Hili hapa baraza la mawaziri la Samia

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametangaza baraza jipya la mawaziri, likiwa na jumla ya wizara 27, mbili mpya, ikiwemo ya Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana.

Rais Samia ametangaza baraza hilo leo, Jumatatu Novemba 17, 2025 katika mkutano wake na waandishi wa habari, uliofanyika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma. Wataapishwa kesho Jumanne.

Amesema ameona umuhimu wa vijana kuwa na wizara kamili itakayokuwa chini ya ofisi ya Rais.

Kutokana na hilo, amesema amefanya marekebisho kidogo na kuunda Wizara ya Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano.

Amesema atakayeshika nafasi hiyo atakuwa na kazi ya kufanya mazungumzo na makundi mbalimbali kuhakikisha mahusiano mazuri.

Aidha, marekebisho mengine yameshuhudiwa katika Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na sasa imehamishiwa Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete amesalia katika wadhifa aliokuwa nao kabla ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, huku naibu wake ni Regina Kwaray.

Kama ilivyo kwa Kikwete, Profesa Kitila Mkumbo naye, amesalia katika Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, huku naibu wake akiwa ni Pius Chaya.

Mwingine aliyesalia katika wizara aliyoiongoza kabla ni Hamad Masauni akiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira na naibu wake ni Dk Festo Dugange.

Vivyo hivyo kwa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Mbunge wa Isimani, William Lukuvi anasalia katika nafasi hiyo na naibu wake ni Ummy Nderiananga.

Balozi Mahmoud Thabit Kombo naye ameendelea kushika wadhifa wake katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na naibu mawaziri wake ni Dk Ngwaru Maghembe na James Ole-Millya.

Mabadiliko pia hayajashuhudiwa katika Wizara ya Maji, Jumaa Aweso ameendelea na wadhifa wake na naibu wake ni Kundo Mathew.

Wizara mpya ya Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana imepata pia mwanasiasa mpya, Mbunge wa Mtwara Mjini, Joel Nanauka na hatakuwa na naibu waziri.

Kwa upande wa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu na naibu wake ni Rahma Riyadh Kisuo.

Katika Wizara ya Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Profesa Rizik Shemdoe ndiye aliyepewa wadhifa huo na naibu wake ni Reuben Kagilwa kwa upande wa elimu na afya ni Dk Jaffar Rajab Seif.

Balozi mstaafu wa Tanzania nchini China, Khamis Mussa Omar ndiye aliyepewa nafasi ya kumrithi Dk Mwigulu Nchemba katika Wizara ya Fedha na naibu mawaziri wawili ambao ni Laurean Luswetura na Mshamu Ali Munde.

Waziri wa Mambo ya Ndani ni George Simbachawene na naibu wake ni Dennis Londo, huku Wizara ya Kilimo ikishikwa na Daniel Chongolo na naibu wake ni David Silinde.

Kwa upande wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Waziri wake ni Rhimo Nyansaho, huku Wizara ya Ujenzi ikiendelea kuongozwa na Abdallah Ulega na naibu wake ni Geoffrey Kasekenya.

Profesa Makame Mbarawa ataendelea kuwa Waziri wa Uchukuzi na naibu wake ni David Kihenzile, huku Wizara ya Viwanda na Biashara itaongozwa na Judith Kapinga na naibu wake ni Patrobas Katambi.

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ni Angellah Kairuki na naibu wake ni Sweetbert Mkama na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu ni Dk Dorothy Gwajima na naibu wake ni Maryprisca Mahundi.

Waziri wa Afya ni Mohamed Mchengerwa na naibu wake ni  Dk Florence Samizi, huku Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia ni Profesa Adolf Mkenda na naibu wake ni Wanu Khafidh Ameir.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ni Dk Leonard Akwilapo na naibu wake ni Kaspar Muya na Waziri wa Maliasili na Utalii ni Dk Ashatu Kijaji na naibu wake ni Hamad Hassan Chande.

Profesa Palamagamba Kabudi anaendelea kuwa Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo na naibu mawaziri wake ni Hamis Mwinjuma na Paul Makonda.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi ni Dk Bashiru Ally na naibu wake ni Ng’wasi Kamani huku Waziri wa Madini ni Anthon Mavunde na naibu wake ni Dk Steven Kiruswa.

Waziri wa Nishati ni Deogratius Ndejembi naibu wake ni Salome Makamba na Waziri wa Katiba na Sheria ni Juma Homera na naibu wake ni Zainab Katimba.

“Wote tutaapisha kesho asubuhi kama taarifa itakavyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi (Moses Kusiruka),” amesema.