Simba, Yanga zapewa marefa wa kadi nyingi CAF

WIKIENDI hii, Yanga na Simba zinashuka uwanjani katika mechi za kwanza za makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika zote zikiwa nyumbani, huku Shirikisho la Soka Afrika (CAF) likiwaanika waamuzi watakaozichezesha wakiwa na rekodi ya kugawa kadi kama njugu.

Kwa mujibu wa ratiba ilivyo ni kwamba Jumamosi Yanga itaanza kwa kuikaribisha AS FAR Rabat ya Morocco kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar, ikiwa ni mechi ya Kundi B, kisha Jumapili itakuwa zamu ya Simba dhidi ya Petro Atletico ya Angola Kwa Mkapa.

Simba yenyewe imepangwa Kundi D sambamba na Stade Malien ya Mali na Esperance ya Tunisia, wakati Yanga imepangwa pia na Al Ahly ya Misri na JS Kabylie ya Algeria.

Kwa mujibu wa CAF, mechi zote za watani zitapigwa kuanzia saa 10:00 jioni, huku ile ya Yanga itachezeshwa na mwamuzi wa kati, Ahmad Imtehaz Heeralall, raia wa Mauritius.

Mwamuzi huyo ana rekodi ya kuzichezesha timu kutoka Tanzania mara tatu katika michuano ya CAF ambapo Yanga ni mbili na Simba moja. Pia aliichezesha timu ya taifa ya Tanzania katika kufuzu Afcon iliposhinda bao 1-0 dhidi ya Uganda, Machi 24, 2023 kupitia bao la Simon Msuva.

Katika mechi za klabu, alianza na Yanga Julai 29, 2018 makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, ikipigwa kwenye Uwanja wa Mkapa ambapo wenyeji walilala 3-2 mbele ya Gor Mahia ya Kenya.

Baada ya hapo, mwamuzi huyo aliichezesha Simba iliyokuwa ugenini dhidi ya Raja Casablanca ambapo Wekundu wa Msimbazi walichapwa mabao 3-1 Aprili 1, 2023 ikiwa ni mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi.

Katika msimu wa 2024-2025, alichezesha mechi ambayo Yanga iliichapa TP Mazembe mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Mkapa, ikiwa ni makundi Ligi ya Mabingwa Afrika iliyochezwa Januari 4, 2025.

Katika mechi moja aliyoichezesha AS FAR Rabat, timu hiyo ilifungwa mabao 2-0 na USM Alger hatua ya robo fainali Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2022-2023.

Kwa ujumla, refa huyo amechezesha mechi 49 za michuano mbalimbali ikiwamo ya kirafiki ngazi ya klabu na timu za taifa zilizo chini ya CAF na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).

Katika mechi hizo 49, ameonyesha kadi za njano 128 ikiwa ni wastani wa kadi 2.6 kwa mechi. Pia ameonyesha kadi za njano mbili, huku mikwaju ya penalti ikiwa tisa.

Mwamuzi huyo aliyezaliwa Julai 11, 1982 akiwa na umri wa miaka 43, alianza kuchezesha rasmi mechi zinazotambulika na CAF na FIFA Mei 23, 2017.

Wakati upande wa Yanga hali ikiwa hivyo, Simba imepewa mwamuzi kutoka Cameroon, Abdou Abdel Mefire mwenye umri wa miaka 29.

Mwamuzi huyo aliyezaliwa Agosti 2, 1996, unaweza kusema ni kama mgeni katika michuano ya kimataifa kwani ana mechi 17 pekee alizochezesha, akionyesha kadi za njano 62, kadi nyekundu moja na penalti mbili.

Alianza kuchezesha mechi za kimataifa msimu wa 2023-2024, ambapo Agosti 22, 2025, alikuwa mwamuzi wa kati Tanzania ilipofungwa bao 1-0 hatua ya robo fainali ya michuano ya CHAN dhidi ya Morocco kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar.

Pia aliichezesha timu ya taifa ya Tanzania chini ya miaka 20, katika mashindano ya AFCON U20 na kupoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Misri, Mei 9, 2025.

Mwamuzi huyo ndiye alichezesha fainali ya CHAN 2024, Morocco ilipoichapa Madagascar mabao 3-2 kwenye Dimba la Moi International Sports Centre nchini Kenya.

Simba iliyopo Kundi D, imepangwa na timu za Espérance de Tunis ya Tunisia, Petro de Luanda (Angola) na Stade Malien (Mali).