwa na imani kubwa kuwa, wagombea wetu katika majimbo ambayo tumefungua mashauri na yale tutakayofungua, wameporwa ushindi wao kumekuwa na ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi,” amesema Shaaban.
Hata hivyo, Shaaban amesema kwa upande wa mashauri yanayohusu wabunge bado hawajafungua na wanaendelea na mchakato wa kukamilisha hatua hizo, kwa kuwa hata kanuni za Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) inatoa fursa ya siku 30 kufungua kesi zinazohusiana na uchaguzi tangu uchaguzi unapokamilika.
Kwa upande wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), kanuni za kesi za uchaguzi zinatakiwa kufunguliwa ndani ya siku saba tangu kumalizika kwa uchaguzi.
Ametaja baadhi ya majimbo ambayo wameyafungulia kesi ni Malindi, Amani, Nungwi, Kijini, Bumbwini, Chaani, Mpendae, Kiembesamaki na Mwanakwerekwe.
Mengine ni Makunduchi, Pangawe, Chumbuni, Tumbatu, Mwera, Mtoni, Welezo na Mkwajuni.
Amesema baada ya kuwasilisha mahakamani, Mahakama kupitia amri ya Naibu Mrajisi, Novemba 10, 2025, walitoa maelekezo kuambatanisha matokeo halisi ya kila jimbo la uchaguzi na ambayo tayari waliwasilisha matokeo hayo.
Hata hivyo, kwa upande wa Pemba amesema tangu wafikishe mashauri hayo Novemba 4, 2025 bado yapo katika ofisi ya Naibu Mrajisi.
Kwa mujibu wa mwanasheria mkuu wa chama hicho, kesi zote za uwakilishi, waliokuwa wagombea wameshalipa ada za Mahakama ikiwamo malipo ya dhamana ya Sh2 milioni kwa kila kesi.
“Kwa upande wa ubunge chama kitaanza kuwasilisha mashauri ndani ya wiki hii, tulianza kuwasilisha mashauri ya uwakilishi kwa sababu kanuni zinatutaka kufanya hivyo ndani ya siku saba lakini kwa ubunge kanuni zinasema ndani siku, hivyo bado tupo ndani ya muda,” amesema.
Shaaban amesema wameshafanya uchambuzi wa majimbo yatakayofunguliwa mashauri na watatoa taarifa kamili baada ya kufunguliwa.
Katika hatua nyingine, Shaaban amesema kupitia Bodi ya Wadhamini ya chama hicho, wamefungua maombi ya madai namba 28632 ya mwaka 2025 dhidi ya INEC na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa Tanzania wakiomba kibali cha Mahakama kwa ajili ya kufungua shauri la mapitio ya kimahakama.
Shauri hilo linaiomba Mahakama kuitaka INEC kufuta uamuzi wake wa namna walivyofanya mgao wa viti maalumu na kuiomba tume ifuate utaratibu uliowekwa na sheria.
Amesema shauri hilo limepangwa kutajwa kwa mara ya kwanza Novemba 19, 2025 mbele ya Jaji Kisanya.
“Tumefungua shauri hili tukiamini kuwa, tume imekiuka kanuni na utaratibu wa namna ya kugawa viti maalumu. Tumekusanya taarifa za kutosha kuhusu idadi ya kura halali za wabunge ambazo chama kimepata nchi nzima, hivyo tukiamini kuwa tunayo haki ya kupata viti hivyo,” amesema.
Akizungumza kuhusu msimamo wao chama kuinga Serikali ya Umoja wa Kitaifa, Shaaban amesema kama ambavyo mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Othman Masoud Othman kwa nyakati tofauti akieleza kwamba wakati huu sio kipaumbele cha chama hicho, kuingia au kutokuingia ndani ya SUK.
“Bado msimamo wa chama ni uleule, kuingia au kutokuingia sio kipaumbele chetu kwa sasa kuna mambo makubwa ya kuangaikia nchi yetu na kupata ufumbuzi wake. Na kama haitoshi kuna haja gani ya kukimbilia jambo kwa wiki mbili ambalo Katiba imekupa miezi mitatu kufanya uamuazi,” amehoji Shaaban.
Hivi karibu wakati Rais wa Zanzibar Hussein Ali Mwinyi akiwaapisha mawaziri Ikulu Zanzibar, aliwasihi viongozi wa chama hicho kuingia ndani ya SUK kwa masilahi ya wananchi na Taifa kwa jumla.
