Mitazamo tofauti adhabu ya viboko bajaji, bodaboda wanaovunja sheria

Dar es Salaam. Kitendo cha baadhi ya askari wa usalama barabarani (trafiki) jijini Dar es Salaam kutumia fimbo kuwaadhibu madereva wa bajaji na bodaboda wanaokiuka sheria, ikiwamo kuingia kwenye barabara maalumu za Mabasi Yaendayo Kasi (BRT), kimezua mjadala miongoni mwa wananchi.

Madereva wa bajaji na bodaboda wamedaiwa kukiuka Sheria ya Usalama Barabarani (Road Traffic Act, Cap 168) na kanuni zake zinawapa polisi mamlaka ya kutoa maagizo, kusimamisha magari, au kuweka vizuizi katika maeneo fulani ya barabara ili kudhibiti matumizi na kuhakikisha usalama.

Hata hivyo, sheria hizo hazitoi mamlaka ya kutumia adhabu ya viboko kama njia ya kuwaadhibu wanaokiuka sheria.

Akizungumzia matumizi ya barabara za BRT, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), Said Tunda, ameiambia Mwananchi kwamba barabara hizo ni maalumu kwa matumizi ya mabasi ya mwendokasi pekee.

Tunda ameongeza kuwa magari maalumu, kama ya wagonjwa, zimamoto, na ya jeshi, huruhusiwa kupita humo kwa kibali maalumu.

Amesema, hata hivyo, bado kumekuwapo baadhi ya vyombo vingine vya moto vinavyokiuka sheria na kutumia njia hizo kwa lengo la kukwepa foleni.

“Wale wanaokamatwa hukutana na adhabu ikiwamo polisi kuwashikilia, kuwalazimisha ‘kulala mahabusu,’ na wengine kutozwa faini hadi Sh. 300,000,” amesema.

Mbali na adhabu hizo, baadhi ya trafiki wamekuja na utaratibu wa kutoa adhabu za papo kwa hapo kwa kuwachapa viboko madereva hususan wa bajaji na bodaboda, sanjari na abiria wao wanapopita kwenye barabara hizo.

Adhabu hiyo imeibua mjadala, wapo wanaoiona kama njia sahihi na rahisi ya kuwalazimisha madereva hao kutii sheria, huku wengine wakiiona kama uvunjaji wa haki na kutweza utu wa madereva hao na abiria wao.

Japo kwa sasa hakuna sheria maalumu ya kupita kwenye barabara za mwendokasi, ikielezwa inayotumia ni sheria ya kawaida ya trafiki.

Akifafanua suala hilo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra), Habibu Suluo, amesema kwamba njia za mwendokasi bado hazijawekewa sheria maalumu zinazozisimamia moja kwa moja.

Suluo amebainisha kuwa, hadi sasa, kanuni na hatua zinazotekelezwa zinategemea masharti ya sheria za usalama barabarani (trafiki), ambazo ndizo zinaongoza matumizi ya barabara hizo kwa muda.

“Ingawa mchakato wake unaendelea, tunachopaswa kukifahamu ni kwamba hizo ni njia maalumu kwa ajili ya mabasi ya mwendokasi pekee,” amesema.

Licha ya baadhi ya watu kuhoji hatua ya baadhi ya trafiki kutoa adhabu ya viboko, ofisa mwandamizi wa kitengo cha usalama barabarani aliyeomba jina lake lihifadhiwe, ameliambia Mwananchi kwamba wanapowakamata na kutoza faini madereva wa vyombo vya moto wanaopita kwenye barabara ya mwendokasi, wanatekeleza sehemu ya majukumu yao kwa mujibu wa sheria.

Alipoulizwa sababu ya kutumia viboko na kwa nini waliamua kubuni mbinu hiyo, amesema hakuna sheria ya kutoa adhabu ya viboko.

 “Trafiki wanaofanya hivyo ni wao wenyewe tu wameamua, lakini hakuna adhabu za viboko, wala trafiki hatakiwi kutoa adhabu hiyo,” amesema.

Mmoja wa trafiki katika wilaya ya Ubungo alipoulizwa sababu za kutumia viboko, amesema madereva wa bodaboda na bajaji bila kutumia njia hiyo ni wasumbufu na wengi wao hawazingatii sheria za barabarani.

“Hawa ndiyo wanaoongoza kupita kwenye mwendokasi, wakigongwa wanakuwa kama wanaonewa. Wakati wanapoona trafiki mbele, wanafanya vitu vya kuhatarisha maisha yao na ya watumiaji wengine wa barabara,” amesema.

