Apple mbioni kutumia AI ya Google Gemini kuiongezea nguvu Siri

Dar es Salaam. Kama unatumia simu za kampuni ya teknolojia ya Apple ni wazi utakuwa unafahamu akili unde iitwayo Siri iliyojipatia umaarufu kwa kujibu maswali na usaidizi mwingine kwa mtumiaji wa simu hizo, kupitia majibu ya sauti.

Katika kuboresha huduma na kuipa nguvu zaidi Siri kampuni ya Apple sasa ipo mbioni kuanza kutumia akili unde (AI) ya kampuni ya teknolojia ya Google iitwayo Gemini. Hii ni kwa mujibu wa chapisho la Bloomberg na Reuters.

Ikumbukwe Siri ilitolewa kwa mara ya kwanza kama programu kwenye Duka la Programu la Apple (Apple Store) mnamo Februari 2010 lakini Oktoba 2011, Apple ilizindua toleo la beta la Siri na iPhone 4S.

Tovuti ya Bloomberg katika taarifa hiyo imeeleza Apple inaingia makubaliano na Google kutengeneza modeli maalumu ya Gemini AI ili kuendesha toleo lijalo la Siri kuanzia mwaka 2026.

Kulingana na ripoti ya Novemba 2 iliyotolewa na Mark Gurman mwandishi wa Bloomberg.

Apple Inc. inapanga kulipa takriban dola bilioni moja kwa mwaka kwa modeli hiyo yenye nguvu iliyotengenezwa na Google ya Alphabet Inc. ambayo ingesaidia kuendesha ukarabati wake wa muda mrefu wa Siri.

Kufuatia kipindi kirefu cha tathmini, kampuni hizo mbili sasa zinakamilisha makubaliano ambayo yataipa Apple ufikiaji wa teknolojia ya Google, kulingana na watu, ambao waliomba kutotajwa majina yao kwa sababu majadiliano hayo ni ya faragha.

Modeli hiyo itapatikana kwenye seva za Private Cloud Compute za Apple, kuhakikisha data ya mtumiaji haipatikani na Google.

Apple inasemekana kutumia jina la siri “AFM v10” (Apple Foundation Model version 10) kwa mfumo huo wa Gemini ili kuficha ushirikiano huo kutoka kwa umma na wafanyakazi wengine.

kinachofanyika kutakuwa na muungano kati ya Siri na Gemini ikiwa ni sehemu ya ukarabati mkubwa wa kufanya Siri iwe na uwezo zaidi, iweze kushughulikia maswali changamano, kufanya muhtasari wa taarifa.

Katika hilo Gemini inatarajiwa kushughulikia hasa kazi za kufanya muhtasari kwa ajili ya Siri, hasa kwa mahitaji ya AI yanayohitaji modeli kubwa ya lugha (LLM).

Siri mpya, inayoweza kuendeshwa na Gemini, inaripotiwa kuanza kutumika na sasisho (update) la iOS katika msimu wa joto (spring) wa 2026.

Apple inaona hili kama hatua ya kimkakati ya muda mfupi huku ikiendelea kuunda modeli yake ya ndani ya kampuni ya kiwango kikubwa cha AI.

Kwa hivyo, Siri haitabadilishwa, lakini toleo lake lijalo huenda likaendeshwa kwa sehemu na Gemini ya Google.

Taarifa kuhusu ushirikiano huu zimeelezwa na vyanzo vikuu na vyenye sifa katika tasnia ya teknolojia, hasa ripoti za Bloomberg kutoka kwa mwandishi wao anayejulikana sana wa habari za Apple, Mark Gurman, kupitia jarida lake la Power On.