Salim: Hii ndo maana ya kauli mbiu ‘ Sauti ya kipa iheshimiwe’

KIPA wa Dodoma Jiji, Ally Salim amefafanua kauli mbiu anayopenda kuitumia ya ‘Kauli ya Kipa Iheshimiwe’ akieleza ni kutokana na ukubwa wa majukumu anapokuwa uwanjani kuhakikisha jicho lake linaona mengi ya kuwasaidia wengine.

Amesema kauli mbiu hiyo alianza kuitumia muda mrefu wakati akiwa Simba katika mechi dhidi ya Ihefu ambayo wekundu hao walishinda 2-0 Aprili 10, 2023 na mechi ya Dabi ya Kariakoo ambayo Simba iliifunga Yanga 2-0 Aprili 16, 2023 sambamba na pambano la CAF ambalo Simba ilipoteza 1-0 mbele ya Wydad.

“Kauli mbiu hiyo ni ya muda mrefu kabla ya kuanza kuaminiwa kucheza, nakumbuka nilianza kudaka dhidi ya Ihefu baada ya kipa namba moja, Aishi Manula kuumia ndipo watu wakaanza kujua nina kitu kama hicho,” amesema Salim na kuongeza; “Maana ya kauli mbiu hii ni kwamba kipa ndiye kocha wa uwanjani.”

SALI 01

“Ni kwa sababu kipa ana nafasi ya kuona kwa ukubwa kinachoendelea katika timu anayoichezea na akawasaidia wachezaji wenzake kuongeza umakini wa kutimiza malengo.”

Kocha huyo aliyetua Dodoma Jiji msimu huu baada ya kuachana na Simba alifafanua zaidi kwa kusema; “Kwa kifupi slogan hiyo inamhusu kila kipa kuongeza umakini muda wote anapokuwapo uwanjani na ndicho tunachoelekezwa na makocha wetu.”

Mbali na hilo alizungumzia ugumu wa Ligi Kuu msimu huu, huku imani yake kubwa ni Dodoma Jiji kufanya makubwa ingawa haijaanza vizuri katika mechi sita imeshinda moja, sare mbili na imefungwa tatu, ina pointi tano na ipo nafasi ya 14 katika msimamo.