Japo amedai yeye hajawahi kutoa adhabu hiyo, wapo trafiki wanaona kuzungumza na kuwakamata au kuwapeleka mahabusu, au kuwatoza faini haitoshi, maana wanalipa na kisha kurudia makosa yale yale, hivyo bora watumie viboko ili wakihisi maumivu wasirudie.

Si dereva pekee, hata abiria aliyenaye hujikuta kwenye adhabu hiyo ya viboko mara nyingi huchapwa mikononi au mgongoni kutokana na ‘timing’ ya trafiki na mwendo aliopita nao dereva.

Baadhi ya waliokutana na ‘kipigo’ hicho ni dereva wa bodaboda katika kituo cha Manzese, Nelson Fundikira, anayesimulia namna yeye na abiria wake walikula bakora za mikono na mgongo.

“Kama nisingekuwa makini, huenda tungeanguka. Nilikuwa nampeleka abiria Mbezi, kulikuwa na foleni kubwa, tukiwa Kibo tukaamua kuingia njia ya mwendokasi.

“Tukiwa tunakaribia kituo cha Bucha, tukawaona trafiki, kurudi nyuma hatuwezi, ikabidi niongeze mwendo nipite hivyo hivyo, kumbe walikuwa na fimbo. Wawili walitoa fimbo, mmoja akanichapa mimi, zikanipata mkono wa kulia, na abiria wangu akaambulia za mgongo. Nilikasirika, lakini kwa kuwa mimi ndiye nilikuwa na makosa, sikusimama,” amesema.

Dereva mwingine, Nasyilinga Kalinga, pia amewahi kukutana na adhabu hiyo katika eneo la stesheni ya SGR. “Nilisimama eneo ambalo haliruhusiwi bodaboda, sikuwa nafahamu akili yangu ilikuwa kupata abiria waliokuwa wameshuka na treni ya Dodoma. Nilipigwa fimbo ya mgongo, ile kugeuka nikakuta trafiki, ikabidi niwe mpole,” amesema.

Mmoja wa madereva jijini Dar es Salaam, Agripina Joseph, amesema, “Jamii inahitaji nidhamu ya barabarani, lakini pia nidhamu ya kutumia madaraka, polisi na wananchi wote wanapaswa kuheshimiana katika kukabiliana na changamoto za barabarani.”

Yonas Andrew amesema kuna changamoto za utekelezaji wa sheria za usalama barabarani, madereva, hasa wa bodaboda na bajaji wengi katika jiji la Dar es Salaam, huwa hawafuati sheria.

“Trafiki wanakabiliwa na changamoto sana katika kusimamia sheria za barabarani. Madereva wengi, hasa wale bodaboda na bajaji, hupuuza alama za barabarani na hufanya kosa lilelile mara kadhaa licha ya faini. Binafsi, naona ni sawa wachapwe tu viboko,” amesema.

Haki za binadamu, wanasheria washauri

Akizungumzia hilo, Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), wakili Fulgence Masawe, amesema mtu anapopigwa viboko barabarani bila utaratibu wa kisheria ni uvunjaji wa haki za binadamu.

Amesema kuchapa viboko ni kutweza utu wa binadamu, akibainisha kwamba hakuna mtu anaruhusiwa kumpa mtu adhabu hadi Mahakama iamue, kama watu wamekosa, wakamatwe wapate adhabu kwa mujibu wa sheria. amesema.

Akizungumza kwa muktadha wa sheria, wakili kiongozi wa kampuni ya sheria ya Haki Kwanza, Aloyce Komba, amesema kutumia viboko si sehemu ya taratibu za kisheria za kudhibiti ukiukaji wa sheria za barabarani.

“Polisi wanaweza kukamata, kutoa onyo, au kutoza faini, lakini si kuadhibu papo kwa papo,” amesema.

Amesema kumpiga mtu ni kinyume cha sheria, na huyo aliyepigwa anaweza kumshtaki trafiki aliyechukua hatua hiyo.

“Ni kama vile polisi anamkamata mtuhumiwa halafu anaanza kumpiga, hiyo si sahihi kwani mwenye mamlaka ya kutoa adhabu kwa mujibu wa sheria ni Mahakama na si vinginevyo,” amesema.

Amesema mtu akivunja sheria akamatwe na kupelekwa kunako husika na si kupigwa viboko.