Watunisha misuli wanne watua na medali

WATANZANIA wanne wamerejea nyumbani kibabe baada ya kunyakua medali mbalimbali za mashindano ya Watunisha Misuli (WFF Africa Bodybuilding and Fitness Championship Pro Qualifier 2025) yaliyofanyika siku mbili huko Zambia.

Zambia ilizindua rasmi mashindano hayo ikiwa ni mwaka wa pili mfululizo kwa nchi hiyo kuandaa mashindano haya makubwa ya watunisha misuli Afrika, ambapo George Kajula alibeba medali ya dhahabu, Rashid na Amani Mkondya medali ya Silver huku Jackson Mwailinga akinyakua medali ya shaba.

Akizungumza na Mwanaspoti, kiongozi wa msafara, Edward Mwakasyuka amesema hiyo ni rekodi kwa mara ya kwanza Tanzania kupata ushindi mnono katika mchezo huo.

Mwakasyuka aliongeza ni jambo la kujivunia kama taifa kuona wachezaji wanne kunyakua medali mbalimbali za mashindano hayo makubwa Afrika.

MISU 01

“Hii ni mara ya kwanza kwa Tanzania kupata ushindi mnono wa aina hii kwenye mchezo wa kutunisha misuli, tulikuja na vijana sita lakini wawili hawakufanikiwa kwenda mbali zaidi na tunashukuru wanne wameonyesha uwezo mkubwa na kutunukiwa medali,” amesema Mwakasyuka ambaye ni msimamizi wa kituo cha mazoezi ya afya The Green Fitness Gym Mbeya.

Uzinduzi wa mashindano hayo uliofanyika juzi ulihudhuriwa na Rais wa WFF Duniani, Graeme Lancefied, Rais wa Shirikisho la Kimataifa la Bodybuilding na Fitness (IBFF), Annie Williams kutoka Afrika Kusini.