Dar es Salaam. Kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili, Mkurugenzi wa Kampuni ya Vanilla International Ltd, Simon Mkondya (40), maarufu Dk Manguruwe, imekwama kuendelea kutokana na Jamhuri kutokamilisha kupandisha nyaraka mtandaoni.
Mkondya na mwenzake, Rweyemamu John (59), ambaye ni Mkaguzi wa fedha wa kampuni hiyo, wanakabiliwa na mashtaka 28 yakiweno ya kuendesha biashara ya upatu na utakatishaji fedha linalomkabili Mkondya pekee yake.
Kwa upande wa mashtaka wa pili ambaye ni John, yupo nje kwa dhamana baada ya kwenda kuomba dhamana Mahakama Kuu na pia hana mashtaka ya kutakatisha fedha.
Wakili wa Serikali, Titus Aron, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo Novemba 17, 2025 wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kusomwa hoja za awali (PH).
Aron ametoa taarifa hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki, anayesikiliza kesi hiyo.
“Kesi imeitwa kwa ajili ya washtakiwa wote kusomewa hoja za awali na usikilizwaji, lakini kwa bahati mbaya Jamhuri bado hatujakamilisha kupandisha nyaraka zote kwenye mtandao wa Mahakama, hivyo tunaomba tupangiwe tarehe fupi kwa ajili ya kuwasomea hoja za awali” amesema Titus.
Hakimu Nyaki amesema kesi hiyo imepangwa kusikiliza mfululizo na itaendelea kesho mchana, Novemba 18, 2025.
Kwa mara ya kwanza washtakiwa hao walifikishwa Mahakamani hapo Novemba 5, 2024 na kusomewa kesi ya Uhujumu Uchumi namba 31523 ya mwaka 2024.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, kati ya mashtaka hayo 28; mashtaka 19 ni ya kuendesha biashara ya upatu na mashtaka tisa ni ya kutakatisha viwanja.
Katika moja ya mashtaka hayo kuendesha biashara ya upatu, washtakiwa wanadaiwa kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba Mosi,2023, jijini Dar es Salaam, walitenda makosa hayo.
Inadaiwa kuwa Mkondya akiwa kama Mkurugenzi wa kampuni hiyo na John akiwa mkaguzi wake waliendesha biashara ya upatu kwa kuwaahidi watu watapata pesa mara mbili hadi tatu kama faida zaidi ya waliyotoa.
Washtakiwa hao wanadaiwa kujipatia kiasi cha Sh92.2 milioni kutoka kwa watu 19 tofauti ambao walitoa kiasi tofauti cha fedha kwa kuwaahidi kuwa watapata faida mara mbili hadi tatu ya fedha walizotoa.
Katika mashtaka 9 ambayo ni ya utakatishaji fedha yanayomkabili Mkondya peke yake, inadaiwa kuwa kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba Mosi, 2023 akiwa katika mkoa wa Dar es salaam na akiwa kama Mkurugenzi wa Kampuni hiyo alijipatia jumla ya viwanja tisa vilivyopo katika kitalu namba AB eneo la Idunda mkoani Njombe.
Pia, Mkondya anadaiwa kujipatia viwanja hivyo huku akijua viwanja hivyo ni mazalia ya makosa tangulizi ya kuendesha biashara ya upatu.
